Mkazi wa Mtaa wa Kyamaizi, Kata ya Kahororo Manispaa ya Bukoba, Abdul Suleiman (30), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Bukoba akikabiliwa na kesi mbili za kuwabaka na kuwalawiti wanafunzi watano wa shule za msingi.
Kesi hizo zenye jumla ya mashtaka saba, zimesomwa jana Jumatano Agosti 14, 2024 mbele ya mahakimu wawili tofauti mahakamani hapo.
Kesi ya kwanza namba 22889/2024 imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Frola Kaijage na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Everester Kimaro.
Akimsomea mashtaka, Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili na Julai, 2024, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka tisa.
Mshtakiwa alikana tuhuma hizo, kesi imeahirishwa hadi Agosti 28, 2024 itakapoanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.