2003 nilipomaliza sekondari mzee wangu alininunulia Hiace dungu (Kipanya) kifanye daladala ili nianze kuwekeza pesa za chuo. Kilikuwa kinapiga route ya Tabata Mawenzi - Buguruni.
Ile gari kila siku ilikuwa haiishi matatizo, kupelekea kupigana sound katika kupewa hesabu jioni ikifika. Hesabu ilikuwa 25,000 kila siku na Jumapili ilikuwa ni ya Dereva na konda. Ila kuipata hiyo 25,000 ilikuwa mbinde.
Siku moja nikaona isiwe kesi, nikaamka na gari. Mimi nilikaa siti ya mbele nazunguka tu na gari. Cha ajabu siku nzima mpaka saa 9 hakukuwa na pancha, kukamatwa wala tatizo lolote. Ilipofika saa 10 dereva akapigiwa simu kuwa kuna tatizo kwake, ikabidi ampe jamaa yake 'deiwaka'. Kipindi hicho bado nipo siti ya mbele.
Dereva wa deiwaka kuingia tu, akamuuliza konda, vipi leo umetoa taarifa ya kukamatwa au kuharibikiwa kwa boss wako. Konda akajifanya haelewi. Dereva alikuwa hanijui, alidhani ni abiria. Na nilipokaa konda hawezi hata kumtonya.
Jamaa akawa busy anamsifia konda kuwa kwa speed wanayokwenda nayo, yeye na dereva wake watanunua hiace yao muda si mrefu maana wamepata Boss mjinga.
Hapo ndipo nilipogundua kulikuwa na hujuma za makusudi ili wao wavune mimi niumie.
Tulipopaki ile gari jioni nilipata pesa yangu kamili ya siku na ikawa ndio mwisho wa ile daladala maana nilimwambia mzee auze tu gari yenyewe.