Fundi...
Nimependa sana hii kuwa mimi siyo ''authority,'' historia ya uhuru wa Tanganyika bali ni ''authority,'' wa akina Sykes.
Umenikosha sana hapa.
Ulikuwa unajua mchango wa akina Sykes katika kupigania uhuru wa Tanganyika kabla mimi sijawaandika?
Historia ya TANU ya Kivukoni ilikuwepo toka 1981 na iliwafuta akina Sykes na wapigania uhuru wengi mbona hukusema kitu ulikuwa kimya?
Unajua kuwa umuhimu wa akina Sykes katika historia ya uhuru wa Tanganyika ni kuwa ni wao katika wale waasisi wa African Association ndiyo walioandika historia ya AA na kuacha nyaraka ambazo ndizo hizi nimezitumia kuandika historia yao na historia ya kuamka kwa Waafrika kudai haki zao katika nchi yao.
Huyu ni baba yao Kleist Sykes mwaka wa 1929.
Sasa njoo kwa watoto Abdul na Ally hawa wanaanza harakati 1942 wakiwa Burma.
Nimetumia nyaraka za Sykes kuandika historia ya TANU na historia ya Julius Nyerere.
Kuna yeyote mwenye ushahidi wa picha na nyaraka wa historia ya Nyerere katika TAA kuanzia alipokutana na Abdul Sykes 1952 na kutiwa katika uongozi wa juu 1953?
Umepata kuona au kusoma popote pale historia ya Nyerere kama nilivyoieleza katika kitabu cha Abdul Sykes?
Sikujua kama kurudisha historia ya zaidi ya miaka 50 iliyofutwa ni udini.
Vipi wale walioifuta historia hii na kuweka ya kwao nini kiliwasukuma kufanya hivyo?
Haikuwa uoga wa kuona kuwa Waislam watakuwa kila mahali katika historia ya TANU na kudai uhuru wa Tanganyika?
Kaa kitako jitulize na fikiri iweje Nyerere afikie mahali asahau hata kama alimkuta Abdul Sykes Secretary na Act. President wa TAA pale alipompokea Dar es Salaam 1952?
Asahau pia aligombea na yeye nafasi ya urais wa TAA.
Inawezekana vipi Nyerere atoe medali 3, 979 wakati anaacha uongozi na Abdul na Dossa hawamo katika orodha ile?
Unajua nini alisema alipoulizwa na watu wake wa karibu kuhusu hili?
Mimi nimewarejesha katika historia Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Sulemaiman Takadir, Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Mohamed Yusuf Badi, Halima Selengia, Tatu bint Mzee. Mama bint Maalim, Amina Kinabo, Nyange bint Chande, Zarula bint Abdulrahman kwa kukutajia wachache katika wanawake waliopigania uhuru wa Tanganyika.
Si akina Sykes peke yao.
Naijua historia kubwa ya Tanganyika kutoka kila pembe.
Sikuwapiga Mama Mkello na Mohamed Mkwawa picha sebuleni kwangu.
Picha hizo nimezipiga majumbani kwao Tanga nikiwa na Ann Lee.
Mimi haya mambo kaka nayajua na si kwa kuwa mimi nina akili kuwapita watu wengine.
Hii historia imekuwapo nyumbani kwetu mimi mdogo wala sikuwa najua nashuhudia jambo kubwa katika historia ya Tanganyika na Zanzibar.
Hivi hujajiuliza kwa nini akina Sykes walinifungulia mimi ile hazina ya nyaraka zao na si mtu yeyote yule.
Hivi unajua baada ya historia ya kweli kuwa hadhir kila mtafiti akienda kuwahoji akina Sykes na kutaka kuona nyaraka zao jibu lao ni, ''Mohamed Said keshaandika someni kitabu chake.''
Unajua kwa nini wanasema maneno haya?
Leo tunaisoma upya historia ya Nyerere na historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hivi hujajiuliza kwa nini Dr. Ghassany alinichukua mimi kama msaidizi wake katika utafiti wa kitabu chake na si mtu mwingine yeyote yule?
Jiuilize maswali haya yote na jaribu kupata majibu.
Hivi unajua kuwa ni Abdul Sykes na Dossa Aziz ndiyo waliompeleka Nyerere Zanzibar kumjulisha kwa Karume?
Baba yangu alikuwa rafiki mkubwa wa Abdulaziz Twala na Jaha Ubwa wote hawa ASP na wanamapinduzi na waliuliwa baada ya mapinduzi.
Inawezekana kweli mimi si ''authority,'' lakini wengi wakitaka kujua mambo wanakuja kwangu hata jopo la Prof. Shivji walioandika Biography of Julius Nyerere walikuja kunihoji na nikawapa picha na baadhi ya Nyaraka za Sykes.
Hii ndiyo nafasi yangu katika historia ya Tanganyika na Zanzibar.
View attachment 2058609
Kulia Prof. Issa Shivji, Prof. Saida Yahya Othman na Dr. Ng'wazi Kamatha wakinihoji nyumbani kwangu kuhusu Julius Nyerere wakati wanatafiti maisha yake kwa ajili ya kitabu chake.