BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 706
- 1,716
Andiko la Haika Kimaro, Kilimanjaro
Ziwa Jipe, lililopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, linakabiliwa na tishio kubwa la kupoteza uhai wake wa kiikolojia kutokana na kuongezeka kwa magugu maji, kupungua kwa kina cha maji, uharibifu wa mazingira na shughuli za kibinadamu zisizozingatia misingi ya uhifadhi.
Hali hiyo inatishia maisha na uchumi wa maelfu ya wananchi wanaolitegemea ziwa hilo kwa shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji na matumizi mengine ya kila siku. Vilevile, inahatarisha uhai wa viumbe mbalimbali, wakiwamo samaki adimu wa asili wanaojulikana kama Jipe Tilapia, ambao wanatajwa kuwa katika hatari ya kutoweka duniani.
1. Mkazi wa Kijiji cha Jipe wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro akitoka kuvua katika ziwa Jipe.
Picha na Haika Kimaro.
2. Wananchi wa kijiji cha Butu wakitoka kuvua samaki katika ziwa Jipe.
Picha na Haika Kimaro
Ziwa Jipe ni rasilimali muhimu ya maji inayotumiwa na wananchi wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, upande wa Tanzania, pamoja na wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta nchini Kenya.
Umuhimu wake hauishii katika shughuli za kibinadamu pekee. Ziwa hilo ni sehemu ya mfumo wa ikolojia unaotegemewa pia na wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi nchini Tanzania na Hifadhi ya Tsavo Magharibi nchini Kenya, pamoja na ndege, samaki na viumbe wengine wa majini.
Aidha, Ziwa Jipe linachangia maji yanayoingia katika Mto Ruvu, ambao ni miongoni mwa mito mikuu inayolisha Bwawa la Nyumba ya Mungu, mkoani Kilimanjaro.
Video ya mwalo unaotumiwa na wakazi wa Kijiji cha Jipe kuingia katika Ziwa Jipe, mwalo huo pia umezungukwa na magugu maji vile inaonekana.
Wadau wa mazingira na watumiaji wa ziwa hilo wanahofia kwamba kuendelea kuzorota kwa hali yake kunaweza kuathiri mtiririko wa maji katika mfumo huo na, hatimaye, shughuli zinazotegemea Bwawa la Nyumba ya Mungu, ikiwamo uzalishaji wa umeme.
Uchunguzi wa miezi miwili wafichua ukubwa wa tatizo
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa takribani miezi miwili umebaini kuwa, licha ya kuwepo kwa viashiria vya hatari inayolikabili Ziwa Jipe, juhudi za kulinusuru bado hazijafikia kiwango kinacholingana na ukubwa wa tatizo.
Magugu maji yameenea katika maeneo mbalimbali ya ziwa, yakizuia shughuli za uvuvi, kupunguza maeneo ya maji yaliyo wazi na kufanya baadhi ya njia zinazotumiwa na wavuvi kutopitika.
Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu waliohojiwa, kina cha maji katika maeneo mengi ya ziwa hilo kimepungua, huku utafiti mmoja ukionesha kuwa sehemu kubwa zina kina cha kati ya mita moja na mbili na maeneo yaliyopimwa hayakuzidi mita tatu.
Kwa upande wa Tanzania, wananchi wa vijiji vya Jipe, Butu, Ruru na Kambi ya Simba ni miongoni mwa wanaotegemea zaidi ziwa hilo kuendesha maisha yao ya kila siku. Wakazi wengine wa Tarafa ya Jipe pia hunufaika na rasilimali hiyo.
4. Muonekano wa mwalo unaotumiwa na wavuvi wa kijiji cha Jipe, kuingia katika ziwa Jipe kwa ajili ya uvuvi. Picha na Haika Kimaro
Hata hivyo, kupungua kwa upatikanaji wa samaki, kuongezeka kwa magugu maji na changamoto za usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo vimezua hofu kuhusu mustakabali wa maisha ya jamii zinazolizunguka.
Uchunguzi umeonesha kuwa maeneo ya upande wa Tanzania yanaonekana kuathiriwa zaidi na magugu maji kuliko baadhi ya maeneo ya upande wa Kenya, hali inayohusishwa na mwelekeo wa upepo, tabia ya magugu hayo na tofauti za hatua za uhifadhi na usimamizi.
Wavuvi waacha shughuli zao, kipato chaporomoka
Omari Ramadhani, mkazi wa Kijiji cha Jipe na baba wa watoto watano, ni mmoja wa wananchi walioathiriwa na mabadiliko ya mazingira ya ziwa hilo.
Baada ya kujipatia riziki kupitia uvuvi kwa takribani miaka 11, amelazimika kuhamia katika shughuli za kilimo kutokana na kupungua kwa samaki na kuongezeka kwa magugu maji.
5. Muonekano wa mwalo (mlango wa kuingia ziwani) unaotumiwa na wavuvi katika kijiji cha Jipe kuingia katika ziwa hilo kwa ajili ya shughuli za uvuvi.
Anasema hali ya sasa inatishia siyo tu shughuli za uvuvi, bali pia uwepo wa ziwa lenyewe katika miaka ijayo.
“Hata kama halitakufa sasa, miaka ijayo halitakuwepo. Magugu maji yamekuwa mengi sana. Hata yakioza yanageuka kuwa kama mbolea au udongo, kisha yanatengeneza kitu kama kisiwa na kuendelea kuzaliana kwa kasi,” anasema Ramadhani.
Anaeleza kuwa wakati wa mvua, magugu maji hukusanyika na kutengeneza mafungu makubwa yanayofanana na visiwa vinavyoelea na kuhama kulingana na mwelekeo wa upepo.
“Wakati wa mvua visiwa vinajikata na kuhama kulingana na uelekeo wa upepo. Kwa wenyeji, tunajua jinsi ya kupita na kurudi nchi kavu, lakini wakati mwingine wapo wanaokwama na hulazimika kuokolewa,” anasema.
Ramadhani anasema athari nyingine imeonekana katika kupungua kwa ukubwa wa samaki wanaovuliwa.
“Zamani ulikuwa unaweza kuvua samaki wa inchi tatu hadi tano, lakini siku hizi wapo wanaovua hata samaki walio chini ya inchi moja,” anaeleza.
Kwa mujibu wake, samaki wakubwa hupatikana kwa nadra, hasa wakati wa mvua kubwa, pale magugu yanapohamishwa na upepo na kuwafanya samaki waliokuwa wamejificha kujitokeza katika maeneo yenye maji ya kina kifupi.
Anasema hali hiyo inaweza kudumu kwa siku mbili au tatu kabla ya samaki hao kupotea tena.
Akikumbuka hali ya uvuvi kabla ya mwaka 2016, Ramadhani anasema mvuvi mmoja angeweza kupata mapato ya kati ya Sh50,000 na Sh300,000 kwa siku, tofauti na hali ya sasa.
Hofu kuhusu mustakabali wa Bwawa la Nyumba ya Mungu
Hassan Salleh, mvuvi kutoka Kijiji cha Kambi ya Simba, anaeleza kuwa athari za kuharibika kwa Ziwa Jipe zinaweza kuvuka mipaka ya sekta ya uvuvi na kuathiri pia rasilimali nyingine zinazotegemea maji yake.
Anahofia kwamba endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, kupungua kwa maji ya ziwa hilo kunaweza kuwa na athari kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu.
“Ziwa Jipe ndiyo ziwa mama la Bwawa la Nyumba ya Mungu. Bila maji ya uhakika, uzalishaji wa umeme unaweza kuathirika. Kwa miaka mingi Kilimanjaro imekuwa ikitegemea umeme kutoka bwawa hilo. Hata kama sasa kuna vyanzo vingine, ni muhimu kuvilinda vyote,” anasema Salleh.
Mbali na changamoto za mazingira, Salleh anataja udhaifu wa usimamizi wa rasilimali za ziwa hilo kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa tatizo.
Kwa maoni yake, hakuna uratibu wa kutosha baina ya taasisi zinazohusika na uhifadhi, matumizi ya maji, uvuvi na usimamizi wa mazingira.
Anasema hali hiyo imechangia matumizi yasiyo endelevu ya ziwa na kusababisha baadhi ya changamoto kuendelea kwa muda mrefu bila ufumbuzi wa kudumu.
“Halmashauri imeelekeza nguvu zaidi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, kana kwamba huko ndiko kuna mapato. Lakini hatari iliyopo hapa inaweza kuwa kubwa zaidi baadaye. Wanashindwa hata kutujengea mwalo,” analalamika.
Meshack Seleman mvuvi katika Ziwa Jipe, akizungumzia uharibifu wa ziwa
Anasisitiza kuwa ukubwa wa tatizo umefikia hatua inayohitaji ushiriki wa Serikali Kuu na ushirikiano wa taasisi zote zinazohusika.
Magugu maji yamekuwa yakiongezeka tangu miaka ya 1980
Omary Salim, mkazi wa Kijiji cha Butu, anakumbuka hali ya Ziwa Jipe ilivyokuwa mwaka 1981, wakati magugu maji yalipokuwapo kwa kiasi kidogo na hayakuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za uvuvi.
Anasema wakati huo magugu hayo yalikuwa sehemu ya mfumo wa kawaida wa ikolojia ya ziwa, tofauti na sasa ambapo yameenea katika maeneo makubwa.
“Kama kweli wewe mwandishi wa habari uko hapa kutusaidia, tunaomba Serikali ije ione hali halisi na tushirikiane kutafuta namna ya kudhibiti magugu maji. Sasa hivi wanavuliwa samaki wadogo ambao hawafai, na hata upatikanaji wao ni mdogo,” anasema Salim.
Anaeleza kuwa juhudi za kukabiliana na tatizo hilo zinapaswa kwenda sambamba na kudhibiti uvuvi wa samaki wachanga na kufanya doria za mara kwa mara.
“Tunaomba Serikali isimamie ili samaki wadogo wasivuliwe. Ikiwezekana tupewe askari wa ulinzi na tupumzishe uvuvi hata kwa miezi minne. Tunaamini hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza tatizo la samaki wadogo, wakati huo huo tukidhibiti magugu maji,” anasema.
Salim pia anaitaka Serikali kuwapatia vitendea kazi, ikiwamo boti yenye injini na askari wa kutosha kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za uvuvi.
Aidha, anatoa madai kuhusu baadhi ya askari kutoka upande wa Kenya kuingia katika maeneo ya Tanzania kwa kisingizio cha kufanya ulinzi, huku akidai kuwa baadhi yao hunufaika binafsi na shughuli za wavuvi.
Madai hayo yanahitaji majibu kutoka mamlaka husika za pande zote mbili.
Mwenyekiti wa kijiji: Ziwa sasa linatoa samaki wa mboga tu
Mwenyekiti wa Kijiji cha Jipe, Hatibu Musa, anasema kuongezeka kwa magugu maji kumepunguza maeneo ya uvuvi na kuathiri kwa kiasi kikubwa kipato cha wananchi.
Kwa mujibu wake, samaki wanaopatikana sasa ni wachache kiasi kwamba sehemu kubwa hutumiwa kwa chakula cha familia badala ya kuuzwa katika masoko.
“Ziwa Jipe sasa siyo ziwa la kuvua samaki wa biashara; ni ziwa la kuvua mboga ili watoto wa maeneo ya hapa kijijini wapate kula,” anasema Hatibu.
Anaeleza kuwa magugu maji yamekuwa yakijikusanya na kutengeneza mafungu makubwa yanayohama kutokana na upepo, na wakati mwingine kuziba kabisa njia za kuingilia ziwani.
Hali hiyo huwalazimisha wavuvi kufungua njia mpya ili waweze kuingia na kutoka ziwani.
“Kutoka Kijiji cha Ruru hadi Kijiji cha Jipe kuna wastani wa kilomita 20. Eneo hilo limejaa magugu maji, wakati zamani lilikuwa maji,” anasema.
Mapato ya serikali ya Kijiji yapungua
Athari za kupungua kwa shughuli za uvuvi zimefika pia katika ukusanyaji wa mapato ya serikali za mitaa.
Hatibu anasema kutokana na kupungua kwa samaki wanaovuliwa, shughuli za biashara ya samaki zimezorota na hivyo kupunguza fursa za ukusanyaji wa ushuru.
“Tunaye mkusanya ushuru aliyeletwa na halmashauri, lakini kwenye samaki hakuna ushuru. Labda kama anapata ushuru wa fito na mkaa, lakini kwenye samaki hakuna,” anasema.
Hali hiyo inaonesha kuwa athari za uharibifu wa mazingira ya ziwa haziishii kwa wavuvi pekee, bali pia zinaweza kudhoofisha mapato yanayohitajika kugharamia huduma za kijamii na maendeleo ya maeneo husika.
Upande wa Kenya wachukua hatua za uhifadhi
Samson Morgan, mvuvi wa Ziwa Jipe kutoka upande wa Kenya, anaeleza kuwa kwao kuna mfumo wa usimamizi wa shughuli za ziwa unaohusisha viongozi wa maeneo husika, Serikali na wadau wengine wa uhifadhi.
Anasema wakati mwingine wanapata msaada kutoka kwa mamlaka na wadau wa Hifadhi ya Tsavo Magharibi katika kuhakikisha kuwa mazingira ya ziwa yanaendelea kuhifadhiwa.
“Magugu maji yapo, lakini kuna wakati Serikali inatusaidia kutengeneza njia ya kuingilia ziwani. Wakati mwingine tembo wanatusaidia kuyapunguza kwa sababu ni chakula chao,” anasema Morgan.
Anaeleza kuwa uwepo wa hifadhi ya wanyamapori umechangia kuimarishwa kwa ulinzi na udhibiti wa shughuli za kibinadamu katika baadhi ya maeneo yanayozunguka ziwa.
Kwa mujibu wake, doria na udhibiti wa watu wanaoingia katika maeneo ya hifadhi husaidia kupunguza vitendo vinavyoweza kuharibu mazingira.
Bonde la Pangani lakiri ukubwa wa tatizo
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani, Segule Segule, anakiri kuwa Ziwa Jipe limeathiriwa na kuongezeka kwa magugu maji.
Hata hivyo, anasema ili kuthibitisha kisayansi ukubwa wa mabadiliko ya eneo na kina cha ziwa hilo, ni lazima kufanya vipimo vya kina vinavyohusisha maeneo yote ya ziwa.
Anaeleza kuwa magugu yaliyopo siyo yale yanayoelea juu ya maji pekee, bali pia yapo yanayojikita katika maeneo ya chini ya ziwa.
“Unaposema ziwa limepungua, hatuangalii eneo la mwanzo pekee. Tunaangalia mwenendo wa ziwa lote. Sasa hilo halijafanyika, kwa hiyo kisayansi hatuwezi kuthibitisha kwa takwimu kwamba limepungua. Lakini kutokana na kuongezeka kwa magugu, tunaamini kuna mabadiliko,” anasema Segule.
Anabainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia kupungua kwa kina cha maziwa ni kujaa kwa mashapo yanayosafirishwa na maji kutoka maeneo ya juu ya mabonde.
Kwa upande wa Ziwa Jipe, anasema uchunguzi zaidi unahitajika ili kubaini kwa usahihi aina na kiasi cha mashapo hayo.
Anataja shughuli za kibinadamu, hususan kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji na milimani, kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza mashapo yanayoingia ziwani.
“Ziwa lenyewe tunavyoliona, tunasema limepoteza kina. Na linapopoteza kina, linapoteza pia kiasi cha maji linachoweza kuhifadhi,” anasema.
Changamoto ya usimamizi wa rasilimali ya nchi mbili
Segule anaeleza kuwa Ziwa Jipe ni rasilimali ya maji inayoshirikishwa na Tanzania na Kenya, hivyo juhudi za kulihifadhi zinahitaji ushirikiano wa nchi zote mbili.
Anasema baadhi ya maji yanayoingia ziwani yanatoka upande wa Kenya, ambako mamlaka za Tanzania haziwezi kusimamia moja kwa moja shughuli zinazofanyika.
Kwa sababu hiyo, mazungumzo na uratibu kupitia vikao vya ujirani mwema na mifumo ya ushirikiano wa mipakani ni muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Anaongeza kuwa matumizi ya kemikali za kilimo katika maeneo ya juu ya bonde yanaweza kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia mabadiliko ya mazingira ya ziwa, ingawa uchunguzi wa kisayansi unahitajika kuthibitisha kiwango cha mchango wake.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa, Segule anasema wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Jeshi la Magereza, katika jitihada za kuondoa magugu maji.
“Tunaendelea na jitihada, ikiwamo kushirikiana na wadau kama TANESCO na Magereza kwa lengo la kuondoa magugu. Pia tuliandaa andiko la kuomba ufadhili wa mtambo wa kuvuna magugu maji, lakini bado hatujafanikiwa,” anasema.
Aidha, anasema wamekuwa wakishirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela katika tafiti zinazohusu mazingira na viumbe hai vinavyopatikana katika magugu maji ya ziwa hilo.
Anasisitiza kuwa kuondoa magugu bila kushughulikia sababu zinazochangia kuongezeka kwake hakuwezi kutoa ufumbuzi wa kudumu.
“Jitihada zinaendelea, lakini kama hutaweza kutibu chanzo, huenda usipate matokeo mazuri. Katika ngazi ya kijiji tunategemea wananchi wawe wa kwanza kutoa taarifa wanapoona shughuli zisizo rafiki kwa mazingira,” anasema.
NEMC yathibitisha kuongezeka kwa magugu maji
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Kaskazini, Benjamin Doto, anakiri kuwa kuongezeka kwa magugu maji kumeathiri mazingira ya Ziwa Jipe.
Anasema magugu hayo yamefunika eneo linalokadiriwa kufikia takribani hekta tano.
Kauli hiyo inaongeza uzito wa haja ya kufanya tathmini ya kina kuhusu ukubwa wa maeneo yaliyoathirika, mabadiliko ya mazingira na hatua zinazohitajika ili kurejesha uhai wa ziwa.
Utafiti wa kisayansi wafichua chanzo cha uharibifu
Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela-Jijini Arusha, Dk Grite Mwaijengo, anasema utafiti alioufanya wakati wa masomo yake ya shahada ya uzamivu ulibaini kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika Ziwa Jipe.
Anasema hali hiyo ilimsukuma kuchunguza sababu za kuongezeka kwa magugu maji na mabadiliko ya kina cha ziwa.
Kwa mujibu wake, matokeo ya utafiti yalionesha kuwa uharibifu wa mazingira katika eneo la bonde linalolisha Ziwa Jipe umechangia kwa kiasi kikubwa changamoto zinazolikabili.
Anataja kilimo na ufugaji usiozingatia kanuni za uhifadhi wa mazingira, ukataji miti, mmomonyoko wa ardhi na shughuli nyingine zisizo rafiki kwa vyanzo vya maji.
“Katika utafiti tulioufanya kwa kuzunguka ziwa lote, upande wa Tanzania na Kenya, tulifanya vipimo vya kina na kugundua kuwa kina hicho hakizidi mita tatu. Sehemu kubwa ya ziwa ina kina cha mita moja hadi mbili,” anasema Dk Mwaijengo.
Anabainisha kuwa jamii nyingi zinazozunguka ziwa hutegemea uvuvi na kilimo kwa ajili ya kipato, huku baadhi ya wananchi wakitumia maji ya ziwa kwa matumizi ya nyumbani.
Hata hivyo, utafiti wake umeonesha kuwa samaki wanaopatikana kwa kila kiwango cha juhudi za uvuvi wamepungua, na wengi wanaovuliwa ni wa ukubwa mdogo.
Samaki wa asili katika hatari ya kutoweka
Moja ya matokeo muhimu ya utafiti huo ni kubainika kwa tishio linalowakabili samaki wa asili wanaopatikana katika Ziwa Jipe, wakiwamo wanaotajwa kwa jina la Jipe Tilapia.
Dk Mwaijengo anasema samaki hao, wanaohusishwa kwa karibu na mfumo wa ikolojia ya ziwa hilo, wanakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na kuzorota kwa mazingira na uvuvi usio endelevu.
Anaeleza kuwa kupungua kwa kina cha maji, kuharibika kwa mazalia na kuongezeka kwa uvuvi wa samaki wadogo kunaweza kuathiri uwezo wa samaki hao kuzaliana na kuendeleza idadi yao.
Katika utafiti huo, wataalamu walichunguza pia mashapo yaliyopo chini ya ziwa na kubaini kuwa yana mchanganyiko wa mchanga na tope linalofanana na mabaki ya vitu vilivyooza.
Kwa nini magugu maji yanaongezeka zaidi upande wa Tanzania?
Dk Mwaijengo anaeleza kuwa tofauti ya kiwango cha magugu maji kati ya maeneo ya Tanzania na Kenya inahusishwa, pamoja na mambo mengine, na mwelekeo wa upepo.
Anasema upepo unapovuma, magugu yanayoelea huweza kusukumwa na kujikusanya katika maeneo ya upande wa Tanzania.
Anafafanua kuwa katika ziwa hilo kuna makundi mawili makuu ya magugu: yale yanayoelea na kusafirishwa na upepo na yale yanayojikita katika maeneo ya pembezoni na chini ya maji.
“Magugu yapo ya aina mbili. Yale unayoyaona katikati ya ziwa, mengi yanatembea, na yale ya pembeni, mengi yamejikita kwenye ardhi,” anasema.
Anaongeza kuwa magugu yanapokufa na kuoza, mabaki yake huchangia kuongeza virutubisho katika mazingira ya ziwa, hali inayoweza kuwezesha kuendelea kwa ukuaji wa magugu mengine.
Kwa mantiki hiyo, kuondoa magugu pekee bila kudhibiti virutubisho na mashapo yanayoingia ziwani kunaweza kusababisha tatizo kujirudia.
Nini kifanyike kulinusuru Ziwa Jipe?
Dk Mwaijengo anapendekeza kuanzishwa kwa programu jumuishi ya kurejesha uhai wa Ziwa Jipe na bonde lake, ikihusisha Serikali za Tanzania na Kenya, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo na jamii zinazolizunguka.
Anasema hatua hizo zinapaswa kujumuisha uhifadhi wa vyanzo vya maji, urejeshaji wa mazingira yaliyoharibika, udhibiti wa mmomonyoko wa ardhi na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile, anapendekeza kuwepo kwa mfumo wa vipindi maalumu vya kupumzisha shughuli za uvuvi ili kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana na kukua.
“Wakati hatua hizo zikitekelezwa, wavuvi wasisitizwe kufuata kanuni bora za uvuvi na utunzaji wa mazalia ya samaki. Pia kuwe na upandaji miti katika maeneo yanayozunguka ziwa na bonde lake, pamoja na kuhimiza kilimo kinachopunguza mmomonyoko wa ardhi,” anasema.
Anashauri pia kuwapo kwa programu za kuwasaidia wananchi wanaotegemea uvuvi pekee kupata shughuli mbadala za kiuchumi.
Hatua hiyo, kwa maelezo yake, inaweza kupunguza shinikizo la uvuvi wa kupita kiasi na kutoa nafasi kwa rasilimali za ziwa kujirejesha.
Magugu maji yanaweza kuwa fursa ya kiuchumi
Licha ya madhara yake, Dk Mwaijengo anasema magugu maji yanaweza pia kutumiwa kama malighafi kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi endapo kutakuwa na teknolojia na usimamizi unaofaa.
Anataja matumizi yanayoweza kuchunguzwa kuwa ni pamoja na utengenezaji wa mbolea, kilimo cha uyoga, vifaa vya kuezekea na bidhaa nyingine zinazoweza kuwapatia wananchi kipato.
“Kuna wazo la kutumia magugu kutengeneza mbolea, kilimo cha uyoga, kuezeka na vitu vingine vingi ambavyo vinaweza kusaidia kupunguza magugu ziwani na wakati huo huo kuwapatia wananchi kipato,” anasema.
Hata hivyo, anaonya kuwa siyo kila aina ya magugu inapaswa kuondolewa kwa sababu baadhi yake yana mchango muhimu katika mfumo wa ikolojia ya ziwa, ikiwamo kulinda mazalia ya samaki na viumbe wengine wa majini.
Kwa hiyo, anasisitiza umuhimu wa kufanya tafiti ili kutofautisha mimea inayochangia kuharibika kwa mazingira na ile yenye manufaa kwa mfumo wa ikolojia.
Fedha za utafiti zahitajika
Dk Mwaijengo anasisitiza kuwa juhudi za kulinusuru Ziwa Jipe zinahitaji kuungwa mkono na fedha za kutosha kwa ajili ya tafiti za kisayansi na ufuatiliaji wa mabadiliko ya mazingira.
Anasema tafiti endelevu zitasaidia kupata taarifa za uhakika kuhusu kina cha maji, kiwango cha mashapo, mabadiliko ya eneo la ziwa, hali ya viumbe hai na athari za shughuli za kibinadamu.
Taarifa hizo, kwa mujibu wake, ni muhimu katika kuandaa mipango ya uhifadhi yenye malengo yanayopimika na kuimarisha usimamizi wa rasilimali ya maji inayoshirikishwa na nchi mbili.
Ziwa la nchi mbili, wajibu wa pamoja
Kwa miaka mingi, Ziwa Jipe limekuwa tegemeo la maisha ya wananchi, chanzo cha shughuli za kiuchumi na sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia unaounganisha Tanzania na Kenya.
Lakini sasa, simulizi za wavuvi wanaopoteza kipato, kupungua kwa samaki, magugu maji yanayoziba njia za uvuvi na matokeo ya tafiti za kisayansi vinaonesha ukubwa wa changamoto inayolikabili.
Pamoja na juhudi zinazotajwa na mamlaka mbalimbali, bado kuna haja ya kuweka wazi mpango jumuishi wa kulinusuru ziwa hilo, ukionesha taasisi zinazowajibika, fedha zinazohitajika, hatua za utekelezaji na muda wa kufikia malengo.
Swali linalobaki ni iwapo Serikali za Tanzania na Kenya, kwa kushirikiana na wadau wa mazingira na wananchi, zitaweza kuchukua hatua madhubuti kabla uharibifu haujafikia kiwango ambacho kitakuwa kigumu zaidi kurekebishwa.

Kwa wananchi wa Jipe, Butu, Ruru na Kambi ya Simba, kulinusuru Ziwa Jipe si suala la mazingira pekee. Ni kulinda maisha yao, uchumi wao na urithi wa vizazi vijavyo.