Hakuna mahala umembana, hebu taja hata sehemu tano ambazo umembana na kama unavyojiaminisha zinaashiria haijui historia, wewe bwana mdogo shida yako nyingine nadhani ni "ulipyoto" kwasababu nukta zako zinajificha sana kisha zinakuwa na Uongo ama kukosa umakini, lakini pia hebu jikiteni katika hoja moja moja na ikitamatika ndio iende nyingine, huu mtindo wa kuzungumza kwa ujumla kwamba tumembana, hajui historia, hawataji wasukuma n. k kisha akiwabainisha mnarukia hoja nyingine si mzuri nadhani hata nafsi zenu zawasuta
Makala...
Historia ina kawaida ya kujirudia.
Baada ya Kura Tatu na TANU kuingia LEGCO pakawa na mabadiliko makubwa sana katika siasa za TANU.
Huu mwaka wa 1958 baada ya Kura Tatu ndipo Sheikh Suleiman Takadir alipogombana na Nyerere.
Kisa kizito sana.
Wakati wa utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes hakuna aliyependa tumzungumze Sheikh Suleiman Takadir.
Ilikuwa Sheikh Haidar Mwinyimvu yeye alikubali na akanipa kisa chote.
Kipo kwa ukamilifu wake katika kitabu cha Abdul Sykes.
TANU ilipoanza ilikuwa inaanza mikutano yake kwa dua iwe New Street ofisini au Mnazi Mmoja.
Taratibu miaka ilipokuwa inasonga mbele mambo yakabadilika ikawa mikutano inaanza na kauli mbiu, ''Uhuru na Kazi.''
Uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961 pakawa na maneno kuwa Abdul Sykes hakuwa na chama cha siasa na TAA kilikuwa chama cha starehe.
Hii ilikuwa kebehi na kejeli.
Ndiyo hizi zinajirudia hapa.
Leo tunasikia kebehi akikebehiwa Abdul Sykes yuko kaburini.
Wanauliza wapi alihutubia mkutano.
Hawajui kuwa ziko shajara (diary) za Abdul Sykes zina hotuba za Nyerere za mwanzo Mnazi Mmoja.
Abdul Sykes akiyasikia haya maneno kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe lakini alibakia kimya hakusema kitu.
Daisy Sykes katika kumbukumbu ya miaka 50 ya kifo cha baba yake aliandika makala iliyochapwa na Raia Mwema.
Kaeleza haya na msimamo wa baba yake ya kustahamili na kuwa kimya.
Haya maneno yakiwachoma sana rafiki zake.
Yakiwachoma kwa sababu walikuwa wanajua nini Abdul kafanya.
Ahmed Rashad Ali akamwambia Abdul Sykes kuwa ikiwa yeye atafungua kinywa chake kueleza historia ya TANU hakuna atakaethubutu kumkabili kupingananae.
Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti Idd Tulio lkavunjwa mwaka wa 1963 na ikawa sasa zile kanzu zilizozoeleka kuonekana ofisi ya TANU Lumumba zikawa zimetoweka.
Na zimetoweka hadi leo.
Abdul Sykes alikataa kusema chochote akawa kimya hadi umauti ulipomfika mwaka wa 1968.
Nimeweka hapa kisa cha ile fadhaa iliyotokea nyumbani kwa Abdul Sykes pale ilipohofiwa kuwa Nyerere kalishwa sumu anataka kuuliwa.
Nimekiweka kisa hiki baada ya kusoma kuwa mikutano ya TANU haikuwa ikifanyika nyumbani kwake wanasema mikutano inawezekana ikifanyika kwa Amir Jamal.
Pamekuwa na ukimya.
Kejeli, kebehi na matusi hayajibiwi bali yananyamaziwa.
Huu ndiyo uungwana tuliofunzwa na walimu wetu.
Sasa hata Abdul Sykes alipofutwa katika historia ya TANU kwa mtu kama Ahmed Rashad Ali haikuwa ajabu, ''He had seen it coming.''
Hizi kebehi ni kwa kuwa wameghadhibika kuwa wao walishamfuta Abdul Sykes na wenzake wote aliokuwanao mimi nimemrudisha.
Kitabu cha maisha yake kipo na sasa yale aliyofanya yanafahamika na nchi imemtunuku Medali ya Mwenge wa Uhuru.
Ngoja nihitimishe kwa kipande hiki.
Siku moja asubuhi nimepokea simu kutoka kwa Bi. Zainab katibu wa Ally Sykes, ''Mohamed mzee anataka kuzungumza na wewe.''
Siku zile Bwana Ally mgonjwa lakini mkaidi lazima aje ofisini.
Baada ya salamu akaniambia, ''Mohamed mimi na Bwana Abdul In Shaa Allah tutapewa nishani Ikulu kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.''
Watu wa Ikulu wamefika hapa ofisini wamenipa taarifa na wameniuliza, ''Kwani Bwana Ally wewe na kaka yako mmefanya nini kustahili hii heshima?''
Sote tukawa tunacheka katika simu.
Bwana Ally alihitimisha mazungumzo yetu kwa kuniambia kuwa aliwapa kitabu cha Abdul Sykes akawaambia, ''Someni hiki kitabu yote yameelezwa humo.''
Ally Kleist Sykes na Julius Kambarage Nyerere nyumbani kwa Nyerere Magomeni 1958