Monday, 20 December 2010 23:53
0
digg
Waandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, anadaiwa kufichua siri za Rais Jakaya Kikwete kwamba kiongozi huyo wa nchi asingependa vigogo serikalini kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa. Kadhalika, mkuu huyo wa Takukuru anadaiwa kushindwa kuwafikisha mahakamani vigogo waliohusika na kashfa ya rada kwa sababu anahofia usalama wake, gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti juzi.
Mbali na hofu hiyo, gazeti hilo pia lilieleza juzi kuwa Dk Hoseah alipewa maelekezo maalumu na Rais Kikwete kutoshughulikia kesi za rushwa zinazowahusu vigogo katika serikali yake na hasa marais waliomtangulia. The Guardian lilitoa taarifa hiyo likiunukuu mtandao wa habari wa WikiLeaks uliojizolea umaarufu duniani kwa kutoa habari za kiuchunguzi hasa baada ya mwasisi wake, Julian Paul Assange, kutiwa matatani.
Kwa mujibu wa habari hiyo, Dk Hoseah, alisema hayo Julai 14 mwaka 2007, alipokuwa akizungumza na mwanadiplomasia wa Marekani, Purnell Delly jijini Dar es Salaam. Alisema uchunguzi wa kashfa ya rada ni hatari kwake kwa kuwa vigogo nchini, hawaguswi kwa tuhuma na kwamba tayari alikuwa ameanza kupata vitisho.
Akizungumza kwa huzuni na kusononeka, Dk Hoseah alidai kuwa kwa ari na utashi alionao katika vita dhidi ya ufisadi, angeweza kuwafungulia mashtaka watuhumiwa wa ufisadi, lakini ameshindwa kwa kuwa kesi hiyo inawagusa vigogo kadhaa, wakiwamo marais na waziri mkuu mstaafu na ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). "Biashara hiyo chafu iliwahusisha maafisa kuanzia ngazi ya Wizara ya Ulinzi na afisa mmoja au wawili wa ngazi za juu ndani ya jeshi, The Guardian lilieleza likinukuu vinasa sauti vya ubalozi huo.
Dk Hoseah alitumia mkutano huo kueleza mafanikio ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa na kueleza kuwa matumaini yake ya awali kusimamia mkakati huo, yamevunjwa moyo. "Alituambia waziwazi (rais) kwamba tuhakikishe kesi inayomhusu rais au waziri mkuu na viongozi waliomtangulia, tusiziguse na ziwekwe chini ya meza," lilieleza gazeti hilo katika taarifa yake.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zake ndogondogo, mtu yeyote aliyewahi kuwa rais wa nchi hawezi kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zozote zinazomkabili.
Lakini, wadau kadhaa wa masuala ya siasa, sheria, haki za binadamu na utawala bora wamekuwa wakiendesha harakati za kudai katiba mpya ambayo pamoja na mambo mingine, wametaka iondoe kinga ya rais ya kutoshitakiwa mahakamani hata mara baada ya kustaafu kwenye nafasi hiyo.
Kuna taarifa za ufisadi ndani ya Beki Kuu ya Tanzania (BoT). Pia Visiwani Zanzibar kuna mambo mengi yanayohusiana na rushwa na ufisadi,"alinukuliwa Dk Hoseah ambaye alieleza kuwa anaamini maisha yake yatakuwa hatarini iwapo atathubutu kuendesha uchunguzi huo.
Taarifa hizo kutoka kumbukumbu za vinasa sauti vya ubalozi wa Marekani nchini, zimeeleza kuwa katika mazungumzo hayo, Dk Hoseah alikuwa anarudia na kusisitiza kuhusu usalama wake, akisema anaamini maisha yake yapo hatarini kwa sababu alishapokea ujumbe wa vitisho kupitia simu yake ya mkononi na barua. "Amesema (Dk Hoseah) amekuwa akikumbushwa mara kwa mara kwamba katika vita hiyo ya ufisadi, anapigana na matajiri na wenye nguvu katika vita dhidi ya ufisadi,gazeti The Guardian lilimnukuu Delly, afisa huyo wa Marekani aliyekuwa akizungumza na Dk Hoseah.
Imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa sababu kubwa ya Dk Hoseah kujaribu kutia mguu kwenye sakata la rada ni taarifa ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuchunguza Ufisadi ya Uingereza (SFO), ambayo ilieleza kinagaubaga kuhusu kesi hiyo. Delly alisema, Hoseah amekuwa akionywa katika vitisho hivyo kwamba anaweza akaiona chungu nchi yake ikiwa ataendelea na mapambano hayo.
"Alisema (Dk Hoseah), ukihudhuria mikutano ya ndani na vigogo wa serikali, wanataka wakuone ukijihisi kwamba wao ndio wamekuweka katika cheo chako, lakini ukiwa mbishi wa kushikilia misimamo yako tu, basi uko katika hatari, gazeti hili lilimnukuu Delly. Awali akizungumza na gazeti hili, Dk Hoseah alikiri kupata vitisho vinavyohatarisha maisha yake kutokana na mapambano yake dhidi ya rushwa, lakini akasema hajaiona habari hiyo iliyonukuu mazungumzo yake na mwanadiplomasia huyo wa Marekani.
Hata hivyo, mtendaji huyo wa Takukuru alisema ni kawaida yake kukutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kila mwaka na kujadiliana nao mambo mengi kuhusu Tanzania. Alisema mabalozi ni wadau wakubwa katika bajeti ya Tanzania na hivyo huwa wanakutana kila mwaka kujadili mambo mbalimbali ya kuhusu kusaidia bajeti ya serikali. Mimi huwa nakutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kwa sababu wao ni wadau katika mradi wa government budget support (Mpango wa kusaidia bajeti ya serikali), hivyo hilo sio tatizo, alisema Dk Hoseah.
Msimamo wangu ni kwamba mapambao dhidi ya ufisadi ni endelevu hadi hapo tutakapofanikiwa kumaliza tatizo hili, alisema Dk Hosea na kukiri: Vitisho vipo vingi tu, kutoka kwa watu wanaotuhumiwa, lakini si hata ninyi waandishi mnamwagiwa tindikali katika mapambano yenu, hivyohivyo hata mimi napata vitisho. Alisisitiza kuwa pamoja na vitisho hivyo, hawezi kurudi nyuma katika mapambano ya rushwa na ufisadi.
Im Tanzanian I will die in Tanzania, it is my country (mimi ni Mtanzania, nitakufa Tanzania, ni nchi yangu), siwezi kuhama nchi kwa vitisho vya watu wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi na rushwa, alisisitiza Dk Hoseah. Hilo la kwamba nafikiria kuhama nchi wametia chumvi si unajua magazeti? Sijafikiria kuhama nchi licha ya vitisho, mimi naona ni changamoto na jambo la kawaida katika mapambano, aliongeza Dk Hoseah.
Kuhusu Rais Kikwete kukwamisha mapambano ya ufisadi kama alivyonukuliwa na gazeti hilo la The Guardian, Dk Hoseah alipiga chenga kulijibu badala yake akaeleza: Ili umpeleke mtu mahakamani si lazima umtuhumu na kumfanyia uchunguzi? Lakini pia lazima tujenge utamaduni wa kuwaheshimu viongozi wetu. Lakini baadaye saa 9:30 alasiri jana,Takukuru ilituma taarifa iliyoeleza kuwa Dk Hoseah ameshangazwa na Ofisa wa Ubalozi wa Marekani kumnukuu vibaya huku akisema hajui ana lengo gani.
Katika taarifa hiyo, Dk Hoseah alikiri kukutana na ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani ofisini kwake Julai mwaka 2007, lakini, akasema ripoti ya mazungumzo yao aliyoipeleka nchini kwake imechakachuliwa. Kwa mfano haikutokea katika mazungumzo yetu kusema kwamba Rais Jakaya Kikwete hakutaka kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake, kuwashitaki vigogo wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kama ilivyodaiwa na Ubalozi wa Marekani, ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya mahusiano ya Takukuru.
Nilichosema ni kwamba Rais hayuko tayari kuruhusu kushitakiwa kwa vigogo wa serikali au mtu mwengine yeyote kwa tuhuma za uvumi au kwa ushahidi dhaifu, kwa sababu kufanya hivyo, serikali itakuwa hatarini kwa kulipa gharama kubwa ya fidia ikiwa mtuhumiwa huyo atashinda kesi mahakamani, ilisema taarifa hiyo na kuongeza.
Kuhusu hofu ya maisha yangu, nakumbuka niliulizwa na Ubalozi wa Marekani kwamba je, naogopea maisha yangu au la, nikiwa Mkuu wa Takukuru? Na jibu langu lilikuwa rahisi kwamba bila ya shaka unapopambana na wakubwa na matajiri kama hao wanaotuhumiwa unapaswa kuwa makini na maisha yako. Lakini hata siku moja sikusema kwamba napanga kuhama nchi kwa sababu maisha yangu yapo hatarini.
Ni mshangao kuona kwa mara nyengine ofisa wa Ubalozi wa Marekani ananinukuu mimi vibaya au nje ya mada na sielewi kabisa lengo lao lilikuwa nini. Alsema rekodi yake, akiwa Mkuu wa Takukuru iko wazi kabisa wakati wowote anapokuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa yeyote wa ufisadi hawaogopi lolote isipokuwa ni kumburuza mahakamani bila ya kujali cheo chake.
Naye Mkurugezi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa muda wote. Kwa upande wa msaidizi wake, Premi Kibanga aligoma kuzungumzia suala hilo kwa kile alichoeleza kuwa hajaisoma habari hiyo iliyochapishwa na gazeti la The Guardian la Uingereza.
Mimi sijaiona wala kuisoma habari hiyo, hivyo siwezi kuzungumzia kitu ambacho sijakiona. Sina uhakika kwamba Dk Hoseah amesema hayo, pengine umemuelewa vibaya, alisema Kibanga. Juhudi za kumpata Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alphonso Lenhardt, kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani kila ilipopigwa.
source mwananchi
Ndugu watanzania mimi sishangai na ujumbe au siri inatolewa na wikileaks, na hata ndugu Hosea kwa ukweli ni kwamba kila jicho la mtanzania lilitarajia kuwa wale wote waliohusiswa na Rushwa, EPA, Richmond, Meremeta, na kila kitu kilichoigrimu serikali pasipo sababu si swala ambalo Jk la kulifumbia macho na watanzania walio wengi walitarajia kuwa angewashulikia wote , kama sasa wote wwaliachiwa kwenye uchaguzi kama Mramba , Lowasa ambao ni watu wanaotuhumiwa, sasa kina Lowasa wanaanza kujisafisha kwa kujipendekeza kwenye makanisa wakichangia ujenzi mbali mbali kwa lengo la kujisafisha kwa maandalizi ya kutafuta urais mwaka 2015, kweli nyani hawezi kujiona kwani hata waliotuibia na kutuingiza kwenye hasara ya mabilioni na matrioni kama Dowas Richmond bado wanajifanya watu wenye nia na wanaitakia nchi yetu amani, wakati ni madubu na Mbwa mwitu.
Hoseah amlipua Kikwete
Asema anaogopa kushughulikia ufisadi wa vigogo
na Edward Kinabo
MTANDAO wa Wikileaks wa Marekani umeibua siri nzito kuhusu uwezo na nia ya Rais Jakaya Kikwete katika kushughulikia ufisadi, ukidai kuwa ndiye anayekwamisha kushtakiwa kwa baadhi ya vigogo serikalini wanaotuhumiwa kuhusika katika rushwa kubwa nchini. Katika taarifa hiyo iliyochapishwa jana na gazeti la The Guardian la Uingereza, likinuu taarifa za kibalozi za Marekani zilizoanikwa na Wikileaks, lilisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, alimweleza mwanadiplomasia mmoja wa Kimarekani kwamba ugumu wa kupambana na ufisadi Tanzania unaanzia Ikulu.
Mtandao huo ulinukuu baadhi ya maelezo ya faragha kuhusu rushwa aliyoyatoa Dk. Hosea kwa mwanadiplomasia wa Kimarekani aitwaye Purnell Delly, walipokutana mwezi Julai mwaka 2007, Dar es Salaam.
Likinukuu mtandao huo, The Guardian liliandika, Dk. Hosea alidokeza kuwa Rais Kikwete hafurahishwi na sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya ufisadi ambao unaweza kuwatia hatiani vigogo wa ngazi za juu serikalini
. Hataki kuweka msingi wa kumwandama kiongozi yeyote miongoni mwa watangulizi wake (wastaafu).
Linasema mwanadiplomasia huyo alisema: Hosea alikuwa akisisitiza kwamba akiamua kuwa na makali, usalama wake binafsi utakuwa hatarini
anadai anaamini maisha yake yako hatarini, kwani amekuwa akipokea ujumbe wa vitisho kwa simu na barua na amekuwa akikumbushwa kila siku kwamba anapambana na watu matajiri na wenye nguvu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Hosea alitoa maelezo yanayokatisha tamaa juu ya mustakabali wa mapambano dhidi ya ufisadi nchini na ugumu uliopo katika kuwashtaki watuhumiwa wa ufisadi mkubwa.
Alituambia bila kufafanua... kwamba kesi zinazomhusu waziri mkuu au rais haziwezi kujadiliwa kabisa, kilisema chombo hicho na kisha kufafanua: Rais Kikwete hataki kumshughulikia mtangulizi wake yeyote mwenye tuhuma zinazostahili kufikishwa mahakamani.
Dk. Hoseah anadaiwa kumueleza mwanadiplomasia huyo jinsi rushwa ilivyokithiri katika Benki Kuu ya Tanzania na visiwani Zanzibar, lakini akadokeza ugumu wa kuishughulikia kwa sababu tu wahusika wakuu ni watu ambao hawahusiki.
Hoseah alidokeza kuwa mambo yakiwa mabaya angeweza hata kukimbia nchi, kwa mujibu wa taarifa hiyo ikimnukuu mwanadiplomasia huyo wa Marekani.
Ukihudhuria kwenye vikao vya juu (vya ndani), watu wanataka ujisikie kuwa wao ndio wamekuweka hapo ulipo. Wakiona huenendi na yale wanayotaka wao, basi hapo unakuwa katika hatari, ilisema sehemu nyingine ya taarifa hiyo ikinukuu maelezo ya Dk. Hoseah.
Aidha, katika mazungumzo yao, Dk. Hoseah alimpa matumaini mwanadiplomasia huyo kwamba TAKUKURU ingeweza kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote waliohusika katika kile alichokiita dili chafu ya rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza, hatua ambayo hata hivyo ilionekana isingeweza kutekelezwa na taasisi hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kauli hiyo ya Dk. Hoseah ilitokana na ukweli kwamba tayari wapelelezi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) walikuwa wameshampelekea faili lote la watuhumiwa likiwa na ushahidi jambo ambalo lingeweza kumuepusha na hatari ambayo ingeweza kumfika kama uchunguzi huo ungefanywa na TAKUKURU yake.
Katika kashfa hiyo, serikali ya Tanzania inadaiwa kununua rada ya kuongozea ndege za kiraia na za kivita kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa gharama kubwa ya dola 40 milioni, huku taarifa za uchunguzi kutoka SFO na vyanzo mbalimbali zikionyesha kuwa ununuzi huo haukuwa wa lazima na uligubikwa na rushwa.
Kashfa ya rada ilitendeka mwaka 1999, katika mazingira yaliyogubikwa na rushwa kwa watendaji serikalini ili waweze kulainisha watoa maamuzi. Kwa mujibu wa taarifa za maelezo ya Dk. Hoseah kwa mwanadiplomasia huyo, watuhumiwa zaidi wa rushwa ya rada wapo katika Wizara ya Ulinzi na jeshini.
Dk. Hoseah aliliita suala la rada kuwa ni dili chafu na kusema inawahusu maofisa wa Wizara ya Ulinzi na vigogo wawili au mmoja wa jeshi (hawakutajwa majina), ilieleza taarifa hiyo.
Kesi ya rada iliendelea kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini London, Uingereza.