Yajue mambo matano (5) yanayoweza kufanya kampuni yako ifutwe na mamlaka nchini Tanzania

Yajue mambo matano (5) yanayoweza kufanya kampuni yako ifutwe na mamlaka nchini Tanzania

Tempus Fugit

JF-Expert Member
Joined
Jun 22, 2016
Posts
850
Reaction score
2,212
Mnamo mwaka 2019 Tanzania ilifanya marekebisho ya sheria yake ya Makampuni ya mwaka 2002 na kuleta mambo kadhaa mapya. Marekebisho hayo yaliletwa na sheria ya “The written laws (Miscellaneous Amendments) (No.3) Act, 2019" Kifungu cha 10 cha sheria hii kilileta kifungu kipya cha 400A katika sheria ya Makampuni ya mwaka 2002 ambacho kilileta mabadiliko kadha wa kadha.

Nchini Tanzania makampuni husajiliwa na Msajili wa Makampuni wa mamlaka iitwayo BRELA . Marekebisho hayo ya sheria ya makampuni yamempa msajili mamlaka ya kuifuta kampuni yoyote katika rejista ya makampuni endapo mazingira yafuatayo yatathibitika kutokea.
  • Endapo kampuni ilisajiliwa kiulaghai (Fraudulent registered company)
  • Endapo kampuni inajihusisha na vitendo vya jinai kama utakatishaji fedha, kufadhili ugaidi, biashara ya madawa ya kulevya, biashara ya binadamu au jinai nyinginezo kama alivyoainisha waziri anayehusika na biashara.
  • Upotoshaji/ulaghai wakati wa kusajiliwa kwa kampuni husika.
  • Endapo wanahisa au ma dairekta wa kampuni hawaruhusiwi kuingia nchini Tanzania kwa matakwa ya kisheria.
  • Endapo kampuni inafanya shughuli tofauti na zilizo ainishwa katika katiba yake.
Endapo mazingira haya yatajitokeza msajili ataiandikia kampuni husika notisi ya kusudia la kuifuta kampuni husika kutoka katika rejista ya makampuni Tanzania. Kampuni ikifutwa inakuwa haipo, haitoweza tena kufanya biashara chini ya usajili uliofutwa.

Je, ufanye nini endapo kampuni yako itafutwa na msajili kwa sababu hizo tajwa?

Kifungu cha 400A (2) cha Sheria ya makampuni ya Tanzania kinawapa wamiliki wa kampuni nafasi ya kufanya yafuatayo baada ya kupokea notisi ya kusudio la kufutwa kwa kampuni yao.
  • Kumuandikia msajili kwa maandishi sababu za kutosheleza za kwa nini kampuni hiyo isifutwe kwenye rejista ya makampuni.
  • Kufungua shauri mahakamani kupinga notisi ya msajili ya kusudio la kuifuta kampuni husika.
Je, endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo ya sababu za kwa nini isifutwe na msajili nini kitatokea?

Kwa mujibu wa kifungu cha 400A (3) cha sheria ya Makampuni endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo ya kwa nini isifutwe ndani ya siku 30 toka ipokee notisi ya kusudio la kufutwa na msajili, au endapo maelezo hayo hayatoi sababu zinazomridhisha msajili basi ataifuta kampuni hiyo katika rejista ya makampuni na kuchapisha maamuzi hayo katika gazeti la serikali.

Endapo kampuni, mwanahisa, au mtu anayeidai kampuni iliyofungwa hajaridhika na maamuzi ya msajili ya kuifuta kampuni, je achukue hatua zipi?

Kwa mujibu wa kifungu cha 400A (4) wahusika ambao hawajaridhika na maamuzi ya msajili ya kuifuta kampuni husika wanaweza kupeleka maombi Mahakamani kuomba kampuni iliyofutwa irejeshwe kwenye rejista ya makampuni. Maombi haya ni lazima yafanywe ndani ya miaka mitano (5).

Baada ya mahakama kupokea maombi ya kurejesha kampuni iliyofutwa je inaweza kutoa maamuzi gani?

Kifungu cha 400A (5) cha sheria ya Makampuni kinaelekeza kuwa Mahakama ikipokea maombi hayo inaweza kuamuru yafuatayo;
  1. Amri ya kuirejesha kampuni iliyofutwa na msajili katika rejista ya makampuni
  2. Kutoa amri nyinginezo zozote itakazoona zinafaa kuhusiana na kampuni iliyofutwa.
Kampuni iliyorejeshwa katika rejista ya makampuni baada ya kufutwa na msajili itachukuliwa kana kwamba iliendelea kuwepo kana kwamba haikuwahi kufutwa.

Kufanya mambo hayo matano nchini Tanzania kunaweza kuifanya kampuni yako kufutwa.
 
Sidhani kama kuna mifumo wezeshi ya kuwafanya Brela kusimamia sheria hizi.

Ni sawa na BASATA/ COSOTA wanavyoshindwa kusimamia hakimiliki za wasanii/ wabunifu. Sheria zinatungwa ndio, ila utekelezaji wake ni almost impossible.

Waboreshe mifumo kwanza, iwe top notch, vingine vitajiratibu vyenyewe.
 
Back
Top Bottom