Gaidi hana sura babu we subiri hadi mwisho wa picha
Ungana nasi kumwombea Mh Friman Mbowe siyo gaidi
LITANIA MAALUM YA KUOMBEA KESI YA MBOWE NA WENZAKE!
KIONGOZI : Mwenyezi Mungu mwenye rehema! Twakushukuru kwa zawadi ya afya na uhai. Tunakuomba utusamehe makosa yetu. Tunatubu kwa ajili yetu na wenzetu na hasa kwa ajili ya Mbowe, Bwire, Lingw'enya, Adamoo, Jaji Joachim Tiganga, Mawakili wa Utetezi, Mawakili wa Mashtaka, Mashahidi katika pande zote mbili, Waendesha Mashtaka na watu walio katika mamlaka.
WAUMINI: Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunamuinua mbele ya Kiti chako cha Enzi Jaji Joachim Tiganga ambaye anasikiliza Kesi hiyo! Tunaomba ukampe kiu ya kutenda haki pasipo kuogopa vitisho na mashinikizo ye yote. Ukamuepushe na rushwa ya kutamani madaraka kupitia Kesi hii. Ukampe ujasiri wa kuhukumu kwa haki pasipo kuogopa wanadamu. Ukampe uwoga wa kupendelea na kufinya haki ili kuwaridhisha watu. Akatambue kuwa akisimama katika haki utamuinua zaidi na kumpa heshima ya kimbingu, akipendelea na kufinya haki atafedheheshwa!
WAUMINI : Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunawaweka mikononi mwako Mawakili Wasomi wa Upande wa Mashtaka! Kwamba wanao wajibu wa kuwaongoza Mashahidi kushuhudia kweli tupu. Kwamba wakifanya hivyo watainuliwa na kupewa heshima ya kimbingu na wataheshimiwa na wanadamu pia. Wakaogope kuwaongoza Mashahidi kushuhudia uwongo mbele ya Mahakama ili kujipendekeza kwa walio na mamlaka ambao wana maslahi binafsi na Kesi hiyo. Watambue kuwa kwa kufanya hivyo kutawaingiza katika fedheha, aibu na laana itakayoshuhudiwa na wengi kwa kuwa wewe ni Mungu unayechukia wanaowashuhudia watu wengine uwongo!
WAUMINI: Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunawaombea Mashahidi wa pande zote mbili! Ukawape ujasiri wale waliojiandaa kushuhudia iliyo kweli. Ukawape ujasiri wa kukataa kupanda kizimbani wale watakaoshawishiwa kushuhudia uwongo. Ukawanyime ujasiri wa kushuhudia uwongo na wakipanda kizimbani kwa ajili ya kushuhudia uwongo, wakakose amani na muelekeo. Wote watambue kuwa wakishuhudia uwongo watafedheheshwa na wakishuhudia ukweli wataheshimiwa na wewe na wanadamu pia!
WAUMINI : Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunawaombea Mawakili Wasomi wa Upande wa Utetezi! Tunaomba ukawape ujasiri wa kukataa ushawishi kupitia rushwa na vitisho! Wakawaongoze Mashahidi kusema kweli tupu. Wakatambue kuwa kupokea rushwa na kuwaongoza Mashahidi kushuhudia uwongo ni fedheha kwao na laana kubwa, lakini kukataa rushwa na kuwaongoza Mashahidi kushuhudia kweli tupu ni heshima kubwa kutoka kwako na kwa wanadamu!
WAUMINI : Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI: Tunawaombea Washtakiwa Mbowe, Bwire, Lingw'enya na Adamoo! Uwape utulivu wakitambua kuwa wewe ni Mungu mwenye haki. Ukawalinde dhidi ya hila zo zote mahali po pote wawapo barabarani, Mahakamani na hata Gerezani. Ukazilinde familia zao na watu wanaowategemea. Ukawape muda mzuri wa kukutafakari wewe wawapo Gerezani na hata kukukaribia wewe zaidi! Pale walipokukosea wewe na wanadamu, wakautumie muda huo kuzijutia dhambi zao ili wapate toba ya kweli!
WAUMINI: Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI: Tunawaombea wenye mamlaka ambao hawahusiki moja kwa moja lakini wako nyuma ya Kesi hiyo! Kama kuna waliohusika kuasisisi, kutunga na kuratibu uwongo basi ukawape neema ya kutubu na kujutia uovu huo, vinginevyo watambue kuwa fedheha, aibu na anguko viko mbele yao! Ukawape ujasiri wa kujitenga na hila ye yote kuanzia leo. Wakijua kuwa wakifanya hivyo watapata rehema na heshima kutoka kwako na wanadamu pia!
WAUMINI : Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunawaweka mikononi mwako wanaoendelea kupanga, kuratibu na kutekeleza hila wakati huu. Wawe wa Polisi Magereza, Jeshi la Polisi, Mahakama na watumishi wake, Waendesha Mashtaka, Mawakili, Serikalini, na Taasisi nyingine iwayo ye yote ile. Wamiminie Roho wako ili watambue uovu wao na kuuacha. Ukafarakanishe mawasiliano yao; hila, uwongo na uovu wao. Mikakati, hila na uwongo wao vikadhihirike hadharani ili wakafedheheshwe. Kama hawatatubu na kuacha na wakiendelea na hayo wakashushwe kutoka katika nafasi zao na kusiwepo na kumbukumbu lao tena katika sehemu zao za kazi!
WAUMINI: Ee Mungu twakuomba utusikie!
KIONGOZI : Tunaomba haya yote kupitia Jina la Yesu Kristo, atawalaye na kumiliki pamoja nawe katika Umoja wa Roho Mtakatifu! Amina!
WAUMINI : Amina!
NB: Sala hii inaweza kutumiwa katika makundi ya watu kuanzia watu wawili na kuendelea. Inaweza kutumika pia katika familia.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula