Ujumbe wa Al-Azhar kwa muqawama Palestina: Nyinyi ni mashujaa, mnapigana na wanyama
Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Misri kimepongeza ujasiri na ushujaa wa wanamapambano na muqawama wa Palestina na kusema kuwa wanakabiliana na jeshi la kigaidi la kinyama.
Chuo Kikuu cha al-Azhar kimesema hayo katika ujumbe wake kwa vikosi vya muqawama katika Ukanda wa Gaza na kuwapongeza wanamuqawama wa Palestina kutokana na kusimama kwao kidete kutetea ardhi na nchi yao.
Kwa mujibu wa tovuti ya Rusiya Al-Yaum, sehemu moja ya taarifa ya Al-Azhar ikiwa taasisi ya juu zaidi ya kidini ya Sunni, inasema: "Pongezi na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa muqawama wa Palestina na watu wasio na hatia wa Gaza, ambao ni kielelezo cha fahari, uthabiti na subira."
Taarifa ya Chuo Kikuu cha Al-Azhar imeongeza kusema kuwa, "Salamu zikufikieni enyi mashujaa, ambao kwa imani yenu mlikabiliana na manowari za kivita, meli za kubeba ndege na washambuliaji wa ndege na kuzisimamisha bila ya woga au wasiwasi wowote."