Waziri Simbachamwene na Mchakato wa mahabusu kufanya kazi wakiwa Magerezani

Waziri Simbachamwene na Mchakato wa mahabusu kufanya kazi wakiwa Magerezani

Suley2019

JF-Expert Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2,203
Reaction score
5,628
J. W Nyoka katika Makala ya Kona ya Haki Jinai anaeleza:

Niliwahi kuandika katika moja ya makala zangu kwamba asiyefanya kazi asile, kwa wafungwa nikasema ni sawa, je, kwa mahabusu vipi, nao wasile?

Yawezekana andiko langu hilo limetoa tafsiri mbali mbali kwa wasomaji, na wiki iliyopita wakati wa shughuli zake za kawaida katika mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nchi George Simbachawene alikaririwa na vyombo vya habari wakati akizungumza na askari Magereza wa mkoa huo kwamba kuna mchakato unaoendelea wa kutaka mahabusu wakiwepo magerezani wafanye kazi kama wafungwa.

Kauli hii haikupokelewa vizuri na watu wengi, na nadiriki kusema sikuona hata mtu mmoja katika mitandao ya kijamii aliyeunga mkono hoja hii.

Aidha Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee alipata kusikika huko nyuma akisema pia itafikia wakati watawakataa mahabusu kuletwa Magerezani na kwamba Polisi wawashughulikie wenyewe huko huko!

Inaonekana suala la mahabusu ni kero kubwa katika uendeshaji wa Magereza na si kwa Tanzania tuu bali ni ulimwengu mzima. Kwasasa duniani kote kuna mahabusu zaidi ya million mbili na nusu(2.5m) katika jumla ya wafungwa 11million wakati Tanzania idadi ya mahabusu kwa wastani ni asilimia 54% ya wafungwa wote.

Suala hili la wingi wa mahabusu katika Magereza Tanzania ni la muda mrefu tunaweza kurudi nyuma hadi mwaka 1983ilipoundwa Kamati toka Ikulu kuchunguza sababu za msongamano magerezani na kutakiwa kutoa mapendekezo yao. Mwaka 1986 ikaundwa Kamati nyingine na (Task Force) Tume ya Kurekebisha Sheria ikawa chini ya Jaji Ernest Mwipopo.

Tume hii ndiyo iliyokuja na mapendekezo ya kuanzishwa kwa parole, pamoja na uanzishwaji wa utaratibu wa ufuatiliaji wa kesi kwa vyombo vya haki jinai uliofahamika kama Case flow management teams.

Bila kusahau juhudi za Rais Kikwete alivyotemebelea Magereza ya Keko Mwezi Mei 2006 na kuona jinsi mahabusi wanavyolala kwa zamu na kuita mlalo wa mzungu wanne.

Na msafara wa dharura wa Rais John Magufuli gereza Butimba Mwanza mwaka jana na baadae Waziri wa Katiba na Sheria Dr Augustine Mahiga pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka Biswalo Mganga zilisaidia kupunguza papo hapo mahabusu 75 kwa mara moja kwa hati ya nolle prosequi. Mahabuusu wengine 300 toka Bariadi, Mugumu, Tarime, Bunda na Kahama nao waliachiliwa baadae. Aidha na sheria mpya ya plea bargain nayo pia ilipunguza idadi ya mahabusu na hadi kufikia tarehe 27 Februari 2020, mahabusu nchi nzima walikuwa17, 396 na wakati wafungwa 14, 502. Hii inaonyesha jinsi gani serikali inajitahidi kulitatua tatizo hili amabalo bado ni pasua kichwa.

Sasa je, uwingi huu wa mahabusu unaozidi idadi ya wafungwa ni sababu tosha ya kuwafanya wafanye kazi gerezani kwa dhana ya Magereza kujitosheleza?

Sheria za nchi na za Kimataifa zinasemaje!
Inawezekana kabisa wale wengi waliokuja na mawazo ya moja kwa moja ya kumpinga waziri Simbachawene hawakumuelewa. Alichosema ni mchakato unaendelea kwahiyo sio mwisho kwani mwishowe itakuwa ndiyo au hapana.

Kuna baadhi ya masuala katika nchi huendeshwa kwa sheria za ndani na nje zile za kimataifa. Kwamfano, mpira wa miguu sheria za FIFA zinatawala huwezi kuchezesha wachezaji 12 wanjani, watu hawawezi kukuelewa.

Halkadhalika Haki Jina(Criminal Justice) inabanwa na sheria zetu za ndani kikatiba pamoja na zile za nje kama wanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Wanachama wa Jumuia ya Madola.

Katika Umoja wa Mataifa, kwa Haki Jinai kuna vyombo muhimu kama nchi inahusishwa na United Nations Crime Prevention and Criminal Justice, United Nations Office of Drugs and Crime, International Covenant on Civil and Political Rights(ICCPR) na United Nations Congress.

Aidha katika Umoja wa Afrika kuna chombo kinacho julikana kama African Commission of Human and Peoples Rights (ACHPR) ambacho Makao Makuu yake ni Banjul Gambia na hukutana mara mbili kwa mwaka.

Vyombo vyote hivi huhusika na masuala mazima ya Haki Jinai pamoja na Haki za Binaadamu na Utawala bora. Kwamfano suala la Wafungwa, United Nation Congress kwa kuputia UNODC ndio iliobuni sheria za kimataifa za uendeshaji wa Magereza tangu mwaka 1955 na kuziita Standard Minimum Rules for Treatment of Prisoners ambazo mwaka 2015 ulifanyika mchakato wa kuzirekebisha na kuziita Nelson Mandela Prison Rules na wanachama wote wanazitekeleza kwa kulingana na uwezo wa kila nchi wa kiuchumi, kisiasa na kijiografia. Lakini kimsimsingi yale mambo yote muhimu yanatekelezwa.

Inawezekana kauli ya Waziri Simbachawene iko katika misingi hio ya kuchakata kwanza huku nyumbani kisha katika ngazi mbali mbali za UN hadi kufikia kwenye Congress ambayo inafanyika mara moja kila baada ya miaka mitano. Mara ya mwisho UN Congress ilikuwa Quarter mwaka 2015 na mwaka huu ilikuwa iwe April lakini wameahirisha kutokana na homa kali ya mapafu COVID~19.

Kwa kuzingatia vyombo nilivyovieleza, wafungwa au mahabusu huhesabika kama watu wasiojiweza(vulnerable) kwakuwa wanawekwa chini ya ulinzi kisheria, magerezani na si kwa matakwa yao kwahiyo serikali inalazimika kuwahudumia kwa mujibu wa sheria za ndani ya nchi na zile sheria za kimataifa, Kanuni za Kadumu zaKudumu za Magereza No. 781 na Nelson Mandela Prison Rules Article 22.

Wafungwa waliohukumiwa wanalazimika kufanya kazi kwa mujibu wa Kanuni za Kadumu za Magereza No. 617 hadi 640 na Nelson Mandela Prison Rules Articles 96, 97 (1 hadi3) na pia wanatakiwa kulipwa katika utaratibu unaojulikana kama Prisons Earning Scheme kwa viwango vinavyo amuliwa na utawala, sheria za ndani Kanuni za Kudumu za Magereza No. 663 hadi 666 na zile za nje, Nelson Mandela Prison Rules Article 103.

Malipo haya ni muhimu kwani hupewa siku mfungwa anapotoka gerezani kama kianzio cha maisha au hata kununuliwa vifaa vya kuanzia kazi atokapo gerezani kuliko hali ilivyo sasa, wafungwa hutoka bila msaada wowote matokeo yake mwingine hawajui wende wapi na mwishowe kurejea magerezani(reoffending).

Kwa mahabusu hali ikoje? Mahabusu hakatazwi kufanya kazi na hashurutishwi kufanya kazi bali kwa afya yake zaidi ya mazoezi anayotakiwa kufanya pia anaweza kushawishiwa kufanya kazi ambayo kulingana na mazingira ya gereza ataona inamfaa. Sheria za kimataifa, Nelson Mandela Prison Rules zinasema ikiwa ataridhia, anaweza kufanya kazi na kulipwa kwa kiwango kinachokubalika na pande zote mbili. Sheria ya ndani ya Nchi, Kanuni za Kudumu za Magereza 617 na zile za nje, Nelson Mandela Prison Rules Article 116.

Katika nchi ambazo zimefanikiwa kuwashawishi mahabusu kufanya kazi ni Uganda ambapo baadhi ya mahabusu wanakubali kufanya kazi na wanashiriki katika uzalishaji mali.

Magereza ya Uganda kwakupitia gereza la Luzira lilitangazwa kuwa gereza bora katika Afrika mwaka 2014 kwa kuwatumia wafungwa kuzalisha mali na kuwezesha kupunguza gharama ya uendeshaji magereza kwa asili mia sabini70%, wakati huo huo kuwa na kiwango cha chini 32% cha urudiaji wa vifungo magerezani (reoffending).

Katika mkutano wa wakuu wa Magereza wa Afrika uliofanyika Mwezi May 2019 Burkina Faso, Uganda ilithibitisha hivyo kwa ubora wake katika shughuli zake za uzaliishaji mali na kuwa mfano mzuri wa Magereza kama chombo cha cha urekebishaji wa wafungwa kwa kuzingatia program za uzalashaji mali na utangamano na jamii.

Sioni tofauti kubwa na juhudi zinazoendelea sasa na Jeshi la Magereza nchini, ni suala la muda kabla Magereza Tanzania haijafika huko.

1591855931620.png

Rais Yowel Kaguta Museveni wa Uganda akikagua shamba la mahindi la Magereza nchini Uganda akiwa na Kamishna Jenerali wa Magereza Dr. Johnson Babashaija. Magereza Uganda inapunguza gharama za uendeshaji wa Magereza kwa 70% na kupunguza pia urudiaji wa wafungwa magerezani kwa 32%.​
 
Suley2019
... kwanza ijulikane kwamba kila mmoja ni mfungwa mtarajiwa; kila mmoja akiwemo waziri mwenyewe na huyo kamishna jenerali wa magereza waandae mazingira bora ya magerezani maana hawana uhakika na kesho yao!

Pili, je, mfungwa kufanyishwa kazi ni sehemu ya adhabu? Si hukumu inatamka "... unahukumiwa kifungo cha miaka XX na kazi ngumu"? Hivyo, kumbe kazi kwa mfungwa ni sehemu ya adhabu baada ya kutiwa hatiani na mahakama.

Kama ndivyo, kumfanyisha kazi mahabusu ambaye hajatiwa hatiani bado sio kumwadhibu kabla ya uthibitisho wa kutenda kosa? Hii kitu inatakiwa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu badala ya mihemuko au kiki za kisiasa!
 
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nchi George Simbachawene alikaririwa na vyombo vya habari wakati akizungumza na askari Magereza wa mkoa huo kwamba kuna mchakato unaoendelea wa kutaka mahabusu wakiwepo magerezani wafanye kazi kama wafungwa.
Viongozi wajizuie kutoa kauli tata, huyu Simbachawene ni mwanasheria, anapaswa kujua umuhimu wa maneno. "Kama wafungwa" ndio tatizo hapa. Ikiwa kutakuwa na mahabusu kuchagua kufanya kazi kwa ridhaa yake hakuna shida, lakini wafungwa hawana ridhaa.
 
Back
Top Bottom