Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Pwani Kaskazini, Ndugu Abdul Ally(kushoto) akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Tanga (Bombo Hospital), Dkt. Frank Shega ikiwa ni dhamira ya Yas kuunga mkono juhudi za Serikali na Sekta ya Afya katika kufikisha huduma bora kwa Watanzania.
Tanga, Tanzania – Juni 2025- Kampuni ya mawasiliano nchini, Yas, imekabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo kama sehemu ya mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), unaolenga kuboresha huduma za afya, hususan kwa wanawake na watoto.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vitanda vya kawaida vya hospitali, magodoro na mashuka, vitanda maalum vya kujifungulia, vifaa vya kusikiliza mapigo ya moyo wa mtoto tumboni (fetal dopplers), vifaa vya kujifungulia salama (maternity kits), na buti maalum (gumboots) kwa ajili ya watumishi wa afya.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Pwani Kaskazini, Ndugu Abdul Ally, alisema msaada huo ni sehemu ya dhamira ya Yas ya kuunga mkono juhudi za Serikali na sekta ya afya katika kufikisha huduma bora kwa Watanzania.
Aidha, Abdul Ally alieleza kuwa afya ni moja ya vipaumbele vikuu katika mpango wa CSR wa kampuni hiyo, sambamba na elimu na uwezeshaji wa kijamii.“Tumeamua kuleta msaada huu hapa Hospitali ya Bombo kwa sababu tunatambua kuwa ni kitovu cha matibabu kwa mkoa huu na tegemeo kwa maelfu ya wananchi,” alisema Abdul Ally.
“Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, wanawake 5 kati ya 10 hupata changamoto wakati wa kujifungua kutokana na mazingira duni ya huduma. Hivyo basi, Yas imeona ni vyema kuchangia kwa vitendo ili kusaidia kuboresha hali hiyo – hasa kwa wanawake na watoto,” aliongeza.
“Sisi Yas, kazi yetu ni kuwaunganisha Watanzania na fursa kupitia mawasiliano ya uhakika na huduma za kidijitali. Lakini pia tunaamini kuwa hakuna njia bora zaidi ya kuungana na jamii kuliko kupitia huduma zinazogusa maisha yao ya kila siku kama afya. Tutaendelea kushirikiana na jamii na wadau wengine kuhakikisha maendeleo ya pamoja yanapatikana,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, Dkt. Frank Shega, aliishukuru kampuni ya Yas kwa msaada huo, akieleza kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa huduma hospitalini hapo.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu kutoka Yas. Vifaa hivi ni msaada mkubwa katika mazingira yetu, na vitasaidia hasa kwenye huduma kwa akinamama na watoto. Tunapokea wagonjwa zaidi ya 2,500 kila mwezi, hivyo msaada kama huu una maana kubwa sana kwa ustawi wa huduma zetu,” alisema Dkt. Shega.
“Pia ninapenda kupongeza jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo anaendelea kuwekeza katika sekta ya afya. Mchango huu wa Yas unaenda sambamba kabisa na dhamira ya Serikali ya kuboresha afya ya Watanzania. Natoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano huu mzuri wa Yas,” aliongeza.
Hospitali ya Bombo ni miongoni mwa hospitali kubwa na kongwe nchini, ikihudumia wagonjwa kutoka ndani ya mkoa wa Tanga na maeneo jirani, ikiwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma bora na za haraka.
Kwa msaada huu, Yas imedhihirisha dhamira yake ya kuwekeza kwa vitendo katika ustawi wa jamii, na kuendelea kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya Watanzania.