Zanzibar kuja na sheria ya adhabu za papo kwa papo kwa madereva ili kupunguza ajali za barabarani

Zanzibar kuja na sheria ya adhabu za papo kwa papo kwa madereva ili kupunguza ajali za barabarani

Miss Zomboko

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2014
Posts
4,599
Reaction score
9,532
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inakusudia kutunga Sheria ya Adhabu ‘’papo kwa papo’’ ili kudhibiti ajali, ambazo zimekuwa zikisababisha vifo vya wananchi wengi wa Zanzibar.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mustafa Aboud Jumbe wakati akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtuhaliwa hadi Chokocho na Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na uzembe, unaotokana na madereva kushindwa kufuata sheria za barabarani. Alisema wapo madereva wanadharau sheria na alama za barabarani, ambapo njia pekee ya kudhibiti ajali ni kuweka sheria kali, ikiwemo kunyang’anywa leseni kwa dereva aliyesababisha ajali.

‘’Tunafikiria kutoa adhabu za faini papo kwa papo kwa ajili ya kudhibiti ajali, ikiwemo kuwanyang’anya leseni madereva wanaosababisha ajali hizo,’’alisema.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk.Sira Ubwa Mamboya alisema mtandao wa barabara katika Kisiwa cha Pemba, umeimarishwa kwa kiasi kikubwa kwa lengo la kurahisisha huduma za usafiri.

Alisema mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 1,561, umeimarishwa hadi vijijini na kusaidia juhudi za wananchi katika kuimarisha kilimo.

‘’Tunaendelea na kazi za kuimarisha miundombinu ya barabara hadi vijijini kwa ajili ya kuimarisha huduma za mawasiliano na usafirishaji,’’alisema.

Mapema, akifungua barabara hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema ujenzi wa barabara hadi vijijini ni moja ya hatua muhimu ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

Aliwataka wananchi ambao barabara imepita katika maeneo yao kuwa walinzi wazuri na kamwe wasikubali matukio ya uharibifu, yatakayofanywa na watu wachache, kwa sababu barabara zinatumia fedha nyingi za walipa kodi.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 5.6, umegharimu Sh milioni 570 na utasaidia maeneo ya kilimo cha karafuu.
 
Back
Top Bottom