Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Ndugu waandishi wa Habari, Ramadhan Kareem
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu (S.W) kwa kutujaalia Neema ya Uhai hadi sasa na kutujaalia kuwa miongoni mwa viumbe wake waliobahatika kuuona Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan. Inshallah tuendelee kumuomba Allah (S.W) atupe nguvu ya kufunga, kukithirisha Ibadah na atukubalie Ibada zetu katika kipindi hiki na baada ya Ramadhan Inshallah.
Ndugu Waandishi, Pili niwashukuru nyinyi kwa kukubali wito wetu kuja kuchukua yale ambayo chama chenu cha ACT Wazalendo kinakusudia kuyafikisha kwa Umma kupitia kwenu. Chama hiki kinategemea sana ushirikiano wenu ili kiweze kufanikisha mambo yake.
Maudhui ya Mkutano
Ndugu Waandishi, nyote mnafahamu kuwa Nchi yetu kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano zitakabiliwa na Uchaguzi ifikapo Oktoba 2025. Uchaguzi ni mchakato wa muda mrefu na sio tukio la siku mmoja. Una maandalizi yake. Kabla ya kufika Oktoba 2025 ambapo kutakuwa na siku ya kupiga Kura, yapo mazoezi na mtukio mengi ya kiuchaguzi yameanza kufanyika na yanaendeleana kusimamiwa na Tume zetu mbili za Uchaguzi za ZEC na INEC.Kwa upande wa Zanzibar hivi sasa tupo katika awamu ya pili ya uwandikishaji wa wapiga kura wapya na upande wa Uchaguzi unaosimamiwa na INEC karibuni tumesikia kuwa wataanza mchakato wa kupitia majimbo ya Uchaguzi. Zote hizi ni hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Ndugu Waandishi, kumekuwa na Tabia ya baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote kwa upande wa Tanzania Bara na hapa Zanzibar kuingilia michakato hii kwa kigezo cha kulinda Amani na Usalama ilhali wanafanya kazi za Ujumbe wa Kamati za Siasa za CCM Wilaya na Mkoa.
Wakuu hawa wa Mikoa na Wilaya wanatumia vyombo vya ulinzi na Usalama kuwalenga wanachama wa vyama vya Upinzani hususan chama chetu cha ACT Wazalendo na kuwatisha, kuwapiga na kuwadhalilisha ili wasifanye kazi zao za kisiasa vizuri katika kufuatilia mwenendo wa mazoezi haya ya Uandikishaji wa wapiga kura.
Kwa bahati mbaya zaidi, Viongozi hawa huwatisha na kuwakamata hata Waangalizi wa mchakato huu wenye vitambulisho vya Tume (yaani accredited observers) bila ya sababu yoyote ya kisheria. Kwa kutumia kofia hiyo Uenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama Viongozi hawa wamekuwa wakiwaagiza Jeshi la Polisi (OCD na OCS) kuwaweka ndani watu hawa bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote kwa kile wanachoita “kuwahifadhi”.
Ndugu Waandishi, Chama cha ACT Wazalendo kama Taasisi yenye commitment na matumaini ya Watanzania na Wazanzibari katika kulinda Haki za Raia na Haki za Kikatiba tumeamua sasa kulipinga jambo hili kwa mwelekeo mpya.
Tumeamua kuwashauri na kuwasimamia kila Raia, awe mwananchama au asie mwanachama ambae muathirika wa matendo haya ya Viongozi wetu hawa wa Wilaya na Mikoa ya kuwaweka watu ndani kwa kigezo cha kutumia Madaraka waliyonayo chini ya kifungu cha 13 cha Sheria ya Tawakla za Mikoa namba 8 ya mwaka 2014 kwa kufungua mashauri Mahakamani na kudai fidia Pamoja nakuombwa radhi kwa kuvunjiwa Utu na heshima zao.
Na katika hili tumeanza na Raia Mmoja mkaazi wa Mwanyanya, Shehia ya Kibweni anaitwa Sadifa Juma Khamis ambae pia kwa sasa anakalia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A” kama Mkuu wa Wilaya. Huyu yeye kwa kushauriana na Ndugu Khadija Anwar Mohammed na Saidi
Muhuzi Bakari waliokumbwa na matumizi mabaya ya Madaraka ya Ndugu Sadifa akitoa Amri kwa personal capacity lakin akitumia kofia ya Ukuu wa Wilaya ameagiza kupigwa, kuteswa na kuwekwa ndani Raia hawa wawili siku ya tarehe 1 March, 2025 na tarehe 3 March, 2025 kinyume kabisa na maelekezo ya Sheria na utaratibu.
Afisi yangu ya Mwanasheria Mkuu wa Chama imetoa msaada kwa Bi Khadija na Bwana Saidi kupata Wakili na tayari Wakili ameshamuandikia Barua Ndugu Sadifa na imepokelewa jana kupitia Sheha wa Shehia yake ya Kibweni ambae amethibitisha kuipata barua. Katika barua hizo (Demand Notices) Wadai wamedai mambo mawili.
Kwanza Fidia ya Shilingi Milioni Mia Mbili (200,000,000/-) kwa kumsababishia mateso, usumbufu na kumnyima uhuru wake wa Kikatiba. Pili, tumemtaka Ndugu Sadifa aombe radhi hadharani tena kwa maandishi na akiri kosa. Wakili wamemtaka afanye hivyo ndani ya siku saba. Ndugu Sadifa ana hiari yake Kujibu au kutokujibu. Sisi tumempa fursa ya kufanya hivyo. Na akipenda anaweza kuwaita wahusika wakapata kuhusu kiwango.
Hata hivyo akiamua kukaa kimya, haitazuia Wadai Kwenda Mahakamani ambapo huko wanaweza kudai zaidi ya hiki kilichodaiwa kwenye barua. Tuna precedents nyingi za kesi za namna hii ambapo Mahakama ilitenda Haki kwa Raia waliathiriwa.
Kesi za (1) Lawrence Sulumbu Tara Vrs Richard Mwaisemba, The Attorney General and Halfan Matipula. (Civil Case No. 16 of 2023) HC Judge Kahyoza , (2) Mary Peter Otaru Vrs Onesmo Buswelu Namsemba Mwakatobe na Attorney General (Civil Case No. 4 of 2020) HC Judge L.M Mlacha, J
WITO
Chama cha ACT Wazalendo kinatoa wito ufuataoWakuu wa Wilaya na Mikoa
Katika Nyakati hizi za Uchaguzi wachunge sana utendaji wao wa kazi. Ni wazi kabisa wao ni wanasiasa na wajumbe wa Kamati za Siasa za Miko ana Wilaya na Mikoa. Wamekuwa wakitoka hadharani kutoa kauli za kuunga Mkono Chama cha Mapinduzi. Watofautisha kazi za Chama na Ukuu wa Wilaya na Mikoa.
Tume za Uchaguzi
Tunawaomba sana Tume watafakari upya namna ya kuwashirikisha Wakuu wa Wilaya na Mikoa katika Michakato ya Uchaguzi. Hawa ni Wanasiasa na Wajumbe wa Kamati za Siasa kwa Chama cha Mapinduzi. Hakuna Mahali kwenye Sheria ya Uchaguzi inawapa nafasi Viongozi hawa.Lakini karibuni inaonekana wazi wameupora mchakato. Wamekuwa wanaingia kwenye vituo wanavyotaka, wanatoa Amri nk. Ni vyema Tume ikatwambia wazi wajibu wa Wakuu wa Wilaya na Mikoa ni nini katika zoezi hili hasa matakwa ya kifungu cha 16 cha Sheria Namba 4 ya 2018 (Sheria ya Uchaguzi)
Jeshi la Polisi na Vikosi vyengine
Tunawaomba sana mjiepushe na kupokea maagizo haramu ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa. Wekeni weledi kwenye kazi zenu. Vituo vya Polisi sio sehemu ya kuhifadhi wagomvi wa Wakuu wa Wilaya na Mikoa. Ni sehemu ya kuhifadhi wahalifu. Tunapochukua hatua za kisheria dhidi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya, hatutaawacha Wakuu wa Vituo vya Polisi wanaowahifadhi watu kwa amri haramuPamoja na Salam za Chama, ACT Wazalendo, Taifa Kwanza, Leo na Kesho!
Omar Said Shaaban, Esq
Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo