Uhusiano kati ya ibada za dini ya Kikristo na ibada za dini ya Kipagani
Katika maelezo yaliyopita tumeona kwa uchache jinsi muasisi wa dini ya Kikristo, Bwana Paulo alivyokuwa akimshutumu Petro, Barnaba na Wayahudi wengine alipokutana nao huko Antiokia (kwa watu wa mataifa au wapagani) kwa kutofuata kwao moja kwa moja desturi (ibada) za watu wa mataifa (wapagani), kinyume na walivyokuwa wakifanya hivyo kabla ya Wayahudi wenzao waliotoka kwa Yakobo (Myahudi) kufika hapo Antiokia. (Rejea Wagalatia 2:11-14).
Zaidi ya hivyo, tuliona pia Bwana Paulo jinsi alivyokuwa akimlaumu Petro kwa kitendo chake cha kuwashurutisha watu hao wa mataifa, yaani wapagani kufuata desturi za Wayahudi (yaani kufuata Torati ya Nabii Musa a.s.) akidai kwamba mwanadamu hatohesabiwa haki kwa matendo ya sheria (Torati); lakini kwa imani ya Kristo Yesu! (Rejea Wagalatia 2:14-16)
Kwa maelezo yake hayo, ikadhihirika kuwa Bwana Paulo alikwenda kwa watu wa mataifa (wapagani) kufuata dini yao ambayo kama tulivyoona, pia ilikuwa ina ibada zake wanazoifanyia miungu yao (miungu-watu) walioiamini kuwa ina desturi ya kujigeuza kuwa wanadamu.
Kwa hali hiyo, kwa kuwa Bwana Paulo anafuata mia kwa mia desturi za dini ya watu wa mataifa, yaani wapagani, tuliona kuwa huo ndio lazima utakaokuwa msimamo pia wa ibada za dini yake ya Kikristo.
Na ili kuthibitisha uhusiano huo (kati ya ibada za dini ya Paulo ya Kikristo na ibada za dini ya kipagani) hapana budi hapa nikazirejea japo kwa uchache ibada hizo za watu wa mataifa (wapagani) kama zilivyotajwa na Yehova; kisha tuzilinganishe na ibada za dini ya Kikristo, tuone jinsi kimsingi zinavyolingana.
Ibada hizo (za watu wa mataifa au wapagani) zimetajwa kwa uchache na Yehova alipokuwa akiwakemea wanadamu wajiepushe nazo kama ifuatavyo:
"Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA, kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako". (Kumbukumbu la Torati 18:9-12).
Bali walijichanganya na mataifa, wakajifunza matendo yao. Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao. Naam, walitoa wana wao na binti zao kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu". (Zaburi 106:35-38).
Katika maandiko hayo, Yehova kwa uchache tunaona amezitaja ibada hizo zisizopungua nane ambazo hufanywa na watu wa mataifa (wapagani) akiwataka wanadamu wajiepushe nazo mbali kabisa ili waweze kupata radhi yake hapa duniani na kesho huko akhera.
Kati ya ibada hizo za wapagani alizozikemea Yehova hapo juu, amezitaja pia ibada nne ambazo nimeziwekea alama ya maandishi meusi sana (bold) kwa ajili ya mazingatio katika uchambuzi ujao hapo punde.
Ibada hizo ni pamoja na kuua wana na binti (kama kafara), kupandisha pepo, kuwaomba wafu na kuzitumikia (kuabudu) sanamu.
Tuzitazamapo ibada hizi, tunaona ndizo leo zimekuwa ibada za msingi katika dini ya Kikristo mpaka dakika hii na hivyo kudhihirisha wazi uhusiano wa kimsingi kati ya ibada zake (Ukristo) na ibada za dini ya kipagani ambazo Yehova amewakemea vikali wanadamu kujishughulisha nazo kwa namna yoyote ile.
Mfano wa ibada kama hizo za wapagani zilizomo katika dini ya Kikristo mpaka leo ni kama zifuatazo:
Kuua wana
Hii ndiyo ibada kuu ya msingi katika dini ya Kikristo mpaka dakika ya leo.
Licha ya Yehova kuwakemea vikali wanadamu kujihusisha nayo, lakini sambamba na kuanzisha dini yake hiyo (Kikristo), Bwana Paulo aliamua pia kuifundisha ibada hiyo kwa kuunga mkono dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu (Nabii Isa au Yesu a.s.) kama kafara ya dhambi kwa waumini wa dini yake hiyo (Ukristo), kwa kusema:
"Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi" (Warumi 5:8).
"Kristo alitukomboa katika laana ya Torati kwakuwa alifanywa laana kwa ajili yetu, maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti". (Wagalatia 3:13)
Kwa uchache, hivi ndivyo Bwana Paulo aifundishavyo ibada hiyo (ya kuua wana) akiunga mkono dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu kama kafara ya dhambi za Wakristo wote.
Sambamba na mafundisho hayo ya Bwana Paulo juu ya ibada hiyo (kuua wana) waandishi wa agano jipya kwa kuwa nao walidhamiria kuuandikia Ukristo wa Paulo, kama ilivyo kazi yao (kusherehesha mafundisho ya Paulo) katika kusherehesha ibada hiyo kama ilivyofundishwa na "mwalimu wao" Bwana Paulo, katika Injili zao na nyaraka zao wamediriki hata kupenyeza maneno kinywani mwa Bwana Yesu (a.s.) wakisimulia kuwa Yesu mwenyewe (a.s.) ati aliwahi kutabiri kuuliwa kwake msalabani (Tazama Mathayo 12:40, 20:17-19; Marko 10:32-34; Luka 18:31-33 na kadhalika).
Nasema waandishi hao wamepenyeza ibada hiyo (ya kuua wana) kinywani mwa Yesu (a.s.) kwa sababu siyo wao tu, bali hata 'mwalimu wao' Bwana Paulo anajua wazi kuwa Bwana Yesu (a.s.) kamwe hawezi akathubutu kufundisha ibada potofu za watu wa mataifa, yaani wapagani, zilizokemewa vikali na Yehova.
Kwa upande mwingine, kutokana na mafundisho hayo ya Paulo yanayounga mkono ibada hiyo ya wapagani (ya kuuwa wana), katika kuunga kwao mkono na kutilia mkazo mafundisho hayo (ya Paulo), Wakristo pia wameibua kitu kiitwacho "Ekaristi takatifu", "Chakula cha Bwana", "Meza ya Bwana" na kadhalika. Hapo hula mikate na kunywa divai wakiashiria kuula mwili wa Yesu (a.s.) na kuinywa damu yake wakijifariji kwa dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu! Sambamba na hilo, pia wamezua "sikukuu ya Pasaka ya Yesu" kama kumbukumbu ya kutukuza dhana ya kuuliwa mwana huyo wa Mariamu kama kafara ya dhambi zao! Kwa ujumla, ibada hiyo ya kipagani inaungwa mkono mia kwa mia na dini ya Kikristo.
Kwa uchache, ibada hiyo (ya kuua wana) ni chukizo kubwa kwa Yehova kwa kuwa alikwishaikemea vikali. InshaAllah upotofu wa ibada hii nitauelezea zaidi katika makala zangu zijazo nitakapokuwa nikiwajibu wapinzani wote wa neno la Mungu waliojitokeza kuzidandia makala zangu zile zilizohusu "Pasaka wa kweli wa Mungu" ijapokuwa waliteleza kwa kufinyangafinyanga maneno wakitoa hoja dhaifu zisizokuwa na msingi wowote.