Na Mhashamu Baba Askofu Bagonza.
UZOEFU TOKA ARGENTINA
Wiki hii tumepokea ripoti tatu zinazofanana. Kwanza, iliyokuwa hotel maarufu ya Grudoto kubadilishiwa matumizi na kuwa bweni la chuo katikati ya kampeini za kitaifa kuboresha utalii. Kama tujuavyo, utalii unahitaji hotel nzuri. Pili, mgogoro kati ya kiwanda cha Dangote na benki ya RSK unaotishia kufunga kiwanda hicho muhimu katikati ya uhaba mkubwa wa saruji nchini. Tatu, tangazo la kufungwa kwa kampuni ya New Habari Corporation kutokana na kushuka sana kwa mauzo ya habari. Kama ni kweli, hili ni pigo kwa soko la ajira rasmi na isiyo rasmi katikati ya kilio kikubwa cha ajira nchini.
Siku za karibuni nilitembelea jiji kubwa la Buenos Aires huko Argentina. Niliweka kambi hotel kubwa iitwayo Gradiose Hotel. Ina vitanda zaidi ya 600.
Dakika chache baada ya kuingia chumbani, alikuja Meneja Mkuu na kuomba kuongea nami kwa dakika chache. Aliniambia yafuatayo:
1. Mwenye hotel aliamua kuuza hotel na kuacha biashara kwa sababu ilikuwa inatengeneza hasara.
2. Wafanyakazi wapatao 300 pamoja na watoa huduma kwa hotel (suppliers) waliungana na kufungua kesi kumzuia mwenye hotel kuiuza.
3. Walishinda kesi lakini kwa masharti kuwa wamlipe mwenye hotel fedha anazohitaji kila mwezi.
4. Wafanyakazi na watoa huduma walikutana na mwenye hotel na kukubaliana wao kuendesha hotel na kumlipa kiasi walichokubaliana kila mwezi.
5. Wafanyakazi walikutana na kukubaliana kupunguza mishahara yao na kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha wanabaki kwenye ajira (bora kupata kidogo lakini uwe kazini).
Baada ya kunieleza hayo akaniomba mambo matatu:
1. Kuzima taa kila ninapotoka nje ya chumba.
2. Kubadili taulo na mashuka kila baada ya siku moja badala ya kila siku.
3. Kufunga maji wakati wa kujipaka sabuni ninapooga na ya kuyafungulia ninapoyahitaji tu.
Alisema nikifanya hivyo nitaokoa fedha na ajira za watu. NILIKUBALI akaondoka.
Tunajifunza nini?
Kila mtu afikiri na kutafuta majawabu. Kufunga kiwanda, kufunga hotel, shule, chuo, kiwanda nk si kumkomoa mmiliki. Wamiliki walio wengi tayari wana hela ya kula, nyumba za kuishi, matibabu, na watoto wao wanasoma. Anayeumia ni serikali anayelazimika kushughulika na wahanga wa kufungwa kwa taasisi hizo. Hata wamiliki wakipelekwa jela, itaongeza ajira ya maaskari magereza na order yangu bunduki na risasi za ziada.
Mkweli kwa Mungu na Taifa langu.