Ukweli ulio wazi ni kwamba filamu za Kibongo ni dhaifu sana, na hatuwezi kukuza filamu za Kitanzania kwa kubeza tu udhaifu wake, bali kwa kukosoa mahali wanakokosea, na ni lazima tuziunge mkono kwani nazo sasa zinachangia pato la Taifa na kwa kiasi fulani zinatoa ajira binafsi kwa watu wenye viwango mbalimbali vya elimu.
Ieleweke kuwa, hakuna filamu iliyowahi kutengenezwa duniani bila kuwa na makosa (mchemko) yoyote, ila filamu yenye makosa machache ndio filamu bora, na yenye makosa mengi ndio filamu mbovu. Hivyo akina
chige (Bongo Movies) waongeze ujuzi na bidii katika kupunguza makosa kwenye filamu zao ili ziwe bora.
Kwa utafiti wangu mdogo nimegundua kwamba tatizo kubwa la kwenye tasnia ya filamu ni kukosa utaalamu, kwa maana ya kutegemea kipaji pekee katika kazi zao. Pia, kutengeneza filamu kwa budget ndogo, ambayo haitoshi kuweza kuchukua kampuni zenye wataalamu wa kutengeneza filamu zao.
Bila shaka wengi wetu tumesikia gharama zinazotajwa na wanamuziki kwa kutengeneza video tu ya muziki zisizozidi dakika saba. Kwa maana hiyo filamu zetu zinahitaji uwekezaji wa uhakika sio mwekezaji asiyetaka kuwekeza kwa msanii, badala yake anafikiria kumkomoa msanii.
Kitu kibaya wanachofanya hawa wasanii wa Bongo Movies, ni kuamua kubaguana (au kufanywa wabaguane), kwa misingi ya umaarufu, kuwa na uwezo kifedha, kuwa chipukizi au kuwa na uwezo mdogo kifedha. Hii inawafanya washindwe kuwa na kauli ya kuwasaidia kwa umoja wao.
Nadhani miaka mitatu au minne iliyopita, script writers wa Hollywood waligoma kwa ajili ya kushinikiza kupanda kwa maslahi yao, na kweli shughuli ya utengenezaji wa filamu mpya zikazimama nadhani kwa muda wa mwezi mmoja hadi wakasikilizwa madai yao, kisha kazi kuendelea.
Sasa kwa mgogoro wao wa sasa alichofanya Steps ni kuwachukua wasanii wachache kisha kuwaahidi pepo ya dunia kwa makubaliano ya kumtetea, kwa kuwa wanaijua shida yao ni kuwa na pesa za kuwaonesha watu kuwa wanazo pesa nyingi na magari ya fahari. Wamemtii Steps na wamewageuka wenzao.
Wakati Kanumba akiwa hai alikuwa akiendesha Lexus nyeusi, lakini ilikuwa na mambo mengi nyuma ya pazia. Kwa gari lile alikuwa na deni la filamu nne kwa Steps, na bado gari lile alilipa nusu, hivyo bado alikuwa anadaiwa. Alifanikiwa kuacha filamu mbili ambazo zilitoka baada ya kifo chake, na akafa na deni la filamu mbili.
Nini kilichotokea baada ya kifo chake? Mwenye gari akadai sehemu iliyobaki ya pesa yake, ikabidi gari liuzwe kwa bei ya hasara, kisha likalipwa deni. Kwa bahati mbaya marehemu alikuwa na madeni mengine ya msingi, ikabidi mali zake nyingine ziuzwe ili kuyalipa, na baada ya miezi mitatu hakukuwa tena na mali inayoweza kuitwa ya Kanumba.
Na hilo ndilo lililofanya Mama Kanumba awalilie Steps angalau wampe sehemu ya mauzo ya filamu mbili alizoacha, lakini akaambiwa marehemu alishalipwa na bado anadaiwa. Ndipo aliposhauriwa acheze filamu ya maisha ya Kanumba, akacheza na haikufanya vizuri, akasogezwa mbali kabisa na sasa ameshasahaulika.
Tatizo la hawa wasanii wanapenda kujionesha kwamba wana uwezo mkubwa kipesa na wananufaika sana kwa mapato ya filamu zao, ndilo ambalo huwafanya wakose utetezi, lakini ukweli ni kwamba wana hali mbaya. Baada ya kifo cha Kanumba, JK ndipo alipopata fursa ya kuujua ukweli juu ya wasanii wa filamu, akasikitika sana na kuamua kufanya nao kikao binafsi, Ikulu.
Na alichosema JB kwenye hicho kikao, nadhani ndicho kilichofanya Rais aanze kuwa nao mbali mpaka hii leo. Nikipata muda baadaye nitaeleza kuhusu hicho kikao, kwani nilikuwepo kikaoni licha ya kwamba sio mmoja wa hao wasanii wa filamu, majukumu yangu ndio yalifanya niwe pale. Huwezi jua pengine nilikuwa muandaa juice ya wageni (hahahahahaaa).
Ova