Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam imepokea kwa mshangao na kupinga vikali kauli za Mkuu wa Wilaya ya Temeke Ndg. Sixtus Mapunda kuhusu mpango wa kuhamisha wakazi na kuathiri uwepo wa kata zipatazo 10 katika Wilaya ya Temeke kwa madai ya kupisha ujenzi au shughuli za Bandari Kavu (ICDs). Kauli hiyo ilitolewa tarehe 27 Agosti 2026 akiwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndg. Albert Chalamila, kwenye eneo la Kirimanjaro ICD, Kurasini.
Katika kauli hiyo, Ndg. Mapunda alisema kuwa Manispaa ya Temeke imeandaa kata 10 nyingine kufuata mfano wa Kurasini kwa ajili ya matumizi yanayohusiana na Bandari, huku akieleza kuwa wananchi wanapaswa kuelewa kuwa ‘Bandari haihami, ila sisi wanadamu tunaweza kuhama.
Inasitikisha sana, ingawa haishangazi kusikia hivyo kutoka Viongozi wa CCM kutoa kauli hizo katika hali ambayo Dar es Salaam imeshuhudia ongezeko kubwa la bandari kavu, vituo vya makasha na maghala ya mizigo. Utitiri huu umechangia msongamano mkubwa wa malori, foleni kubwa barabani, uharibifu wa barabara, ucheleweshaji wa mizigo, kuongezeka kwa gharama za biashara na kuvurugika kwa maisha ya wananchi.
Kauli ya awali ~ DC Mapunda: Baada ya Kurasini, Temeke tumetenga Kata 10 nyingine kwa matumizi ya Bandari
ACT Wazalendo Mkoa hatutakubali wananchi wa Temeke kuwa wahanga wa uzembe wa Serikali katika mipango miji na usimamizi wa sekta ya usafirishaji. Hatutakubali kata za wananchi kufutwa, wakazi kuhamishwa na maisha yao kuvurugwa wakati Serikali yenyewe imeshindwa kutumia maeneo ambayo tayari iliyatenga na kuyawekea miundombinu kwa ajili ya shughuli za bandari kavu.
Serikali tayari ilitenga na kuendeleza eneo la Kwala, Mkoa wa Pwani, kwa madhumuni ya kuhudumia shughuli za bandari kavu. Eneo hilo limeunganishwa na miundombinu muhimu ya usafirishaji na lilikusudiwa kupunguza msongamano wa mizigo katika Jiji la Dar es Salaam.
Kwa hiyo, ni kinyume cha mantiki kwa Serikali kushindwa kutumia kikamilifu Kwala halafu leo ije na mpango wa kufuta kata na kuwahamisha wananchi wa Temeke ili kupisha shughuli ambazo zinaweza na zinapaswa kupelekwa nje ya Jiji la Dar es Salaam.
ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam tunaendelea kuunga mkono tamko la Waziri Kivuli wa Miundombinu, Ujenzi na Uchukuzi wa ACT Wazalendo Ndg. Abdallah Mtutura la kutaka bandari kavu ziondolewe katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kusitisha utolewaji wa vibali vipya na shughuli hizo kuelekezwa Kwala.
Aidhai, tunamtaka Mkuu wa Wilaya wa Temeke kusitisha mara moja mpango wowote wa kuwahamisha wakazi au kufuta kata za Temeke kwa kisingizio cha kupisha Bandari Kavu;
Iwapo Serikali itaendelea kupuuza sauti za wananchi na kusukuma mbele mpango huu wa kuwaondoa wakazi wa Temeke katika maeneo yao, ACT Wazalendo itahamasisha wananchi wa Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba ya kuandamana kwa amani na kupaza sauti dhidi ya mpango huu.
Tunawaambia wananchi wa Temeke kuwa hatutawaacha peke yao katika mapambano haya. Tutatumia njia zote halali kupinga mpango wowote unaolenga kuwanyang'anya wananchi makazi yao na kufuta maeneo yao kwa sababu ya kushindwa kwa Serikali kupanga mji na kusimamia shughuli za bandari.
Imetolewa na:
Ndg. Felix Kamugisha
Katibu wa Mkoa, Dar es Salaam
3 Septemba, 2026