Kwanza niwashukuru wachangiaji wote katika mada hii na mambo mengi nimejifunza na ninaamini kama watawala wetu wanapitia hapa kujifunza (siyo kuchunguza nani ni nani) wao pia yawezekana wamejifunza kitu au zaidi.
Maendeleo yana gharama
Mojawapo ya nyaraka muhimu sana ambazo tumewahi kuzipata katika Tanzania ni maandishi ya hotuba mbalimbali za Mwalimu ambayo yaliwekwa kwenye vitabu viwili "Uhuru na Maendeleo" na "Binadamu na Maendeleo". Ndani yake kuna elimu kubwa sana ya kuweza kujenga hoja juu ya dhana nzima ya maendeleo. Katika vitabu hivyo kama vichwa vyake vya habari visemavyo vimejenga hoja nyepesi; kwamba Uhuru wa mwanadamu unahusiana moja kwa moja na maendeleo yake - yaani mwanadamu asiye huru hajaendelea. La pili ambalo ni jambo ambalo naamini bado Mwalimu alikuwa mbali sana ni kuwa lengo la maendeleo yoyote yale ni mtu. Maendeleo yasiyo muendeleza mtu kumudu mazingira yake ni maendeleo ya vitu. Maendeleo ni lazima yalinde utu wa mtu.
Ndio maana utaona kuwa Marekani licha ya kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumu haishikilii nafasi ya kwanza katika index ya Maendeleo ya Binadamu (Index of Human Development Report). Hivyo, ni lazima turudi kwenye misingi ya vilivyo muhimu katika maendeleo na hapa namba moja ni WATU.
Ubunifu, uvumbuzi, na ufundi ni kichocheo cha maendeleo
Katika kuleta maendeleo ya watu basi tunajikuta hatuna budi pia kuendeleza vitu; kwa sababu mtu na vitu kuna uhusiano wa moja moja tangu milenia na milenia. Ni pale mwanadamu alipoweza kuboresha kisu chake cha jiwe na kuanza kutumia cha chuma ndipo alivyoweza pia kuboresha maisha yake; ni pale alipoweza kubuni gurudumu (wheel) ndivyo mambo mengi ya mabadiliko ya viwanda yalipoanza kufanyika na zana nyingine nyingi kufuatia. Hivyo, mwanadamu anapoendeleza vitu kwa lengo la kuboresha na kurahisha maisha yake ndivyo anavyojikuta anaendelea.
Hata hivyo mara nyingi huko nyuma mambo mengi yalitokana na vipaji vya mtu na matokeo ya nasibu. Maendeleo ya sayansi hata hivyo yaliongoza kwenye dhana nzima ya kukaa na kufanya utafiti. Lengo la utafiti basi ni kugundua vitu na kuviboresha kwa kufuata kanuni za kisayansi na endapo jambo jingine la kinasibu linatokea basi linatokea kwa sababu ya juhudi hizo mahususi.
Ni kwa sababu hiyo, utaona kuwa nadharia za sumaku, kanuni za mwendo, na kanuni nyingine za sayansi zilibakia kuwa kanuni tu hadi pale zilipoanza kuwa applied katika maendeleo ya teknolojia. Hivyo haitoshi kujua sayansi au elimu ya darasani bila kuweka mkazo katika applied science.
Ni kwa misingi hiyo basi utafiti unahitajika kwa sababu hauwezi kutenganishwa na maendeleo. Tatizo letu naamini ni kuwa tunataka kuendelea lakini tunataka wengine ndiyo wafanye utafiti na kubuni vile vitakavyotuendeleza.
Nurujamii, hapo nyuma katoa mfano rahisi tu, kuhusu kwanini tunawatafuta wajapani kuja kutufanyia utafiti suala la msongamano wa magari Dar? Hivi hatuna wataalamu ambao wanaweza kuangalia data zile zile na kujaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu na hata kubuni visivyokuwapo? Ni lazima tujenge uwezo wa kujiamini.
Wiki kadhaa kuna mtu alibandika hapa picha ya mtasha mmoja akitoa maelezo kwa watendaji wa kata fulani jinsi ya kukabiliana na tatizo la uchafu katika mazingira yetu; nilijihisi kichefu chefu!
Gharama ya kwanza ni watu
Hatuwezi kuendelea bila kulipa gharama ya kuendeleza watu watakaobeba jukumu la kusimamia utafiti na ubunifu nchini. Katika hili ni lazima tudhamirie kuendeleza rasilimali watu (human resources) na hapa nina maana ya kuendeleza the "best brains" in Tanzania.
Huwezi kuwa na mtafiti Chuo Kikuu ambaye anapokuwa maabara baadala ya kufikiria "panya wake wa maabara" anajiuliza kama maji yatapatikana nyumbani au kama piki piki yake inahitaji matengenezo. Ni lazima siyo tu kuwaenzi wanasayansi wetu lakini kuwatendea bora zaidi ili jambo kubwa na la pekee wao kuhangaika nalo kichwani liwe ni utatifi na utafiti tu. Hii ni gharama ambayo hadi hivi sasa hatuko tayari kuilipa.
Tuanze na kizazi kipya cha watafiti
Naamini kuwa miaka kadhaa iliyopita tumeenda kombo na tumechepukia pembeni. Tumetegemea watafiti toka nje na utafiti toka nje. Leo hii kutokana na teknolojia ya mawasiliano vijana wetu wanaweza kujikuta wana"kopy" na kupaste tafiti za watu wengine huku wakibadilisha majina ya mada na kuyafanya zionekane ni za kwao. Sijui kuna utaratibu gani wa kuangalia tatizo la plagiarism katika mambo ya utafiti nchini.
Nakumbuka jinsi tulivyokuwa tunapewa zile "project" na kwenda kuzifanyia utafiti na kuandika report bila ya kuwa na internet wala nini. Tulijifunza then kanuni mbalimbali za kisayansi za kufanya emperical analysis ya data. Leo hii unaingia kwenye google na kupata analysis waliofanya wengine!
Ni kwa sababu hiyo naamini ipo haja ya kurudi nyuma na kuanza kuteka mioyo ya vijana wetu na kuwachochea kwenye sayansi na utafiti. Tusipoteze mawazo ya vijana na kuwaacha wakimbie masomo ya sayanasi na wale walioko kwenye sayansi kujikuta kuwa "sayansi hailipi". Nakumbuka rafiki yangu mmoja alikuwa anapenda hesabu sana na alikuwa anazikokotoa kama mtu anavyo gigida maji; baada ya kwenda Chuo Kikuu badala ya kuendelea na hesabu alizokuwa anazipenda akaamua kuswitch na kwenda BCom kwa ajili ya ajira zaidi ingawa mwenyewe angependa kufanya utafiti wa mambo ya hesabu zaidi. Sijui ni wangapi ambao walijikuta wanaacha michepuo ya sayansi na kuingia sanaa.
Nitawapa mfano binafsi; nilipokuwa kidato cha nne nilikuwa nafundisha Fizikia ya kidato cha pili na nilifundisha (nikisaidiana na mwalimu wangu mkuu aliyekuwa mwalimu pekee wa physics) karibu term nzima. Nilikuwa napenda Physics lakini si kemia. Hata hivyo nilipoendelea na kidato cha tano na sita (licha kufaulu Fizikia na kufeli hesabu - don't ask me how)nilijikuta sina combination yenye akili na kuamua kuishia kufanya HGE na nilipoenda Chuo nikachukua masomo ambayo hayakaribiani na HGE!!
Sasa naamini kama kungekuwa na jinsi ya kuendelea na Physics nadhani ningeenda mbali zaidi; siku hizi nasoma mambo ya physics kama hobby tu nikiishia kutamani.
Je tuwapoteze vijana wetu namna hii? Naamini wakati umefika wa kuanzisha High Schools za sayansi tu na teknolojia ambazo zitakuwa ndiyo vitovu vya wanafunzi wanaoenda Vyuo Vikuu kusomea sayansi. Shule kama Iyunga, Ilboru, Usagara, Bwiru, Mzumbe, n.k zinaweza kugeuzwa na kuwa shule za Sayansi na Teknolojia (siyo za wenye vipaji tu).
Shule hizo siyo tu zibadilishwe kuwa za sayansi lakini ziwezeshwe kufanya sayansi na utafiti na kuchochea wanafunzi wao kuwa wabunifu wakichezea maabara usiku kucha na mchana kutwa. Wakitoka hapo wanaenda kwenye Vyuo Vikuu vya Sayansi na Teknolojia kama MIT, DIT AIT, na Tanga Tech etc. Wale wanaobobea kutoka vyuo hivyo ndiyo wanapewa ofa ya kungia katika National Labs na ofa yenyewe lazima iwafanya wajisikie wanathaminiwa. Hii ni gharama ambayo lazima tuilipe kwa sababu tunaweza.
Hakuna njia ya mkato ya maendeleo endelevu
Tunaweza kutumia njia ya mkato ya kuendeleza vitu tu; lakini kama tunataka maendeleo ya kweli hatuna budi kuendeleza watu wetu. Leo hii hizi milioni 700 tukazotumia kujenga barabaraba na miundo mbinu zinaonekana zina lengo zuri. Lakini endapo tukio la kimungu au la kiasili likitupiga na kuharibu barabara na miundo mbinu hiyo ni nini tulicho nacho cha kushikilia? Itabidi tuombe tena misaada ya kujenga tena barabara hizo.
Leo hii barabara zinazotengenezwa hapo Dar na sehemu nyingine zikiharibika tunatafuta tenda tena za wataalamu toka nje waje watutengenezee. Tusipoweza kuendeleza watu wetu tutaendelea kuwa na maendeleo tegemezi; yaani yale yanayotegemea misaada na utaalamu toka nje.
Naomba niishie hapa kwa sasa..