Nimetafakari nikajua CHANZO CHA MARADHI MENGI NI WEWE MWENYEWE! Kwa nini nasema hivi? Ni kwa sababu maradhi mengi yanayowapata watu siku hizi yanatokana na namna tunavyoishi.
Mfano, unakula nini? Unakunywa nini? Je, unafanya mazoezi ya kutosha ili kuufanya mwili wako kuwa active? Unakunywa maji kiasi gani kwa siku?
Kwa kawaida tunakula milo miwili au mitatu kwa siku. Je, baada ya kula milo hiyo kwa siku, unapata haja kubwa mara ngapi kwa siku? Au ndiyo zinapita siku 2, 3, 4 hadi week nzima ndiyo upate haja kubwa?
Ok, labda unapata haja kubwa vizuri. Je, kinatoka chenyewe au unatumia nguvu kukisukuma ili kitoke? Kama unatumia nguvu kukisukuma jua kwamba tayari kuna tatizo kwenye mfumo wa mmeng'enyo wako wa chakula.
Naomba ujiulize maswali hayo kisha ujijibu mwenyewe then utatambua ni kwa namna gani chanzo cha maradhi mengi ni wewe mwenyewe.
Mlo kamili ni nini hasa? Mlo kamili hutokana na mchanganyiko wa chakula kutoka katika makundi mbalimbali ya vyakula. Kwa nini tunashauriwa kula mlo kamili? Ni kwa sababu mlo huo huupatia mwili virutubisho vyote vinavyohitajika kwa ajili ya lishe na afya bora.
Tunashauriwa kula walau milo mitatu iliyo kamili kwa siku. Ili kupata mlo huo kamili tunapaswa kuchagua vyakula kutoka katika makundi yafuatayo:
(1) vyakula vya nafaka mizizi na ndizi. Mfano mahindi, mihogo, viazi, mbatata, ndizi n.k
(2) vyakula vya jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama. Mfano soya, choroko, njegere, maharage n.k, samaki, nyama, mayai n.k.
(3) mboga mboga na matunda. Mfano aina zote za matunda, mboga zote za majani, karoti, hoho, biringanya, ngogwe, nyanya n.k
(4) mafuta na sukari. Mfano karanga, nazi, mafuta ya kupikia, miwa n.k.
(5) maji. Tunashauriwa kunywa maji kwa wingi kadiri mtu awezavyo lakini pia isiwe chini ya glass 8 kwa siku. Lakini pia sahani ya mlo kamili inapaswa kuwa na mboga mboga kwa wingi kuliko vyakula vya mizizi na nafaka hii ni kwa sababu mboga mboga zina nyuzinyuzi (fibre) za kutosha zinazosaidia mmenge'enyo wa chakula tumboni.
MUHIMU:
👉 tumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira unayoishi.
👉 pendelea kula nyama nyeupe zaidi kuliko nyekundu.
👉 kula mboga mboga kwa kiasi kikubwa kuliko nafaka.
👉 zingatia usafi na usalama wa chakula na maji.
👉 tumia mafuta na sukari kwa kiasi.
👉 punguza matumizi ya chumvi, kahawa, chai na soda.
Baada ya kuangalia makundi hayo jaribu kujitathmini mwenyewe. Je, unayazingatia hayo? Kama siyo, anza sasa.