Katika orodha ya wanaotajwa kuwania uteuzi wa ccm kwa nafasi ya urais wa JMT-2015, namba mbili (2) katika nisio shawishika nao ni Mh. Bernard Membe. Mh. Membe hanishawishi kuwa anastahili nafasi hiyo kwa sababu zifuatazo:
- 1. Historia halisi ya utendaji wake kama Mbunge na Waziri haina matokeo yanayosimama kumshuhudia Mh.Membe kama mtu wa kuleta mabadiliko chanya au maendeleo.
Asiyeweza katika dogo, ataweza katika makubwa? Mbele ya wapigakura wa Jimbo la Mtama, Mh. Membe anaonekana kama mtu aliyeshindwa kutimiza ahadi zake za muhula wa kwanza (2005-2010). Na walio wengi hawaoni umuhimu/mchango wa ukaribu wake na serikali katika kuwaletea mabadiliko. Ndo maana Mh. Membe alipata wakati mgumu sana kutoka kwa mgombea wa TLP, mtu ambaye hakuwa na jina, mali wala pesa bali support ya wananchi. Lakini kwa kutumia utaalamu aliojaaliwa, Mh. Membe aliweza "kumshughulikia" na kumdhibiti mpinzani huyu pekee na kuhakikisha wapiga kura wanakosa chaguo mbadala wakati wa uchaguzi. Ninashawishika kufikiri kuwa hata mpinzani mmoja angepenya na kusimama, matokeo ya Jimbo la Mtama yangekuwa sawa na ya Nyamagana.
Kuna jambo moja ambalo Mh. Membe ameshiriki na watu wasio na kumbukumbu nzuri au wafupi katika kuchambua mambo wanaweza kusema kalifanikisha. Ni suala la kurejeshwa kwa fedha za rada kupitia serikali badala ya NGOs kama wezi walivyotaka. Hii haiwezi kuhesabika kama jitihada ya Mh. Membe wala serikali ya Tanzania. Hili silielezi kwa ufasaha ili watu wajadili……………………..
- 2. Misingi ya mbinu anazotumia Mh. Membe katika kusaka kuungwa mkono na makundi yenye ushawishi mkubwa katika jamii haina maslahi kwa Taifa na inatengeneza viporo vya uporaji wa rasilimali za nchi na migogoro mikubwa ya kijamii hapo baadae.
Mathalani, katika suala la serikali kuanzisha na kuendesha Mahakama ya Kadhi na serikali ya JMT kujiunga na OIC, Mh. Membe akiwa mbele ya waandishi wa habari amekuwa akiwaondoa hofu wahusika kuwa haya mambo hayana shida na serikali iko katika hatua mbalimbali za kuyatekeleza. Mara tu upande wa pili wakianza kupaza sauti za kupinga, Mh. Membe hu-haha na hukimbia kimya kimya kwenda kwa viongozi wakuu wa upande wa pili "kutuliza mambo" kwa kificho. Katika hili, Mh. Membe anataka kuuma na kupuliza na ni ndumila kuwili. Ni vema, si kwa Mh. Membe tu, bali wanasiasa wote kuimarisha msingi wa msimamo ambao umekwishafikiwa na serikali katika suala hili nyeti.
Mh. Membe anasimama miongoni mwa viongozi wa Bara la Afrika waliosimama kidete kuomboleza kifo cha Shujaa wetu Mummar Gadaff. Lakini nyuma ya kilio na maombolezo ya msiba huu, kumefunikwa giza totoro la vitendawili juu ya nini haswa "majonzi" ya Mh. Membe? Wako wanaotoa nuru ili kutegua vitendawili kwa hadithi tofauti tofauti ambazo kwa ujumla wake ukizikusanya kwa ushambuzi makini unapata picha pana juu ya makubaliano/fadhila za utawala uliongushwa Libya kwa mgombea mtarajiwa. Watanzania tunapaswa kuwa tumejifunza madhara ya wagombea wetu kufadhiliwa na matajiri (nchi au mtu binafsi). Tutumie 2015 kuepuka kurudi chini ya utawala wa waliofadhili wagombea katika chaguzi kuu.
Mh. Membe anapigania uraia wa nchi mbili. Kwa faida ya nani? Binafsi sioni kama hili jambo lina tija kwa Taifa lenye uchumi unaomilikiwa na asilimia mbili (2%) ya wananchi wake na ndio asilimia tisini na nane (98%) ya hao hao tayari wana uraia wa nchi zaidi ya mbili. Hapa Mh. Membe hasimami kutetea rasilimali watu za Watanzania walioko nje bali kutafuta kuongeza wigo wa kuungwa mkono na watu wasiokuwa na uchungu wa nchi hii. Hawa tunaowaita "Watanzania wenye asilia ya Kihindi" ambao ndo wanashawishi sana suala hili tayari wanao uraia Uswizi, Canada, Marekani na hapa kwetu kutokana na udhaifu wa idara zetu za uhamiaji wanaishi na kufanya wanalotaka kwa jeuri ya pesa yao.
Nahitaji kushawishiwa kwa historia na utendaji upi Mh. Membe anastahili kuomba ridhaa ya kubeba bendera ya ccm katika uchaguzi mkuu 2015. Michango yenu ikiwemo matusi na dhihaka vinakaribishwa. Na kuwa na hakika, nitavipokea vyote kama vilivyo. Kwa namna ya pekee nausubiri mchango wa MBOPO, mtu ambaye mara nyingi hujitahidi kujibu hoja na si kujadili mtoa hoja katika kumtetea Mh. Membe.
Nawatakia Mwaka Mpya Mwema na Wenye Mafanikio.
Omutwale kutoka Kanyigo.