Nakubaliana na wewe kwa kiasi kikubwa. Ila natamani tujifunze kutoka kwa hao uliowataja na wengineo wa Ulaya kwa jumla. Licha ya kuwa wamezoeleka kufika mbali, wananchi wao hawakuwananga na kuwalaani kwa kutolewa. Wamewapa moyo. Del Bosque amepewa timu anedelee nayo hadi 2016. Sisi Afrika ambao hatukuzowea kufika mbali, timu zetu hunangwa na kusimangwa kila zinapotolewa, bila hata ya kuangalia mazingira ya kutolewa. Nilitegemea mara hii tujivune angalau kwa kufikisha timu mbili kati ya sita za awali kwenye 16 bora. Lakini wapi! Ni kama vile tunashindwa kuelewa kwamba zinazoingia raundi ya pili ni timu 16 tu, robo fainali ni nane tu, nusu ni nne tu, fainali ni mbili tu, na inayobeba kombe ni moja tu. Kwa timu 6 za Afrika, kikubwa zinazoweza kufanya ni zote kuingia 16 bora (hivyo kuziachia timu 26 zilizosalia nafasi kumi zilizobaki - inawezekana kweli?), kisha zote sita ziingie robo fainali (hivyo kuziwachia timu kumi zitazosalia nafasi mbili tu -inayumkinika?), kisha nne kati ya hizo zikutane kwenye nusu fainali (na kuzitoa timu nne zote zitazocheza robo fainali - inaingia akikini?), na hatimaye zenyewe mbili zikitane kwenye fainali. Uwezo wa kimpira kwa timu 6 kati ya 6 kuingia hadi robo fainali na baadaye mbili zao kulazimika kuachia unaweza kuwapo. Lakini kiuhalisia je? Namna rahisi ya kubaini ukweli wa hili ni kuwa hatima ya yote, timu 31 zinatakiwa kuachia kombe hilo kwa timu moja tu. Si kweli kwamba hiyo moja tu ndiyo itakuwa imefanya vizuri. Ziko za kwenye 16 zilizotolewa mwanzo zitazokuwa zimefanya vizuri ila zililazimika kuachia kwa kuwa nafasi hazikutosha, kadhalika nane zilizosalia, nne za nusu fainali na moja ya fainali. Kwa nini tusizichukulie baadhi ya timu zetu zilizotolewa kwa namna hii kuwa ni best-losers zilizokosa nafasi ya kuendelea kwa sababu haikuwapo, badala yake ni lawama, lawama, lawama?