BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 525
- 1,257
Ushauri huo umetolewa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Simai Mohamed Said wakati wa uzinduzi wa Hoteli ya Crowne Plaza jijini Dar es Salaam(an IHG Hotel), Novemba 26, 2022.
Akitolea mfano kuwa ni rahisi watalii wanaofika Dar kwenda Zanzibar au wanaofika Zanzibara kwenda Dar, na kwa kuwa usafiri mkubwa wa sehemu hizo ni ndege na boti, itapendeza mamlaka zote zikizingatia ubora wa huduma ili ikiwezekana wawe rafiki na mazingira yetu.
Amesema: “Niwaombe wasimamizi wa bandari ya Dar, wasimamie huduma nzuri kwa kuwa hiyo ni sehemu ya utalii, haitakiwi kuwa zogozogo kama vile wapo sokoni.
“Mkurugenzi Mkuu wa Bandari hayupo chini yangu lakini nashauri tu kwa kuwa Zanzibar tunaitegemea njia hiyo, sote pia ni Watanzania, mapungufu yetu tuyaseme wazi kwa pande pande zote mbili za bandari (Dar na Zanzibar) kwa faida yetu sote pia.”
Ameongeza kuwa kuongezeka kwa hoteli zenye ubora na gharama nafuu kama Crowne Plaza ambayo ina ‘brand’ kubwa Duniani kunazidi kuongeza nafasi kubwa ya kuwa na watalii wengi.
Amebainisha kwa kusema: “Sisi tuliopo katika Sekta ya Utalii tunaangalia fursa ambazo vijana wetu wanazipata katika mafunzo, siyo tu kujenga hoteli lazima tuwe na mazingira ya kutengeneza watu wetu kujifunza.
“Nashauri pia ikiwezekana yaanzishwe matamasha ambayo yanaweza kuwa makubwa kuunganisha wadau ili yaweze kuongeza wageni wengi, matamasha siyo lazima yawe ya mziki, inawezekana ikawa ni muziki lakini ndani yake kukawa na lengo la kuongeza utalii.”
Aidha, Waziri Simai amegusia Sera ya Uchumi wa Bluu kuwa haiigusi Zanzibar peke yake bali sehemu nyingi za Tanzania ikiwemo Tanga, Dar, Mtwara na kwingineko.
Amekemea matumizi mabahaya ya vyanzo vya maji kama kuvua Samaki kwa kutumia mabomu, akieleza kufanya hivyo ni kuharibu mazingira ya baharini na kuharibu maisha yajayo ya kizazi kinachofuata.
“Uchumi wa Bluu unatakiwa kufaidisha wananchi wa kawaida na Serikali, na hatuwezi kuendelea uchumi wa Bluu wakati kuna wenzetu wa sehemu nyingine fulani anatumia mabomu kutafuta Samaki.
“Utalii una fedha nyingi kuna mzunguko mzuri wa biashara, na ni biashara ambayo inatufanya tuwe wamoja, Watanzania tukiwa mabalozi wa sekta hii tutachangia kuongezeka kwa soko la utalii na kuongeza fedha ndani ya nchi,” amesema.