Binafsi naitafakari kauli ya Zitto Zuberi Kabwe na ninafurahi kuona kuwa kile nilichoonya kuwa kijana mwenzangu anatumiwa vibaya na ccm sasa kimetimia.
Wakati akihojiwa katika kipindi kiitwacho, Exclusive interview na Millard Ayo cha Clouds FM
Amesema hivi nanukuu Wazee wetu walitusaidia kutupatia maendeleo ya kisiasa, sasa ni jukumu letu kuleta maendeleo ya kiuchumi. Ila naomba nisisitize, jukumu hili haliwezi kutekelezwa na mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya uhuru, na ninatangaza kuwa nitagombea urais mwaka 2015?
Naunga mkono kwamba vijana tujitokeze kuleta maendeleo kwa taifa letu, lakini napingana vikali kauli jukumu hili haliwezi kutekelezwa na mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya uhuru
Kwanza mimi nasema amewatukana wazee wote Tanzania, huku ni kukosa busara heshima na hana sifa ya Uongozi kwani ni mbaguzi. Wapo Wazee waliozaliwa kabla ya uhuru na wanailetea Tanzania maendeleo na wapo wapuuzi waliozaliwa baada ya uhuru ni wapuuzi wa kutisha yeye akiwemo. Zitto hana busara kwa hili
Amejisemea bila kufikiri. Ana maanisha hata kama mtu ni msomi kama akina Dr Slaa, Dr Gharibu Bilali mtaalamu wa nyuklia na Prof Lipumba hawawezi kusaidia isipokuwa wale waliozaliwa baada ya uhuru? Huu ni uhuni wa kawaida wa Zitto ambaye hujitahidi kujionyesha kama thinker wakati siyo hasa ikizingatiwa hata akiwa shule alipita hivyo hivyo.
Nadhani kwa thinker mzuri hana haja ya kuwatenga watu kwa umri wao bali tabia zao hasa linapokuja suala zima la ujenzi wa taifa. Mbona tuna vijana waliozaliwa baada ya uhuru kama yeye mwenyewe Zitto na wengine lakini bado ni mafisadi???
Kitendo cha kutangaza nia ya kugombea urais 2015 sio kibaya kwakuwa ni haki yake kikatiba, lakini kutangaza nje ya ya utaratibu wa chama chake huu ni uhaini kwa chama. Zitto anajua anachokifanya, na anajua matokeo yake lakini ni jambo la kusikitisha kuwa hajui madhara yake kwake.
Katika tafakuri yangu kwa mapana ya nera, nikamkumbuka mwalimu wangu pale Moscow Urusi, Prof Radav Metbarg aliyenifundisha uhandis wa umeme, huyu alinidokeza aina ya binadamu, hakika ilikuwa muhimu sana ndio maana leo imenijia akilini nikalazimika kuzama kimangamuzi zaidi, nimefanya hivyo ili nimtambue huyu mtu aitwae Zitto Kabwe kiundani zaidi, Katika aina za binadamu Zitto ni wa aina ya Sanguine, hii ni kwamujibu wa tabia zake za kisiasa. Hakika naamini watu wa aina hii ni hatari hasa ukiwasogeza jirani na uongozi popote pale basi wanaouwezo na msukumo mkubwa wa kukupindua. Hiyo ni sehemu ya sifa ya watu wa aina hiyo na kwa ujumla ni waroho wa madaraka.
Lakini najiuliza kwani Magharibi mwa Tanzani ndiko aina hii ya watu inapatikana kweli au yeye ni chipuzi tu? Nikiangalia wenye tabia zake nawaona kama Kafulia, Mkosamali na Shibuda. Lakini sitaki kujikita katika dhana hiyo ya ukanda bali nasimamia kuwa hao ni chipuzi la aina hiyo ya tabia za binadamu ambao ni hatari hasa uwasogezapo katika vyeo vya juu basi huutaka ufalme hata kwa njia ya uasi tu. Muono wangu ni kuwa Zitto hautaki urais na anajua fika kuwa kwa mujibu wa katiba iliyopo yeye hastahili kugombea URAIS, ila kwa gharama kubwa amejichimbia msituni kukihujumu chama chake kilichomlea na kumfanya leo ajione fahali la masika.
Ninarudia tena Zitto hana nia ya urais, nasema hana hata chembe za kuutaka urais ila analengo moja tu nalo nikukivuruga Chama chake tu. Mwili wa Zitto upo Chadema ila moyo wake upo ccm palipo panono, kweli pesa mwanaharamu.
Lakini wadadisi wa siasa za Afrika tunapaswa kulaumiwa sana, tulipopokea mageuzi ya siasa za kidemokrasia na kuziacha siasa zetu za kiimla lakini tulishindwa kupokea hata miundo ya siasa hizo, mathalani vyama vya siasa vyenye ukwasi wa kidemokrasia huwa na utaratibu wa kutengeneza viongozi wa chama, kitaifa na viongozi wa kimataifa. Hili nadhani hata Hayati Mzee Nyerere alifanikiwa kuliasisi lakini baada ya kufariki mabaka demokrasia wamebaka na kubuni mifumo ya kuzalisha watawala sio kuzalisha viongozi tena.
Hili lisiwe turufu kwa Zitto, naamini anatambua njia aipitayo na madhaifu ya muundo huu wa vyama vyetu vya siasa. Ningefurahi na ninaamini wadadisi wote wa siasa za Afrika wangefurahi pia kama Zitto angeanzisha harakati za kuboresha muundo wa vyama vyetu vya siasa hususani Chama chake cha Chadema kilichobeba tumaini kuu la wazalendo na wengi wa nchi hii. Je ccm ya leo bado inautaratibu wa kuandaa vijana kwaajili ya siasa za kesho? kwaajili ya urais? kwaajili ya wanadiplomasia wa kimataifa wakesho? Chadema je? UDP je? NCCR je?
Jambo la kumshukuru Mungu nikuwa Chadema wanajua kila anachokifikiria kufanya, anachokifanya, anakolalia, anakoamkia, anakokutania na wafadhiri wa uasi huu na kila kitu. Kwaujumla chama kinamjua utosi hadi unyayo.
Chadema wamekuwa wakipigana vita mbili kwa mda mrefu, vita hiyo ni ya nje (ccm) na ndani (Zitto, Shibuda na mamluki wengine) lakini mda wote chadema imeshinda na itashinda na itaendelea kushinda daima kwakuwa ni vita kati ya wema na ubaya kumbuka na elewa kuwa kwenye wema Mungu yupo.
Ninachoamini katika siasa duniani ni kuwa hakuna aliyejuu ya chama chake.