Mgodi wa Bulyanhulu, utafiti wake umefanyika kwa miaka mingi kuanzia miaka ya 1970. STAMICO walifanya wakaishiwa pesa na utaalam. Wakafuata Placedome, wakaja Sutton Resources na baadaye Barrick. Utafiti ndiyo unaowezesha mgodi kuanza kujengwa. Mgodi siyo shamba la mahindi au maharage ambalo mazao yake huweza kubadilika kufuatana na msimu au hali ya hewa. Taarifa zilizopatikana kabla ya kuujenga mgodi ni hizo hizo mpaka leo, na ndiyo zinazoongoza uchimbaji na uchenjuaji.
Taarifa hizo hupatikana baada ya kazi ya muda mrefu iliyohusisha watu wengi wenye ujuzi mbalimbali. Sisi ndiyo tuliofanya utafiti. Nilikuwepo pia miaka ya mwanzo ya uzalishaji. Baadaye niliondoka na kuendelea na kazi hizo hizo ndani na nje ya Tanzania mpaka leo. Alichoandika Mruma na wenzake hakipo katika Ulimwengu huu labda kama ni ugunduzi mpya. Na kama ni ugunduzi mpya basi ungekuwa kwa mgodi mpya siyo huu ambao taarifa zake zinafahamika sana.