SoC04 Wenye elimu ya msingi wasigombee nafasi za Ubunge

SoC04 Wenye elimu ya msingi wasigombee nafasi za Ubunge

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
Dibaji.

Maisha ya Tanzania kwa miaka 30 nyuma hayalingani hata kidogo na maisha ya sasa katika kila eneo, iwe kimazingira, kiuchumi, kielimu, kiteknolojia, mitindo ya maisha na kilakitu.Na hii ni kwa dunia nzima, ndio maana kuna kitu kinaitwa historia, tafsiri yake ni kwamba maisha hubadilika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Yapo mabadiliko chanya na hasi yaani tunayoyafurahia na yale tusiyopendazwa nayo ,hivyo hatuna budi kuendana nayo. Hata kiutawala tunaona kila kipindi fulani kuna miswaada mipya inapitishwa kusudi kutengeneza sheria ambazo kimsingi zitatuongoza vyema kwa wakati husika.

Utangulizi.

Kwenye miaka ya 80 mtu aliyehitimu darasa la 7 alitambulika kama Msomi mwenye ufahamu na uwezo wa kutosha kuchukua hatamu yeyote ya uongozi Serikalini au kuwa na wadhifa mkubwa wa kuheshimika na watu. Mabadiliko yaliyochagizwa na maendeleo katika nyanja zote yalipelekea miaka ya 90 idadi ya wahitimu wa darasa la 7 nchini ikaongezeka, hivyo ikaonekana ni hatua ya elimu isiyo na tija.Hapo ndipo mwishoni mwa miaka ya 90 elimu ya Sekondari ikageuka kuwa ndio kipimo kizuri cha mtu msomi.

Miaka ya 2000 tumepiga hatua kubwa kama taifa kwenye nyanja zote hususani kwenye elimu, na hatimaye mtu msomi alitambulika kwa cheti cha kidato cha sita au vyeti vya chuo kwa ngazi tofauti tofauti yaani Stashahada, Shahada ya kwanza na kuendelea. Hivyo mtu akiwa na elimu ya ngazi hizo ndipo anaweza kupata nafasi ya kazi za ngazi za juu,Serikalini na hata Sekta binafsi.

Katiba iongeze sifa za mgombea Ubunge.

Kwenye mchakato wa kupata katiba mpya swala la kuongeza sifa za mgombea wa ubunge litiliwe mkazo ili kupata wawakilishi bora wa wananchi, wanaofaa kwa zama hizi.

Ikumbukwe Mbunge ni muwakilishi wa wananchi wote,yaani wasomi na wasio wasomi.Wakulima,wafanyabiashara,wafanyakazi na makundi mengine.

Na kwa mujibu wa katiba ya jamhuri wa Muungano wa Tanzania inabainisha….
View attachment 3021335
Nadhani kipengere (a), kinachosema awe anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza, inapaswa sasa iwe ‘Awe amehitimu kidato cha nne na anajua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza. Lazima tukubaliane uhalisia uliopo kujua kusoma na kuandika haithibitishi mtu anafaa kuongoza watu,tunahitaji mtu mwenye maarifa yanayoendana na zama hizi za dijitali.

Japo nafahamu elimu ya darasa la 7 au la 8 la zamani ilikuwa ina thamani kwa miaka michache nyuma kwa sababu ya mtaala uliokuwa bora. Lakini elimu ni mfumo rasmi wa kupata maarifa na ujuzi ili kukabiliana na mazingira yaliyopo.Hivyo hatupaswi kubeza hata kidogo muendelezo au maboresho katika mfumo wa elimu.

Kwa maana hiyo, kama kwenye jamii zetu kuna wasomi wengi ,basi si busara wakaongozwa na mtu mwenye elimu ndogo zaidi. Kuna msemo nauamini unasema “Akili ndogo haiwezi kuongoza akili kubwa.”

Sisemi muwakilishi wa wananchi awe na elimu ya ngazi za juu zaidi ,hapana nadhani angalau tuongeze sifa za mgombea awe na elimu ya kidato cha nne mpaka cha sita.Naamini atakuwa na uwezo wa uchanganifu na ufahamu wa mambo kadha wa kadha.

Yapo mengi ambayo kimsingi yanaweza kuongezwa kwenye sifa za mgombea wa Ubunge,mfano awe ameishi jimboni kwa asilimia kubwa ya maisha yake, na sifa zinginezo.Lakini kwa mtazamo wangu nimeona sasa ifike tamati ya wenye elimu ya msingi kugombea Ubunge.

Kwani ngazi hii ya elimu imepitwa na wakati katika uwakilishi wa wananchi kwa zama hizi.Ukizingatia Serikali yetu ina mahusiano mazuri na mataifa mengi ulimwenguni kote ,hivyo kuna Dira na taarifa nyingi zinatolewa,hivyo kama kiongozi anatakiwa awe wa kwanza kuzipata, kuzielewa, kuzihusishanisha na mazingira yake na kuzitafsiri kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara hadi kwenye utekelezaji wake. Kiongozi ni Nabii kwa watu wake ,hivyo lazima awe ni mbeba maono na siyo kilasiku awe wa kufundishwa na kukumbushwa wajibu wake.

Hali halisi.

Maisha ya sasa kiuhalisia mtu mwenye elimu ya shule ya msingi, ataishia kupata kazi za ulinzi na zinginezo ambazo kwa kifupi ni za hadhi ya chini. Kulingana na mahitaji ya sasa ,hakika elimu ya msingi haimsaidii mtu kuwa na ufahamu mkubwa, kwasababu tunahitaji maarifa na ujuzi zaidi ili tuweze kumudu mazingira tuliyonayo zana hizi za dijitali.

Japo ni vizuri muwakilishi wa Wananchi awe Moderate ,lakini zama zinabadilika ,leo hii kiwango cha elimu cha wastani sio darasa la 7 tena. Wabunge wa miaka ya nyuma ambao waliishia darasa la 7 ,waliweza kuongoza vizuri kwasababu ya uhalisia wa maisha ya wakati huo.

Nafahamu kuna aina ya uongozi ambao kitaalamu wanaitwa “Leaders by Charisma”, ni viongozi kwa asili ,pasi na kutegemea elimu.Lakini mahitaji ya maisha ya sasa yanahitaji kiongozi ambae ni taswira ya daraja kati ya wananchi na Serikali.Na nchi yetu imeendelea sana kwenye eneo la elimu.

Aina ya Mbunge anayeendana na zama tulizonazo, lazima awe mwenye maarifa na ujuzi wa kutatua changamoto kwa mipango-mikakati,pia ajue namna ya kutumia rasilimali ili kutengeneza fursa na kutatua matatizo, awe mwenye uwezo wa kuishawishi Serikali kusaidia jimbo analoongoza kwa hoja tunduizi akiwa bungeni,awe mwenye kujua hali za wananchi wake kwa maana ya kuwa mtafiti na mwenye mahusiano mazuri na watu wa hadhi zote. Atumie vizuri fedha za maendeleo ya jimbo kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi pamoja na uzoefu wake.

Na kimsingi kila jimbo linatamani kutoa Waziri ,na Rais hawezi kumteua Mbunge kwa sababu ana mvuto kisiasa,anazingatia weledi wake.

Pia yapo majadiliano yenye mashiko zaidi kama yale ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yaliyofanyika 2021 , hapa kiuhalisia wanahitajika wawakilishi wenye ufahamu mkubwa wa uchanganuzi na kuzua hoja tunduizi.Mpango huu wa tatu wa kutekeleza dira ya Maendeleo ya Taifa unahitaji utashi wa kisiasa katika ufanisi wake.

Ukifuatilia bunge letu tukufu utagundua changamoto nyingi zinazotokana na kukosa elimu ya kati au ya juu,hasa pale wabunge wanapouliza maswali yao. Kwanza kuna mapungufu katika kujenga hoja,kuna makosa ya matamshi na sarufi kwa ujumla, namna wanavyosikika unang’amua kabisa kuna shida ya ujuzi wa kimawasiliano (Communication skills.), lugha ya kingereza imekuwa ni mtihani mkubwa kwa wabunge walio wengi,japo si lugha ya taifa lakini ndio lugha ya kimataifa,kuna kukosa namna sahihi ya kutia utani kidogo badala yake huzua taharuki,vicheko visivyohitajika kwa waheshimiwa, hupelekea kutojua kutumia muda vizuri ambao Spika wa bunge anawapa.Hayo ni baadhi tu ya mapungufu.

Yapo madhara ya kuwa na Wabunge wenye elimu duni.

Wakati tunawapitisha Wabunge wenye elimu ya msingi, tukumbuke pia Rais anawateua Mawaziri wasomi ili washirikiane nao katika kutatua changamoto za wananchi na kuchochea maendeleo ya nchi.Hapo ndipo kunatokea migongano na kutoenenda sambamba katika utekelezaji wa maazimio,chanzo chake ni kuzidiana kwa kiwango kikubwa cha maarifa.
  1. Hawawezi kujenga hoja tunduizi ili kuishawishi serikali iweze kutazama kwa jicho yakinifu mazingira ya majimbo yao.Athari zake ni jimbo kutozingatiwa na Serikali katika miradi ya kijamii.Mwishowe maendeleo huchelewa na wananchi kuishi maisha duni na kuilalamikia Serikali ya chama tawala.
  2. Hushindwa kung’amua vipaumbele vya Wananchi kwenye maeneo yao.Ni wazi kila jamii ina mahitaji yao ya msingi japo yapo maeneo sensitive ,lakini mbunge lazima awe na jicho pevu na msikivu kwa wananchi.
  3. Hushindwa kuwatafsiria wananchi sera za serikali na Dira ya Serikali kwa wakati husika kusudi Wananchi waelewe na kuepusha migogoro kati ya Wananchi na viongozi wao.
  4. Kuwa na mawazo mgando, kwa maana ya mapungufu ya maarifa na ujuzi .Wakati mahitaji ya zama tulizonazo ni kuibua mawazo yenye kutatua changamoto mpya na zijazo, lakini kwa mtu mwenye elimu duni ana mipaka katika fikra zake.Hivyo hukosa sifa bora ya muwakilishi wa Wanannchi kwa Serikali.
  5. Kushusha heshima ya bunge kwa wafuatiliaji.Kimsingi bunge ni chombo kinachoaminika na kuheshimika na wananchi kwa mamlaka ilio nayo ya kupokea miswaada na kutunga sheria ,pamoja na kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa kila mwaka.Hayo ni baadhi ya majukumu mazito ya bunge.Kwahiyo tunapowaingiza wabunge ambao wana maarifa madogo ni kulikosea heshima bunge tukufu.Matokeo yake uvunjifu wa maadili na kuzua taharuki kunajitokeza mara kwa mara bungeni.
  6. Kuongezeka kwa matukio ya rushwa katika mchakato wa uchaguzi mkuu.Iko wazi wagombea wasomi wana hoja tunduizi na wana nguvu ya ushawishi kwasababu ya elimu.Hivyo, maranyingi wasio na elimu silaha yao kubwa ni kutoa fedha ili wachaguliwe,hapa ndipo napata mashaka japo wapiga kura ndio waamuzi lakini fedha ina nguvu kubwa.Zaidi, urasimu katika mchakato wa kuwapata madiwani, huyu Mbunge huwa na hofu juu ya diwani mwenye elimu kwahiyo humlazimu kuhonga ili kuwaweka madiwani anaowamudu.
  7. Kukosa viongozi bora wa kitaifa, kama Bungeni ndipo sheria hutungwa basi sidhani kama ni busara kuwa na wawakilishi wenye maarifa madogo ,kulingana na uzito wa mambo yanayo jadiliwa.
  8. Aidha, kukosa njia madhubuti za kutatua migogoro ya wananchi na changamoto mbalimbali.Wengi wao wanaamini katika kufuatwafuatwa majumbani ili kusikiliza kero za wananchi ili watoe fedha au amri kwa wadhifa walionao ,amri kwa maana kuwapigia simu baadhi ya watumishi ili kutatua changamoto.Lakini Wabunge wasomi daima hutoa suluhu endelevu kupitia miradi na usimamizi mzuri ,pia hutoa mashauri jengefu kwa wananchi, ili wananchi wasiwe na utegemezi siku zote.
Hitimisho.

Sambamba na hilo la kuongeza vigezo vya wagombea wa Ubunge hasa kwenye eneo la elimu,pia kuwepo na mkakati wa Wabunge kuongeza elimu-saidizi pindi wanapoingia madarakani.Ni elimu maalumu kupitia kozi za muda mfupi ili kuwaimarisha zaidi Wabunge waweze kumudu majukumu yao. Mfano wa kozi hizo ni kama,Communication skills,Community healthy,Community Development,Laws na short courses zinginezo sambamba na Work Ethics.Lakini isiwe ndio sababu ya kuwaingiza wabunge wenye elimu ya msingi.

Asante kwa muda wenu.

Nawasilisha.
 

Attachments

  • 206DE5B2-267C-4040-BC2A-CE7AF3A26288.jpeg
    206DE5B2-267C-4040-BC2A-CE7AF3A26288.jpeg
    268.7 KB · Views: 6
Upvote 5
Back
Top Bottom