Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Daraja la J.P Magufuli kati ya Kigongo - Busisi lenye urefu wa Kilomita 3 lililopo kati ya Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza.
Kufunguliwa kwa Daraja la Magufuli kunakwenda kuondoa adha kwa wananchi waliokuwa wanaipata kwa miaka mingi kutokana na Vivuko kuzidiwa na idadi kubwa ya magari na abiria wanaoelekea Mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma pamoja na nchi jirani Uganda, Burundi na Rwanda.
Ujenzi wa daraja hilo uliasisiwa na Hayati. John Magufuli, ambae alifariki Machi 17, 2021, ambapo daraja hilo likiwa limefikia 25% za utekelezwaji wake na mrithi wake, Rais Samia Suluhu Hassan amendeleza na hatimaye leo kukamilisha kwa asilimia 100.
Akizungumza katika uzinduzi huo Rais Samia ametoa agizo la kulindwa kwa daraja hilo kwa sababu ni mradi wa kimkakati na lazima uwe salama
"Nitoe agizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga kulinda daraja hili [JP Magufuli]. Hili ni daraja la kimkakati, ni la aina yake ndani ya nchi, lakini si la Tanzania peke yake, ni daraja ambalo pia litatumika katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, na hatuna budi kulilinda."
"Inafurahisha kuwa katika mradi huu [Daraja la JP Magufuli], asilimia 92 ya wafanyakazi walikuwa ni Watanzania, kwa maana ya wazawa wa Taifa letu. Hakika hili daraja lilitokana na wazo la Watanzania wenyewe, lililogharamiwa na Watanzania wenyewe, na lililojengwa kwa nguvu za Watanzania wenyewe. Hii ni fahari nyingine kubwa kwa nchi yetu." Amesema Rais Samia wakati akizindua daraja hilo
Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema watakaohitaji kutumia daraja la JP Magufuli kwa ajili ya kupiga picha au kurekodi video za muziki watalazimika kuomba kibali Wizara ya Ujenzi kupitia Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza.
msaka habari