Absalom Kibanda: Namuogopa Abdurahman Kinana

Absalom Kibanda: Namuogopa Abdurahman Kinana

WOWOWO

JF-Expert Member
Joined
Aug 3, 2011
Posts
599
Reaction score
456
Great Thinkers,
Baada ya kuisoma makala hii ya Absalom Kibanda Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, nimejikuta napata mashaka sana na zaidi kupoteza imani na uzalendo wake. Pia nimejikuta nikiamini maneno niliyokuwa nikiyapata kijiweni kwamba Kibanda ni mmoja wa beneficieries wa Ufisadi kutoka tasnia ya Habari nchini.

NAMUOGOPA ABDURAHMAN KINANA

Na Absalom Kibanda

Kwa mara nyingine tena, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeandika historia mpya baada ya kufanya mabadiliko mazito katika safu yake ya uongozi wa kitaifa.

Ni mabadiliko mazito si kwa sababu tu yamefanywa na CCM ambayo imekuwa na rekodi ya kubadili sura za watendaji wake kwa namna na kwa njia tofauti, bali kutokana na ukweli kwamba safari hii mabadiliko hayo yamehusisha watu wazito, wenye historia ya kipekee katika medani ya uongozi ndani na nje ya chama hicho.

Ingawa kwa mtazamo wa haraka haraka, mabadiliko hayo yanaweza yakaonekana kuwa ni ya kuyabeza au kuyapuuza kama ilivyotamkwa na baadhi ya wadadisi wa mambo wakiwamo wachambuzi wa masuala ya siasa na hata wanazuoni, ukweli unabaki pale pale kwamba kile kilichofanywa na CCM kinaweka alama ya kipekee katika mwenendo wa siasa za kitaifa za siku zijazo.

Wasifu mzito na historia za kutukuka za baadhi ya wateule wanaounda timu ‘mpya' ya viongozi watendaji wa CCM kwa kiwango kikubwa ndicho kitu kikubwa pekee kinachosababisha mtu yeyote makini ajikute akipata shida kuyabeza yale yaliyofanywa na chama hicho tawala mwishoni mwa wiki kule Dodoma.

Msuko mpya wa safu ya wakuu wa idara za CCM uliotangazwa na Rais Jakaya Kikwete ukiwajumuisha wanasiasa wasiojua mizaha wawapo kazini kama alivyo Philip Mangula, au makada wa muda mrefu wa chama hicho wa kariba ya Muhammad Seif Khatib na Zakia Meghji una kila sababu ya kutafutiwa dawa mahususi na makamanda wa kambi ya upinzani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana kuing'oa CCM madarakani.

Ni mtu asiyejali au mpuuzi asiyezijua vyema siasa za Tanzania anayeweza akasimama na kuudharau uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete ambaye baada ya kushindwa mara kadhaa hatimaye amefanikiwa kumshawishi, mmoja wa wanasiasa makini na wakongwe, mtumishi wa umma wa muda mrefu, mwanadiplomasia na Kanali Mstaafu wa Jeshi, Abdulrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Kwa muktadha wa makala ya leo na kwa kuzingatia nafasi kuu ya utendaji aliyopewa, nitazungumzia kwa sehemu tu wasifu wa Kinana, mtu ambaye naamini anapaswa kuangaliwa kwa jicho la karibu na wakati mwingine kudhibitiwa ili kasi yake ya kukijenga chama alichopewa dhamana ya kukinusuru isije ikasababisha kuyumba kama si mauti ya kisiasa kwa baadhi ya vyama vya upinzani.

Ni wazi kwamba, kuteuliwa kwa Kinana kuwa Mtendaji Mkuu wa CCM Taifa, akirithi mikoba iliyomshinda, Wilson Mukama, kumetutia ganzi baadhi yetu ambao kwa muda mrefu tumekuwa ‘mashabiki' au waumini wa kuchagiza kwa njia ya kalamu na wakati mwingine katika mijadala ya wazi kwamba, taifa lilikuwa na haja ya kutafuta mabadiliko ya uongozi kutoka nje ya chama tawala.

Sitaki kuwa miongoni mwa wapenda mabadiliko ambao kwa njia za kujifariji au za kujipa matumaini hewa wameingia katika mkumbo wa jumla jumla wa kumbeza Kinana kwa namna wanayotaka kuuaminisha umma wa Watanzania kwamba, mtu huyo anaweza akasukumwa kirahisi kwa namna ile ile ilivyopata kuwa kwa watangulizi wake kadhaa waliopata kushika wadhifa huo.

Hupaswi kuwa na akili nyingi kutambua kwamba, umahututi wa CCM kisiasa, kulikokifikisha chama hicho tawala kufikia hatua ya kupoteza dira na kuanza kuliona kaburi la kupoteza madaraka ya dola ndiko kulikorejesha hekima za usikivu kichwani mwa Kikwete hata akalazimika kuwarejesha akina Kinana, Mangula, Seif Khatib na Meghji katika kilinge cha siasa za ushindani mkali ndani na nje ya CCM.

Siyo siri hata kidogo kwamba, hekima hii mpya ya Kikwete ya kumrejesha Kinana ulingoni, ambaye siku chache tu zilizopita alitangaza kustaafu siasa huku akisema alikuwa akikusudia kuwaachia vijana kusukuma gurudumu la uongozi, inahusisha kichwa zaidi ya kimoja kutoka ndani na nje ya CCM.

Kama ilivyo kwa wengi wengine nilianza kulisikia jina la Kinana likihusishwa na ukatibu mkuu wa CCM miaka miwili au mitatu iliyopita hali ambayo ilipata kusababisha nifikie uamuzi hata wa kumuuliza yeye mwenyewe kuhusu taarifa hizo.

Jibu ambalo Kinana mwenyewe alipata kunipa kwamba alikuwa akipenda kuona akiendelea kupata fursa ya kukitumikia chama chake kama mshauri na kwa nyakati mahususi kama zile za kampeni na si kwa nafasi ya ukatibu mkuu lilikuwa likinipa sana faraja.

Kilichokuwa kikinipa faraja si kingine chochote bali fikra zangu (sahihi au potofu) ambazo siku zote zilikuwa zikinifanya niamini kwamba, ukatibu mkuu kwa Kinana ilikuwa ni silaha moja ya maangamizi kwa vyama vya upinzani ambavyo naamini vinapaswa kuendelea kupewa fursa ya kuaminiwa na kukomaa.

Katika mazingira ambayo CCM imeweza kuepuka zahama ya kumeguka vipande viwili kwa kuzingatia maono aliyokuwa nayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwangu mimi Kinana wa zama hizo alikuwa na anaendelea kubakia kuwa tishio kubwa kwa ustawi wa upinzani ambao ni rutuba muhimu kwa maendeleo ya demokrasia na misingi ya utawala bora.

Hili ndilo ambalo naamini wapinzani wanapaswa kulitazama na kulitafakari nyakati hizi wanapoendesha harakati zao za kukabiliana na maguvu ya dola na haya mapya ya hoja ambazo aghalab zitaongozwa na Kinana nyakati hizi taifa linapojiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa miaka mitatu ijayo.

Haitoshi kwa kina Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Dk. Willibrod Slaa na Zitto Kabwe kumbeza Kinana na timu ya watendaji wake eti kwa hoja nyepesi na zisizo na mashiko za ufisadi au uchafu wa jumla jumla wa CCM.

Wapinzani na wachambuzi wa mambo wanapaswa kujua na kutambua kwamba, Kinana ni mwanasiasa wa vitendo, msomaji mzuri wa vitabu, ripoti, taarifa, magazeti, msikilizaji na msikivu mzuri wa mambo mepesi na mazito kuliko alivyokuwa ‘utopia' Mukama anayeamini na kuzitetea nadharia zisizotekelezeka.


Si hilo tu, wapinzani wanapaswa kutambua kwamba, historia yake ya uaskari alioutumikia miaka 20 hadi mwaka 1972 akifikia cheo halisi cha jeshi cha Kanali ikimhusisha na mafunzo mahususi ya kimkakati ni sehemu ya mambo ambayo yanatawala nidhamu ya kazi ya aina ya kipekee iliyomfanya Kinana akawa jemedari wa mapambano ya CCM tangu mwaka 1995 hadi leo.

Wachambuzi wa mambo, nikiwamo mimi mwenyewe ambao siku zote tumekuwa tukiiona CCM kuwa chama kinachokufa kwa maana ya kuchungulia kaburi, tunapaswa kuanza kutafakari upya mawazo yetu hayo, nyakati hizi Kinana alipopewa dhamana ya kuwa mtendaji wake mkuu.

Tutakuwa wendawazimu iwapo tutamlinganisha Kinana na Mukama na kusahau kwamba huyu aliye kilingeni leo ndiye aliyemuongoza Benjamin Mkapa katika mapambano makali ya kisiasa mwaka 1995, zama Augustine Mrema alipokuwa tishio la kwanza la kweli dhidi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu.

Alikuwa ni Kinana aliyefanya kazi kubwa katika kipindi chote cha kampeni akiratibu na kuongoza kampeni zote za Mkapa zilizomjumuisha pia Mwalimu Nyerere katika mazingira ambayo wengi walikuwa wakiamini CCM ilikuwa katika mwelekeo wa anguko la kihistoria.

Kinana ambaye kabla ya mwaka 1995 alikuwa tayari amepata kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ulinzi alitumia vyema mbinu za medani na zile za kidemokrasia na kiplomasia kumjengea uhalali Mkapa ambaye wakati huo alikuwa mwanasiasa ambaye hakuwa akijulikana sana.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, siku chache tu baada ya kuingia Ikulu kwa mara ya kwanza mwaka 1995, kwa sababu ama ya ulevi wa madaraka au kwa kutingwa na kazi za kimamlaka, Mkapa alisahau kazi kubwa aliyofanyiwa na Kinana.

Ni katika kipindi hicho cha kati ya mwaka 1995 na 2000 ndipo nilipokutana kwa mara ya kwanza na mara kadhaa na Kinana nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam nikiwa nimeongozana na mhariri wangu, Muhingo Rweyemamu, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambako nilipata fursa ya kumsikiliza na kuufahamu upeo mkubwa wa kuona mambo aliokuwa nao mwanasiasa huyo.

Tangu wakati huo hadi wakati wa kampeni za mwisho za mwaka 2010, niliendelea kukutana kwa nyakati fupi fupi na Kinana na mara kadhaa nikawa mtu wa kufuatilia na kuzisikiliza kwa makini, habari zake kutoka ama kwa marafiki au maadui zake wa kisiasa.

Sikushangazwa hata kidogo niliposikia tena kwamba, Mkapa alilazimika kumuangukia tena Kinana na kumuomba aongoze tena kampeni zake mwaka 2000 kabla ya Kikwete naye hajafanya kile alichofanya mtangulizi wake alipomuomba mwanasiasa huyo adhibiti joto la kiti cha urais mwaka 2010.

Uwezo wake mkubwa wa kisiasa, umakini wake na upeo mkubwa alionao katika kuona na kuchambua masuala ya siasa, uchumi na jamii ndivyo vitu ambavyo kwanza kwa nyakati tofauti vimepata kumfanya Kinana awe Mbunge wa Jimbo la Arusha kwa miaka 10, Mbunge wa Afrika Mashariki na Spika wa Bunge hilo.

Si ajabu hata kidogo kwamba, hata kabla ya kufikia huko, ni Kinana huyo huyo ambaye alipata kuwa Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Rais wa Tanzania katika eneo la Maziwa Makuu na kabla ya hapo akiwa Mwenyekiti wa Mawaziri wa Ulinzi wa Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC) zama akiwa Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Awamu ya Pili iliyokuwa ikiongozwa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Uzoefu wake katika siasa za kiraia unaanzia mwaka 1972 wakati alipostaafu jeshi akiwa Kanali baada ya kulitumikia kwa miaka 20 ndiyo ambao amekuwa akiutumia kama silaha kubwa ya kukijua chama chake na pengine kumfanya awe mmoja kati ya watu wachache ambao wamepata kuwafanyia kazi marais wote wane wa Tanzania.

Anarithi mikoba ya Mukama akiwa mmoja wa wanasiasa wachache wa CCM wa rika ile ile la kina Kikwete ambaye alilikimbia na kulikana kundi la mtandao mwaka 2005 ambalo baadhi yetu tunaamini kuwa, ndilo lilisababisha kuzaliwa kwa siasa mpya za kupakana matope, kuzushiana na kuhujumiana ndani na nje ya CCM.

Lakini pengine kubwa katika yote hayo anaingia madarakani huku akiwa na hazina ya uzoefu mkubwa wa kuongoza mapambano dhidi ya vyama vya upinzani na kushinda katika mazingira ambayo aghalab yamekuwa yakiacha vidonda visivyopona kwa wapinzani tangu mwaka 1995. Huyu si mtu wa kumpuuza au kumbeza hata kidogo.
My Take:
-Hapo kwenye RED naona Kibanda kajikita katika kueleza kifo tarajiwa cha upinzani kwa kumezwa na rekodi ya kinana tu bila hata kuzingatia nyakati zilizopo za kisiasa, kupwaya kwa ushindi wa JK kwneye matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na zaidi mchoko wa kimaisha walionao watanzania sasa. Kibanda amejaza mahaba binafsi kwa Kinana pasipo kuzingatia muktadha wa kisiasa uliopo nchini.

Lakini pia Kibanda amejikita katika kusisitiza hatari ya upinzani kufa kutokana na Kinana kuwa GS wa CCM bila kueleza ni kwa vipi anaweza kupambana na hoja zinazotoka kambi ya upinzani hasa CDM au ni Uluteni wake tu Jeshini ndiyo utamfanya aue upinzani.

Aidha, Kibanda anatumia Umeneja Kampeni wa Kinana kwa wagombea wa urais wa CCM bila hata kusumbua kichwa chake,kwamba kuwa meneja haina maana unakuwa incharge wa ushindi wa mgombea bali timu nzima ya kampeni ya Chama ndiyo hufanya kazi hiyo. Mathalan, utamsifu vipi Kinana kwa ushindi wa Mkapa mwaka 1995 wakati Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kivuri chake kilikuwa bado kinaishi ndani ya mioyo ya watanzania? Ni kweli hili si la kubeza lakini si la kumpa credit kubwa kiasi anachotoa Kibanda

-Kwenye Blue, Kibanda kawa kipofu kiasi kwamba kwakwe yeye tuhuma za ufisadi zinazomkabili Kinana na baadhi ya wana safu wa Sekretarieti mpya ya CCM anaziona nyepesi na zisizo na mashiko. Kwake yeye (Ufisadi ni mwepesi na si hoja kwa sasa) bali hoja ni Kinana na rekodi yake tu tena ya huko nyuma.

Tujadili kwa pamoja hii makala.

PIA, SOMA:

-
Absalom Kibanda (Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri) avamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa
 
Muogope sana. Juzi tu katuhumiwa kusafirisha meno ya tembo kupitia kampuni yake yani ukicheza anaweza akakusafirisha na ww.
 
Ama kweli Tanzania bado tuna safari ndefu sana kufikia Ukombozi! Yaani Mwandishi wa Habari anathubutu kuandika Makala ya kuita "hoja ya Ufisadi" kuwa ni "Hoja Dhaifu"!!! Kama mpaka Tasnia ya Habari imeshafisadiwa ki-fikra kiasi hiki, tutawezaje kuutokomeza huo Ufisadi??? Tafakari!!!
 
Ama kweli CCM mtahangaika sana kufufua maiti, yaani mnapamba visivyopambika

Kibanda ameonesha sura yake halisi lakini pia napata shaka sana na uwezo wake wa uchambuzi wa mambo maana makala imekosa vitu vingi vya kumfanya afikishe hitimisho lake.
 
Kibanda ni miongoni mwa wahariri wachache ambao mimi binafsi nilishapoteza imani na makala zao, tangu pale alipoanza kumvurumishia makombora Samuel Sitta na kumsafisha Lowasa.

Kwamba kwake yeye ufisadi wa Samwel Sitta wa kununua madawa ya shilingi milioni mbili na kujenga ofisi ya spika ya sh.500 milioni jimboni kwake urambo ni zaidi ya ufisadi ambao umekuwa ukifanywa na Lowasa miaka nenda rudi na ambao kimsingi umeliingiza taifa hili katika matatizo makubwa sana ya kiuchumi na kusababisha umasikini mkubwa kwa watanzania.

Hapa tulipofika si mahali pa kuwahofia wanaccm na hasa huyo kinana, kinachomsumbua kibanda ni kuwa anaishi katika mwavuli wa historia ya kinana. Anasahau haraka kiasi kwamba ni kinana huyu huyu aliyekuwa kampeni manager wa kikwete na tukashuhudia mporomoko wa kura za kikwete kwa kiasi cha 20%, kama uwezo na mikakati ya kinana ni ya hali ya juu kwanini mwaka 2010 ameshindwa kumpa mgombea wao ushindi wa kishindo kama alivyofanya 2005 na kwa mkapa 1995 na 2000?

Kwa hali ya ccm ya sasa hawana namna yoyote ya kujinasua na anguko , hata kama watamteua nani kuwaongoza kwakuwa walipokifikisha chama chao ni beyond repair na ni muhimu kuzingatia kuwa watanzania hawa wamekuwa wakijitambua taratibu na kutodanganyika kirahsi kama ambavyo kibanda anadhani.
 
Sasa nimeanza kupata picha halisi kuwa jamaa kanunuliwa sio na mafisadi ila na fisadi PAPA lowasa
 
Kibanda ameonesha sura yake halisi lakini pia napata shaka sana na uwezo wake wa uchambuzi wa mambo maana makala imekosa vitu vingi vya kumfanya afikishe hitimisho lake.

Nadhani wengi hamumjui Kibanda, mimi hiyo Makala niliona online nilipoanza kuisoma wala sikupoteza muda wangu kuendelea kuisoma maana ni ushuzi mtupu.

Ni kweli Kibanda anamuogopa Kinana kwa sababu Kibanda ni kibaraka wa Lowasa na uwepo wa Kinana kama katibu Mkuu wa CCM si habari njema kwa kina Kibanda & co, huyu ni mtu wa ovyo sana.

Namshangaa sana Freeman Mbowe kuendelea kumvumilia Mhariri mpumbavu wa namna na kusababi Gazeti la Tanzania Daima kushuka mvuto na kupitwa na Gazeti la Mwananchi wakati mwanzo Tanzania Daima ndio lilikuwa linaongoza. Kama kuna mtu ambaye yupo karibu na Mbowe na anapenda Tanzania Daima lifanye vizuri basi huyu Kibanda afutwe kazi mara moja na nafasi yake apewe Ansbert Ngurumo.
 
Baada ya kuisoma makala hii ya Absalom Kibanda Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, nimejikuta napata mashaka sana na zaidi kupoteza imani na uzalendo wake. Pia nimejikuta nikiamini maneno niliyokuwa nikiyapata kijiweni kwamba Kibanda ni mmoja wa beneficieries wa Ufisadi kutoka tasnia ya Habari nchini

Kwanza nianze kwa kusema, Great Thinker hawezi kujenga hitimisho kwa kusoma makala moja ya mwandishi ambayo ukiichunguza kwa undani inajaribu tu kueleza wasifu wa mlengwa (Kinana).

Nafikili umeisoma makala kwa jicho moja huku tayari ukiwa una mawazo hasi kwa mlengwa (Kinana), matokeo yake hata mwandishi wa makala naye utamuona ni hasi.

Huu ndiyo ukweli, Kinana kwa kiasi kikubwa ameiwezesha CCM kujikusanya wakati wa kampeni zote za marais katika mfumo wa vyama vingi nchini. Hata pale ambapo kampeni za mwisho (2010) za urais zilitawaliwa na makundi aliweza pia kuyakutanisha na kuwa kitu kimoja.

Kelele za mizengwe haziwezi kufuta ukweli. linapokuja swala la oganaizesheni, Kinana ni kinara kwa hilo.

Kazi ya Ukatibu mkuu wa chama siyo kila kukicha kupiga kelele majukwaani kama wengi wanavyoaminishwa, bali ni oganaizesheni ndani ya chama.

kumuhukumu Absalom Kibanda kwa hili na kusema ni puppet wa mafisadi ni kutomtendea haki ukilinganisha na makala zake nyingi nyingine alizoandika pamoja na kwamba kila kitu Tanzania kinawezekana.
 
Umahiri wa Kinana kiutendaji siuoni na in fact ni kosa kubwa tena sana kumpima Kinana kwa nafasi ya Kampeni Meneja wa chaguzi zetu ambazo siyo huru na haki. Sura halisi ya Kibanda sasa ipo wazi. Huyu tunayemsoma sasa ndiye Kibanda mwenyewe. Yule wa mwanzo alikuwa feki. Kibanda genuine ni huyu anayedhihaki vita dhidi ya ufisadi na bila shaka atakuwa tayari amevuta mlungula unaotokana na huo ufisadi.
 
kajichokea, najua baada ya kumaliza kuandika utumbo wake alimpelekea kinana asome kwanza ndio akatoa gazetini. njaa kitu mbaya sana.amenichefua!
 
Kwamba ufisadi ni hoja nyepesi isiyo na mashiko? Hizi bahasha zimepofusha wanahabari wetu.

Hivi vijichenji kutoka Uswiss vinawafanya vibaya
position.jpg
 
Honesty is a very expensive GIFT. Do not expect it from cheap people.LIKE KIBANDA Nau sio Mwita Maranya?

Nimekusoma nivea lakini nikuulize kitu, una uhakika kwamba kibanda amekuwa honesty katika hii makala yake ama anamtumikia kafiri apate mradi wake. Angekuwa honesty kama angekiri tu kwamba ana maslahi na mtu/watu hao.

Ukijitahidi kuunganisha dots utaona ni kwanini kibanda anaandika makala very cheap kama hii. Tafuta uhusiano ama ukaribu/umbali wa Kinana na Lowasa ndipo ujue kilichopo nyuma ya pazia.

Kwamba kwake yeye ufisadi wa Samwel Sitta wa kununua madawa ya shilingi milioni mbili na kujenga ofisi ya spika ya sh.500 milioni jimboni kwake urambo ni zaidi ya ufisadi ambao umekuwa ukifanywa na Lowasa miaka nenda rudi na ambao kimsingi umeliingiza taifa hili katika matatizo makubwa sana ya kiuchumi na kusababisha umasikini mkubwa kwa watanzania.

Hakuna namna yoyote mtu unaweza kuwa honest kwa kutetea ufisadi na mafisadi. Angekuwa honest angewashambulia wote kwakuwa hakuna fisadi mdogo wala mkubwa.
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom