Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 2,203
- 5,610
Ziara hiyo ya Dkt. Hussein Mwinyi ni ya kwanza kuifanya mara tu baada ya kushika wadhifa wa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambapo alifika bandarini hapo kujua sababu zinazopelekea kuchelewa kushushwa kwa mizigo, mlundikano wa makontena pamoja na meli kukaa kwa muda mrefu nje ya Bandari hiyo.
Katika maelezo yake Dkt. Hussein Mwinyi alisisitiza kufanyika jitihada za makusudi za kutafuta ufumbuzi wa kuondoa makontena bandarini hapo kwa lengo la kuondosha usumbufu na mlundikano wa makontena katika eneo hilo.
Rais Mwinyi alisema kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana bandari na pale pasipokuwepo ufanisi katika utendaji wa shughuli zake ni dhahiri kwamba uchumi hauwezi kuimarika.
Aliongeza kwamba katika hali ya sasa kuna meli zinateremsha mizigo katika bandari za Mombasa na Dar es Salaam na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara kiasi ambacho huwasababishia kupata hasara.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara walioamua kutokuleta mizigo yao Zanzibar kutokana na mizigo yao kukaa kwa muda mrefu, hivyo alisisitiza haja ya kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Rais Dkt. Hussein aliutaka uongozi huo wa bandari kuongeza kasi ya ushushaji wa mizingo ili kupunguza muda wa kukaa meli muda mrefu nje ya bandari.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa kumekuwepo changamoto ya kupanda bei kwa bidhaa kiholela kutokana na utendaji wa bandari.
Alisisitiza haja ya kuwepo kwa eneo la kuweka makontena (bandari kavu) ili kuondosha mlundikano wa makontena katika eneo hilo la bandari ya Malindi.
Hivyo, Rais Dkt. Hussein aliusisitiza uongozi huo haja ya kuwajibika kwa kufahamu kuwa bandari ni kitovu cha uchumi wa nchi huku akizuia utumiaji wa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuweka makontena (bandari kavu) huko Maruhubi.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliutaka uongozi huo kutumia fedha walizonazo ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za bandari.