Makala...
Nakupa historia ya babu yangu kwa ufupi.
Ndani ya gazeti la Raia Mwema (Januari 3-9, 2018) kulikuwa na makala ya maisha ya Mzee Fredrick Mchauru.
Kama kawaida yangu kupenda kusoma maisha ya Watanzania maarufu niliitupia jicho.
Haikunipitikia kabisa kama Mzee Mchauru niliyemtaja katika kitabu changu cha historia ya uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1998 bado atakuwa hai.
Jina hili likawa linajirudia akilini kwangu. Naam Mzee Mchauru yu hai akiwa sasa na umri wa miaka 97.
Huyu Mchauru ndiye yule aliyekabiliana na babu yangu Salum Abdallah katika uwanja wa mpira wa Town School Tabora chini ya miembe wakati wa kupambana na wakoloni, babu yangu akisimama na wananchi wa Tanganyika wakati Mchauru akiwa mtumishi wa serikali ya Waingereza?
Naam ndiye yeye.
Makala ile ilikuwa tamu haikuisha imekuja kuhitimishwa na toleo la juma hili la Raia Mwema (10 – 16 Januari 2018).
Katika toleo hili mwandishi Ezekiel Kamwaga kanitaja kwa jina kuwa nimemwandika Mzee Mchauru katika historia ya uhuru wa Tanganyika.
Kamwaga akaeleza kuwa nimepata kusema kuwa Mzee Mchauru alipata shida kuelewana na wale waliokuwa wanapigania uhuru wa Tanganyika.
Dhulma ilikuwa imezidi sana na wafanyakazi wa bandarini Dar es Salaam wakiongozwa kwa siri na Abdul Sykes wakati ile kijana mdogo wa miaka 23 waliamua kufanya mgomo kudai haki zao.
Mgomo wa Makuli kama ulivyokujafahamika ulienea Tanganyika nzima.
Lakini ili kuuelewa mgomo huu ni muhimu sana msomaji akasoma historia nzima ya mgomo huu chanzo chake na vipi wananchi waliweza kujiunga pamoja hadi kufikia kuwa na uwezo wa kuitingisha serikali kwa mgomo kuenea Tanganyika nzima.
Haiwezekani kwa hapa kueleza historia yenyewe nitakachofanya kukunyambulieni ilikuwaje hadi babu yangu akapambana uso kwa macho na Fredrick Mchauru katika mgomo wa wafanyakazi wa mwaka wa 1947.
Tabora, Western Province 11 Septemba, 1947
‘’…mgomo huo ulioenea kama moto wa makumbi ulikumba nchi nzima kwa kasi ya ajabu.
Ilikuwa kama vile wafanyakazi wa nchi nzima wametaarifiana.
Wafanyakazi wa Tanganyika Railways huko Tabora wakiongozwa na Salum Abdallah waliingia kwenye mgomo tarehe 11 Septemba.
Chama cha African Association mjini Tabora kilimteua Mwalimu Pinda, aliyekuwa akifundisha shule ya St Mary, kuwa 'mshauri' wa wafanyakazi waliogoma.
Asubuhi ya siku ya mgomo wafanyakazi wa Tanganyika Railways walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira chaTown School, wakakaa chini ya miembe kujikinga jua.
Tabora ni maarufu kwa miti hiyo.
Tangu siku hiyo kiwanja hiki kikawa ndicho uwanja maalum kwa mikutano yote ya siasa.
Serikali ilimtuma kijana mmoja kutoka Masasi aliyesoma katika shule za misheni, Frederick Mchauru kuwahutubia wafanyakazi na kuwaomba wasimamishe mgomo na warudi kazini.
Mchauru alikuwa Mmakonde kutoka Newala.
Alielimishwa St. Joseph's College, Chidya na St. Andrewís College, Minaki.
Mwaka 1946, Mchauru alikuwa amerudi kutoka LondonUniversity akiwa amehitimu masomo yake na kuanza kazi mjini Tabora kama Assistant Social Development Officer.
Wafanyakazi waliokuwa kwenye mgomo walimpigia kelele wakimtaka anyamaze huku wakimwita msaliti.
Inashangaza namna shule za misheni zilivyowatengeneza watumishi wa serikalini walio wasomi wawe watiifu na waaminifu kwa dola.
Wasomi hawa mara nyingi walijikuta wanasigana na wale waliokuwa wakipinga ukoloni na udhalimu.
Mchauru alishindwa kutambua hali halisi iliyokuwapo pale siku ile.
Mchauru alipuuza zile kelele akaendelea kuzungumza akijaribu kuwasihi wafanyakazi warudi kazini kwao.
Ghafla hali iligeuka.
Watu walipandwa na hasira na kusikia wakisema ashikishwe adabu.
Watu waliokuwa wamehamaki wakaanza kumsogelea.
Salum Abdallah, akiwa kiongozi wa watu wale, alihisi kuwa endapo hatachukua hatua ya kumnusuru Mchauru huenda watu wakamuadhibu.
Alienda pale aliposimama Mchauru.
Aliinua mikono yake juu akawataka watu watulie.
Salum Abdallah alikuwa mtu wa miraba minne na alikuwa na sauti kubwa.
Wanachama wengi wa TRAU wanamkumbuka kwa sauti yake, hasira zake na kwa umbo lake kubwa.
Salum Abdallah alikuja kuunda chama cha TRAU mwaka wa 1955 akiwa Rais muasisi na Kassanga Tumbo Katibu muasisi wakaiegemeza TRAU kwa TANU kupigania uhuru wa Tanganyika.
Wafanyakazi walipomuona Salum Abdallah walitulia na Mchauru akaondoka pale kimya kimya kupeleka taarifa kwa hao waliomtuma kuwa watu wamegoma, hawasikii la muadhini wala la mnadi sala…’’
(Rafiki zangu kwa muda mrefu wanatia shinikizo niandike kitabu cha historia ya babu yangu).
View attachment 2062111
Viongozi wa TRAU Salum Abdallah ni huyo kwenye mshale na anefuatia ni Kassanga Tumbo