MABINGWA mara 17 wa Tanzania Bara, Yanga leo inashuka dimbani kuikabili Azam FC katika harakati zake za kusaka ubingwa msimu huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyokusanya pointi 40 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Simba kwa pointi tano wanajua endepo watapoteza mchezo huo wa leo ndoto yao ya ubingwa itakuwa shakani zaidi ya kugomea nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho pamoja na Azam.
Kocha wa Yanga, Sam Timbe alisema kuwa mchezo wa leo ni mgumu kutokana na mvutano wa pointi uliopo katika ligi hiyo hasa katika timu hizo tatu za juu zinazogombea kuchukua ubingwa au nafasi ya pili.
''Najua Azam ni timu nzuri wenye wachezaji bora, lakini mechi hiyo ni muhimu kwetu tushinde ilituweze kuifukuzia Simba katika harakati za kuchukua ubingwa kwani tukipoteza mchezo huo itakuwa ngumu kuchukuwa ubingwa msimu huu,'' alisema Timbe.
Yanga imebakiza mchezo na Azam leo, Toto na African Lyon, lakini Timbe alisema mechi hizo ni ngumu kwa kuwa timu zote zinapigana kucheza kufa na kupona kuhakikisha inashinda mechi zake.
Akizungumza na Mwananchi makao makuu ya klabu hiyo jana, Timbe alisema ni vigumu kubashiri timu yake kuchukua ubingwa kutokana na upinzani uliopo wakati wapinzani wao Simba wanashikilia kilele na wanataka kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo.
"Ligi ya Tanzania ni ngumu kutokana na uchache wa timu zinazoshiriki, timu 12 ni chache sana, zingekuwa zinashiriki timu 20 sasa hivi tungekuwa tunamechi nyingi bado za kucheza, wala tusingekuwa na presha ya kutwaa ubingwa, lakini kwa mfumo huu wa ligi ni mgumu kusema unachukua ubingwa."
"Itakuwa ni furaha Simba wakipoteza mechi zao zilizosalia ingawa najua lakini hii ni soka chochote kinaweza kutokea, ningependa kuona nashinda mechi zangu zote zilizobaki na wapinzani wangu wakipoteza nadhani itakuwa njia nzuri ya sisi kuchukua ubingwa."alisema kocha huyo raia wa Uganda.
Naye Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema kuwa anajua kuwa anacheza na timu kubwa na yenye wachezaji wazoefu na mashabiki wengi, lakini kwa upande wake haogopi hilo.
Alisema anajiamini kushinda mchezo huo kutokana na kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji ambayo inaweza kuiletea madhara Yanga.Stewart alisema mchezo huo ni muhimu sana kwao kushinda iliwaweze ujiakikishia kuchukua nafasi ya pili kwani siku zote michezo ya mwisho ndio inakuwa migumu sana kwani kila mmoja anataka amalize ligi hakiwa katika nafasi nzuri.
Source: Mwananchi