ZAFELA: Ushiriki wa Wanawake katika nafasi za maamuzi (hasa ya kisiasa) bado ni mdogo

ZAFELA: Ushiriki wa Wanawake katika nafasi za maamuzi (hasa ya kisiasa) bado ni mdogo

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Na Salma Said, Zanzibar

Ushiriki wa wanawake katika masuala uongozi ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele sana na watetezi wa haki za wanawake wakitaka kushirikishwa kikamilifu kama azimio namba tano la umoja wa kimataifa linalotaka asibakishwe mtu nyuma.

Wadau wanatambua kuwa kuna changamoto nyingi na vikwazo mbalimbali vinavyopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika kufikia kwenye malengo yao ikiwemo nafasi za uongozi kwenye ngazi tofauti.

Miongoni mwa vikwazo hivyo ni dini, mila na desturi, mfumo dume uliojikita katika nchi nyingi hasa za kiafrika, mitizamo hasi, sheria kandamizi, rushwa, dharau, utayari katika vyama vya siasa pamoja na ukatili na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake kwenye majukwaa ya kisiasa na hata katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla wake.

Hali hiyo imewafanya wanawake wengi kusimama na kuanza kupiga kelele za kutaka kushirikishwa kikamilifu katika nafasi na kutizama vikwazo vilivyopo na kuanza kuviepuka na kurekebishwa kwa sheria mbali mabli ambazo zinaonekana ni changamoto na kuwabakisha wanawake nyuma.

Kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu na maakazi ya mwaka 2012 takwimu zinaonyesha idadi ya wanawake ni zaidi ya 51% tu ambao wapo katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi ingawa hali hiyo inaanza kubadilika kutokana na sauti kupazwa na wanawake wenyewe kutaka washirikishwe kikamilifu katika ngazi za maamuzi na serikali hupata msukumo wa kutekeleza azimio la umoja wa kimataifa.
Wanawake wanaonekana ni wachache katika vyombo vya maamuzi ikilinganishwa na wanaume mnamo mwaka 1985 wanawake Bungeni 1985 Wanawake walikuwa 9% ya idadi ya wabunge wote
o 1995 Wanawake walikuwa 17% ya idadi ya wabunge wote
o 2000 Wanawake walikuwa 21% ya idadi ya wabunge wote
o 2005 Wanawake walikuwa 31% ya idadi ya wabunge wote
o 2010 Wanawake walikuwa 36% ya idadi ya wabunge wote
o 2015 Wanawake walikuwa 36.9% ya idadi ya wabunge wote

Halikadhalika kwa upande wa Zanzibar idadi ilikuwa ndogo ya wawakilishi wa wananchi kutoka kwenye majimbo ya uchaguzi.

Lakini kadiri siku zinavyokwenda na kutolewa elimu basi wanawake wamenza kuongezeka na sasa idadi ya wajumbe wanawake wa baraza la wawakilishi wameanza kuongezeka kutoka idadi ya wajumbe watatu kuanzia mwaka 1995 hadi kufikia wajumbe wanane wanaowania kwenye majimbo.

Wakati ambao wajumbe wanawake waliogombea majimboni wameongezeka zaidi ni mwaka huu wa 2021 ambao wanatarajia kuendelea hadi mwaka 2025 baada ya kukamilisha miaka mitano ya utumishi wao wa wananchi.

Idadi ya wajumbe wanane katika Baraza la kumi la mwaka huu wa 2021 ambalo linatarajiwa kumalizika mwaka 2025.
Mwaka 2016 -2020 katika baraza la tisa la wajumbe wanawake walikuwa jumla ni saba ambao waliwania nafasi hizo kufuatia kuteuliwa na kupitishwa kwenye kura za maoni ya vyama vyao ambao ni wote wakiwa kutoka Chama Cha Mapinduzi kutokana na kuwa chama cha upinzani kilisusia uchaguzi wa marejeo kwa kuwa uchaguzi wa 2015 waliushutumu kuvurugwa na kufutwa.

Baraza la nane la mwaka 2010 hadi 2015 wajumbe wanawake walikuwa watatu, Baraza la saba la 2005 hadi 2010 idadi ya wajumbe ilibaki ile ile ya wajumbe watatu wanawake kutoka kwenye majimbo ambapo mwaka huo.

Kwa mujibu wa takwimu za baraza la wawakilishi katika Baraza la tano lililoketi mnamo mwaka (1995 -2000) kulikuwa na wajumbe wanawake waliochanguliwa kutoka kwenye majimbo ni wanne pekee.

Pamoja na miongozo na matamko mbali mbali bado hali ya mwanamke kupewa fursa ya kushiriki na kushirikishwa kikamilifu katika ngazi za maamuzi inaonekana inahitaji kuongezewa kasi ya kupaziwa sauti pamoja na kufanyiwa mabadiliko kwa sheria mbali mbali.

Maazimio kadha ya viongozi wa dini kuitaka Serikali, watetezi wa haki za wanawake na wadau kuendelea kuhamasisha jamii juu ya umuhimu na haki wa wanawake kushiriki katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiuongozi.

Aidha viongozi wa dini wameonekana ni watu muhimu katika kusukuma ajenda za kuwainua wanawake na kutakiwa kupaza sauti zao kwenye mahubiri na madarasani wanaposomesha na kuendelea kukemea na kuzuia migogoro mbalimbali hasa lugha za kashfa dhidi ya wanawake katika majukwa ya kisiasa pamoja na kuhimiza wanawake waliopo kwenye nafasi kutetea na kupaza sauti juu ya haki za wanawake katika kushiriki kwenye siasa.

Vile vile viongozi wa dini wamekuwa wakiwahamasisha wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa kutumia mahubiri na vitabu vitukufu vya dini pamoja na kuielimisha jamii usahihi wa maandiko matakatifu kama Qoran na Biblia juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii.

“Tunapaswa kuielimisha jamii katika hali zote za maisha ya mwanaadamu kuwa anapaswa kuishi bila ya kubaguliwa na anaishi katika maisha ambayo anapewa nafasi ya elimu na nafasi nyengine za kimaisha tusitumie vitabu vya dini kuwanyima fursa wanawake” alisema Ustadh Mohammed Suleiman mwalimu wa Madrassa.

Professa Issa Ziddy ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ni miongoni mwa waandaaji wa nyaraka mbali mbali za kwenye makongamano zinazoeleza nafasi ya mwanamke katika jamii kwa kushiriki na kushirikishwa ikianzia kutakiw akupewa elimu na kushiriki masuala mengine ya maendeleo anaona hakuna katazo katika dini kumzuwia mwanamke asishirikishwe katika maamuzi ya nchi yake.

Anaona njia muhimu ni kuendelea kuwajengea uwezo wanawake kuanzia ngazi ya familia.

Ukiacha viongozi wa dini pia wanaharakati na watetezi wa haki za wanawake wamekuwa wakifanya juhudi ya kutaka kuondosha vikwazo kwa kuzipitia upya sheria mbali mbali ambazo huonesha kwa njia moja au nyengine zinamkandamiza mwanamke.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud Juma anasema jumuiya yake imeshafanya mapitio ya sheria mbali mbali zinazomkwaza mwanamke kushiriki katika ngazi za maamuzi ambapo jumla ya sheria nane zimepitiwa mwaka huu na kuona mapungufu yake ikiwemo (1) Sheria ya elimu – inamfukuza mtoto wa kike shuleni akiolewa (2) Sheria ya Uchaguzi- haoneshi uwiyano wa kijinsia katika kugombania nafasi za uongozi.(3) Sheria ya vyama vya siasa – hailazimishi vyama vya siasa kuweka uwiyano wa kijinsia katika nafasi za uongozi za chama na hata katika kugombea uongozi (4) Sheria ya Utumishi wa umma- inakataza watumishi kujiingiza kwenye siasa wakiwa watumishi na (5) Sheria ya Kuzuwia Rushwa- haijaweka wazi kosa la rushwa ya ngono kwenye uchaguzi.

ZAFELA imesema inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi (hasa ya kisiasa) bado ni mdogo, hali ambayo inakinzana na azma ya kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi kama ilivyobainishwa kwenye dira ya taifa 2017-2022, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na sheria mbalimbali za nchi zinazosisitiza usawa wa kijinsia.

Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ) na Shirika la PEGAO wanatekeleza Mradi wa (SWIL) wa miaka minne ulianza mwaka 2020 na unaotarajiwa kumaliza 2023 na kufadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

Miongoni mwa jukumu la ZAFELA katika utekelezaji wa mradi huo ni kufanya mapitio ya sera na sheria, kuwajengea uwezo asasi za kiraia zipatazo 60 juu ya uhamasishaji na ushawishi (advocacy) kwa wanawake kuweza kushiki katika masuala ya Demokrasia, siasa na uongozi.

Jukumu jengine ni kusimamia mikutano, midahalo na makongamano ya uhamasishaji wa kijamii ili kuwajengea uwezo na hoja washiriki wa mikutano hiyo kujua umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi.

Mradi unategemea kupata matokeo chanya ambapo jumla ya wanawake 6,000 wanategewa kufikiwa katika kipindi chote cha utekelezaji katika wilaya mbali mbali za Zanzibar.

“Tunategemea kuona wanawake wengi wanashiriki katika ngazi za maamuzi pamoja na kugombea nafasi mbali mbali za kisiasa na kushiriki katika masuala ya kidemokrasia, na mimi naamini chini ya mradi huu wanawake wengi wanajitokeza mwaka 2025 kutaka kuwania nafasi za uongozo katika ngazi ya chini hadi ngazi za juu” alisema Jamila Mahmoud.

ZAFELA ambayo baadhi ya malengo yake makuu ni utetezi wa haki za wanawake na watoto, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuondoa mifumo kandamizi inayochochoa udhalilishaji wa kijinsia kwa makundi hayo, kwa kufanya ushawishi (advocacy), utetezi pamoja na kufanya mapitio ya sheria na sera mbali mbali zinazomhusu mwanamke inaona ina fursa bado ya kutimiza malengo yak echini ya mradi huo.

Katika mradi huo ni kuongeza uelewa kwa umma kuhusu umuhimu wa ushiriki wa Wanawake katika siasa, demokrasia na Uwongozi kwa kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi.

“Katika kufanikisha lengo kuu la mradi huu, ZAFELA imewajengea uwezo wahamasishaji jimii (Community Brigades) wapatao 60 kutoka Mikoa mitatu ya Unguja katika kuhamasisha jamii kupitia makundi mbali mbali ya vijana wanawake na wanaume na kuwapa uwelewa wa umuhimu wa kuwashirikisha wanawake katika nyanja zote bila ya kujali jinsia zao” alisema Mkaurugenzi huyo.

Katika hatua nyengine ZAFELA, inakusudia kuendesha midahalo kupitia wahamasishaji jamii kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa, demokrasia na uongozi kuanzia ngazi ya shehia, wilaya hadi mkoa.
IMG-20210909-WA0004.jpg

Mkurugenzi wa Jumua ya Wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud (katikati)kushoto mratib wa mradi wa kuwawezesa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi Khairat Hamid na kulia ni mratib wa mradi huo kutoka TAMWA-ZNZ Salma Amir Lusangi walipokua wakizungumza na waandishi wa habari.
 
Kwa nini mnakomalia maamuzi ya wanawake yawe makubwa?
Mbona sisi hatukomalii maamuzi ya chakula, viungo vya mboga wala vicoba?
Wanawake kubalini kuwa wanawake. Fullstop
 
Kwa nini mnakomalia maamuzi ya wanawake yawe makubwa?
Mbona sisi hatukomalii maamuzi ya chakula, viungo vya mboga wala vicoba?
Wanawake kubalini kuwa wanawake. Fullstop
Tena hata waliopo asilimia kubwa hawana mchango wowote,
Mfano Wabunge wa viti maalumu uwepo wao bungeni hauna tija zaidi ya kugonga meza na kuwatukana Wabunge wa upinzani kipindi kie walikuwepo.
 
Back
Top Bottom