Saa Mohamed
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa makusanyo ya fedha kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo, mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru amesema muda wa kuzungumzia suala hilo bado baada ya familia yake kuhusishwa katika makusanyo ya fedha kituoni hapo.
Waziri Pinda alitoa agizo hilo baada ya kutembelea kituo hicho na kustushwa na taarifa za mapato, akisema kuna harufu ya rushwa katika uendeshaji mzima wa stendi hiyo inayotumiwa na mabasi yatokayo na yaendayo nje ya Dar es salaam.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, mshauri huyo wa rais wa masuala ya siasa alisema kwamba, hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa muda muafaka haujafika.
Pia, Kingunge, ambaye amefanya kazi katika serikali zote za awamu nne zilizopita, alisema haamini kama Waziri Pinda alitoa tamko kama hilo, lakini hakuwa tayari kuendelea kufafanua kwa maelezo kuwa muda muafaka haujafika.
"Kwanza napenda nikusahihishe kuwa tamko hilo halikutolewa na Pinda, hivyo sina maoni na nasema tena sina comment kwa hilo," alisema Kingunge ambaye anaaminika kuwa ni mmoja wa waumini wazuri wa siasa ya ujamaa.
"Muda wa kuzungumzia suala hilo, bado haujafika. Ukifika nitasema."
Waziri Pinda hakuitaja familia ya Kingunge wakati alipokuwa akitoa maagizo hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake jijini Dar es salaam, lakini taarifa za mapato zilizotolewa wakati alipotembelea kituo hicho zilimstua.
Kituo cha mabasi cha Ubungo kinaendeshwa bila ya bodi wala kamati ya uendeshaji na kina mkataba na kampuni binafsi ya kukusanya malipo ambayo huigawia Halmashauri ya Jiji kiasi cha Sh1.5 milioni kila siku.
Lakini Pinda alisema kiwango hicho ni kidogo kwa kuwa kuna mabasi mengi yanayoingia kituoni hapo na kutoka.
Alisema kuwa kiasi cha ushuru kinachokusanywa kituoni hapo hakilingani kabisa na hali ilivyo kwa kuwa kuna idadi kubwa ya magari yanayotumia kituo hicho tofauti na mapato.
"Taarifa niliyopewa nilipofika katika kituo hicho ni kwamba ushuru unaokusanywa kwa siku ni Sh1.5 milioni hata kama kuna idadi kubwa ya magari, sasa tujiulize fedha nyingine zinakwenda wapi," alihoji.
"Hatuwezi kuvumilia hata kidogo
tumeamua kumuambia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aende afanyie kazi suala la makusanyo ya soko la Kariakoo na kituo cha mabasi cha Ubungo; atupe ripoti baada ya kuchunguza mambo yanavyokwenda."
Kutokana na malalamiko mengi aliyoyapata kwa wafanyabiashara mbalimbali katika kituo hicho, Pinda alisema kuna haja ya kuchunguza hali halisi ya utendaji na uendeshaji wa kituo hicho.
Alisema pia kwamba, hana hakika ushuru wa maduka, baa na vibanda vya biashara vilivyozagaa ndani ya kituo hicho unalinufaisha jiji au watu binafsi.
Alifafanua kuwa inawezekana kukawa na vikwazo vya kisheria katika masuala ya mikataba, lakini akasema mikataba isiwe kikwazo cha kupatikana kwa huduma bora zinazokidhi matakwa ya wananchi na kuwa na tija kwa serikali