Fundisho Kuhusu Patakatifu pa Duniani ,Na Jinsi linavyoakisi Huduma ya Yesu Katika Patakatifu pa Mbinguni
Katika Biblia patakatifu pa duniani ni mfano wa patakatifu pa mbinguni. Paulo anapaita patakatifu pa duniani kuwa ni kivuli cha Mambo ya Mbinguni. Biblia yasema hivi;’-watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima. [Waebr8:5]. Hivyo Basi tunaona Ukweli Ufuatao
1. Patakatifu pa duniani ni mfano wa patakatifu pa mbinguni. Patakatifu pa mbinguni ni kitu halisi ambapo patakatifu pa duniani ni kivuli chake, ama mfano wake.
2. Patakatifu pa duniani palikuwa na Hema mbili zilizotenganishwa kwa pazia katikati, Hema ya kwanza iliitwa patakatifu, na Hema ya pili iliitwa Patakatifu Mno. [Tazama Ebr9:2-3].
3. Hema ile ya Kwanza iitwayo Patakatifu palikuwa na vitu vifuatavyo. Palikuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho, na madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba;Tazama Kut40:22-27,Tazama pia Waebr9:2]
4. Hema ile ya Pili iliyiitwa Patakatifu mno ilikuwa na vifuatavyo;”-Chetezo cha dhahabu,Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote,Kopo la Dhahabu lenye Mana, Fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao viwili vya Agano,[Taz Ebr9:3-5].
5. Katika ile Hema ya kwanza iitwayo Patakatifu, Makuhani waliingia kila siku, Lakini katika Ile Hema ya Pili iitwayo patakatifu Mno Kuhani Mkuu aliingia mara moja kwa Mwaka.[TazamaEbr9:6-7].
6. Huduma za kutoa kafara zilizokuwa zinafanyika kila siku Asubuhi na Jioni daima katika Ile hema ya kwanza iitwayo patakatifu zilikuwa zinafanyika ifuatavyo. Mdhambi alikuwa anakuja na mnyama wake awe kondoo ama ng’ombe mkamilifu, anamleta mbele ya kuhani katika ile Hema ya kukutania. Na kisha anaweka mkono wake juu ya mnyama na kuziungama dhambi zake zote juu ya mnyama yule. Mnyama yule anafungwa na kuwekwa juu ya madhabahu na kisha mdhambi anaagizwa amchinje. Kisha Kuhani aliyetiwa mafuta anaitwaa baadhi ya damu ya yule mnyama na kuingia nayo hadi patakatifu na kisha anainyunyiza juu ya mapazia ya hekalu na juu ya madhabahu ya kufukiza uvumba. Hivyo kwa njia ya damu dhambi zilizotubiwa za mdhambi zinaamishwa hadi patakatifu kwenye mapazia ya hekalu. Na Baada ya hapo yule mnyama alikuwa anateketezwa kwa moto. Tazama[Wal4:1-11].
7. Huduma za kutoa makafara zilizokuwa zikifanyika mara moja kwa mwaka katika ile Hema ya pili iitwayo Patakatifu Mno ilikuwa kama ifuatavyo. Mara moja kwa Mwaka ilikuwa inaitwa Siku kuu ya upatanisho. Wana wa Israeli wote walikusanyika mbele ya Hema ya kukutania, wakijichunguza nafsi zao na kuziungama dhambi zao mbele za Mungu. Kuhani Mkuu akiisha kufanya Upatanisho wa nafsi yake Mwenyewe, Walichaguliwa Mbuzi wawili wakamilifu na kupigiwa kura ili apatikane Mbuzi wa Bwana na Mbuzi wa Azazeli. Yule aliyeangukiwa kuwa Mbuzi wa Bwana, anachukuliwa na kufanywa sadaka ya dhambi.Mnyama yule anachinjwa na Kuhani anaichukua Damu ya yule mnyama na kuingia nayo patakatifu mno, na kuinyunyiza juu ya kiti cha Rehema, na mbele ya kiti cha rehema, na kisha atatoka nje na ile damu na kuinyunyiza juu ya madhabahu iliyo mbele za Bwana. Hivyo kwa njia hiyo machafu yote ambayo yalikuwa yakihamishwa kwa njia ya damu hadi mle kwenye Hema ya kwanza iitwayo patakatifu yalitoka yote na kuwa juu ya mikono ya kuhani. Na kisha kuhani alimchukua yule mbuzi wa Azazeli na kisha kuziungama dhambi zile zote za Mkutano wa wana wa Israeli juu ya mbuzi wa Azazeli. Na kisha anachaguliwa Mtu ambaye atamchukua Mbuzi wa Azazeli na kwenda naye mpaka jangwani na kumwacha huko. Hivyo ndivyo Patakatifu palivyotakaswa katika Hekalu la zamani. [Tazama Wal16:1-34]
8. Kama tulivyoona Mwanzoni kuwa patakatifu pa kale pa kidunia palikuwa ni mfano ama kivuli cha patakatifu pa mbinguni, na Musa aliagizwa kutengeneza patakatifu pa kidunia kwa mfano wa patakatifu pa mbinguni kama alivyoonyeshwa. Hivyo kwa maana nyingine ni kwamba patakatifu pa mbinguni ndipo patakatifu halisi, na ambapo pa dunia ni mfano wake. Hivyo mfumo wa patakatifu pa duniani ni taswira na mfanano wa patakatifu pa mbinguni.
9. Swali ka Kujiuliza ni kwamba Je Mbinguni kuna patakatifu[ Santuary]? Na kama lipo linafananaje?
10. Biblia iko wazi kuwa Mbinguni kuna patakatifu, ile hema ya kweli ambayo imefanyika pasipo mikono ya Mwanadamu ambamo Yesu amekwenda kuhudumu kwa ajili yetu. Biblia yasema hivi;’-Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu. [Ebr8:1-2].
11. Nabii Yohana alionyeshwa Mlango wa Hekalu la Mbinguni ukifunguliwa, Akaonyeshwa ile Hema ya Kwanza iitwayo patakatifu na akamwona Mungu akiwa ameketi kitini pa enzi akizungukwa na Wazee ishirini nan ne, na wale wenye Uhai wanne. Mbele zake zinawaka taa saba za Moto na ndizo Roho saba za Mungu. Taz Ufu4:5]. Tunatambua kuwa hapa ni ile hema ya kwanza iitwayo patakatifu sababu zle taa saba za Moto katika patakatifu pa duniani ziliwakilishwa na kile kinara cha taa chenye taa saba. Katika Kitabu cha Ufunuo 8;3-5, tunaona madhabahu ya dhahabu ya kufukiza Uvumba iliyo mbele za Bwana, chetezo cha kufukiza uvumba, Madhabahu ya dhahabu ya kufukizia Uvumba ilikuwepo katika ile Hema ya kwanza iitwayo Patakatifu.
12. Nabii Yohana alionyeshwa pia Hekalu lililoko mbinguni likifunguliwa tena na kisha akaona Sanduku lile la Agano lenye kubeba Amri kumi. Hapa Nabii alionyeshwa ile Hema ya pili iitwayo Patakatifu mno. Sanduku la Agano katika Hekalu la Kidunia lilikaa patakatifu Mno.Biblia yasema hivi;’-Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana. [Ufu11:19]
13. Hivyo basi tunaona kuwa kama patakatifu pa kidunia palivyo na sehemu mbili ambazo zinatanganishwa na pazia yaani patakatifu na patakatifu Mno, hali kadhalika na patakatifu pa mbinguni pana sehemu mbili ambazo ni Patakatifu na Patakatifu mno.
14. Hebu sasa tuangalie Mfanano wa huduma kama zilivyokuwa zikifanyika katika patakatifu pa duniani na patakatifu pa mbinguni.
15. Katika patakatifu pa kidunia makuhani ama kuhani Mkuu aliingia patakatifu kwa damu ya wanyama ili kuwafanyia wana wa Israeli upatanisho. Katika patakatifu pa mbinguni Yesu anaingia kwa damu yake mwenyewe ili kuwafanya watu wake upatanisho. Biblia yasema hivi;’- wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. [Ebr9:12]
16. Katika Patakatifu pa duniani, Kiti cha rehema na Sanduku la Agano lilikaa katika Ile hema ya pili iitwayo Patakatifu mno, Lakini Utukufu wa Mungu ulipopashukia Patakatifu mno na kukaa juu ya kiti cha rehema, Utukufu wa Mungu ulipajaza mahala pote patakatifu na patakatifu mno, kama ishara kuwa Uwepo wa Mungu unapatikana kote kote iwe ni Patakatifu ama iwe ni patakatifu mno. Hali kadhalika na katika patakatifu pa mbinguni Mungu anaonekana katika Hema zote mbili iwe ni patakatifu ama patakatifu mno.[Tazama Kut40:34]
17. Kila Siku daima, Makuhani waliingia Patakatifu wakiwa na damu ya mnyama ili kufanya upatanisho, Hali kadhalika na Kristo baada ya kupaa na kwenda mbinguni, alikwenda kukaa mkono wa kuume wa Mungu na kuanza kazi yake ya kuwafanyia watu wake upatanisho na kuwaombea. Biblia yasema hivi;’-Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu. [Ebr8:1-2].
18. Mara moja kwa Mwaka Kuhani Mkuu aliingia patakatifu mno ili kupatakasa patakatifu. Hali kadhalika na Kristo Aliingia patakatifu mno Mwaka 1844 AD, ili kupatakasa Patakatifu kulingana na unabii wa Daniel wa siku 2300 ambao ni sawa na Miaka 2300.Unabii unasema kuwa Mwishoni mwa siku 2300 ndipo patakatifu pataakaswa. [Tazama Dan8:14.]
19. Katika Patakatufu pa kidunia, Baada ya Mdhambi kumchinja mnyama, Kuhani aliichukua ile damu na kisha kuinyunyiza katika mapazia ya Hekalu, na hivyo kwa njia ya damu Dhambi za mdhambi aliyetubu kuhamishwa katika mapazia ya hekalu kama kumbukumbu ya dhambi zake, zikisubiri kusafishwa mara moja kila Mwaka. Katika patakatifu pa mbinguni, dhambi zote za watakatifu zilizosamehewa na kutubiwa, zinarekodiwa katika vitabu vya mbinguni, pamoja na ushahidi wa toba yake ya dhati, vikisubiri kuja kuondolewa kwa umilele wakati wa kazi ya Yesu katika ile hema ya pili iitwayo patakatifu mno. Musa alipowaombea wana wa Israel aliomba hivi;’- ;’-Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao - na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.[Kut32:32]. Lakini Jibu la Mungu likawa hivi;’-Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. [Kut32:33].Pia soma Ufu20:12.
20. Mara moja kwa Mwaka katika patakatifu pa kidunia Kuhani mkuu aliingia Patakatifu Mno na damu ya Mbuzi ili kupatakasa patakatifu. Mbuzi wawili walipigiwa Kura mmoja awe wa Bwana na Mwingine awe wa Azazeli. Mbuzi wa Bwana alichinjwa na kuhani aliichukua damu ya mnyama na kuinyunyiza juu ya kiti cha Rehema, na mbele ya kiti cha rehema, na hivyo dhambi zote zilizokuwa zikihamishwa ndani ya ile hema ya patakatifu kwenye mapazia ya Hekalu zilikuwa zinaondolewa zote na patakatifu panatakaswa na dhambi zote zinakuwa juu ya mikono ya kuhani. Na kisha anachukuliwa yume Mbuzi wa Azazeli na Kisha kuhani anaweka Mikono yake juu ya Mbuzi wa Azazeli. Hivyo machafu yote ya wana wa Izraeli yalitoka kwenye Mikono ya kuhani hadi kwa Mbuzi wa Azazeli, na kisha Mtu aliyewekwa tayari aliagizwa amchukue Mbuzi huyo na kwenda naye jangwani na kumuacha huko. Hali kadhalika na Patakatifu pa mbinguni, Nabii Danieli alionyeshwa kuwa Mwishoni mwa siku 2300 ambayo ni sawasawa na Miaka 2300, ambazo kulingana na Unabii ziliishia mwaka 1844 AD, Yesu aliingia Patakatifu Mno pa Mbinguni ili kupatakasa patakatifu. Tokea Mwaka huo vitabu vya mbinguni vimekuwa vikikaguliwa na kuchunguzwa, na wale watakatifu waliotubu katika Damu ya Yesu dhambi zao zinafutwa milele, na majina yao yanadumishwa katika kitabu cha Uzima. Lakini wale watakatifu ambao wataonekana kuwa kuna dhambi ambayo haikutubiwa, basi dhambi zao hazitafutwa hata milele na majina yao yatafutwa yatoke katika kitabu cha Uzima. Dhambi ambazo watakatifu walizitenda zitafutwa na zitawekwa mikononi mwa Yesu, na kazi yake katika patakatifu pa mbinguni ikiisha, ndipo ataziweka dhambi zote ambazo watakatifu walisababishiwa kuzitenda juu ya Shetani, na Shetani atafungwa hapa duniani na malaika zake mda wa Miaka Elfu, akisubiri Uangamivu wake wa Mwisho. Kazi ya Yesu katika patakatifu mno mbinguni ikiisha, Anapewa Ufalme, na idadi ya waliokombolewa inakamilika. Yesu atarudi kuwachukua watakatifu.
21. Nabii Danieli alionyeshwa Baba akihama toka patakatifu na kwenda patakatifu mno kwa kiti chake cha Enzi cha Moto na chenye Magurudumu ya moto. Alionyeshwa malaika Maelfuelfu wakisimama mbele zake na kumtumikia. Alionyeshwa vitabu vya mbinguni vikifunguliwa na kuchunguzwa, na Upinga Kristo uliovaa vazi la Udini ukihukumiwa. Biblia yasema hivi;’- Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. [Dan7:9-10].
22. Nabii Daniel alionyeshwa Yesu akija na Mawingu ya Mbinguni, sii kuja hapa duniani, bali akimkaribia mzee wa siku huko Patakatifu mno mbinguni, ili kumalizia kazi yake ya Mwisho ya Upatanisho katika patakatifu pa mbinguni, na kusimama kama mtetezi wa watakatifu wakati rekodi zao zinapokaguliwa mbele za Baba. Kazi yake ikiisha anapewa ufalme, na kisha anakuja kuwachukua watakatifu. Biblia yasema hivi;’- Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. [Dan7:13-14]