1. Kujiunga SUK ni kuhalalisha Uchaguzi haramu?
Hapana. ACT Wazalendo kimechukua na kinaendelea kuchukua hatua mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuupinga uchaguzi huu na matokeo yake. Chama kitaendelea kufanya hivyo, ikiwemo kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi nchini unakuwa huru na wa haki.
2. SUK ni hisani ya CCM?
Hapana. SUK ipo kikatiba. Hatupewi na CCM. Tumepewa na Katiba ya Zanzibar. Majimbo tuliyotangazwa kushinda (Pemba) tulishinda kweli. Hata hivyo, Kuporwa kingi hakuhalalishi kususia kidogo kilichopatikana. Ni muhimu ikumbukwe pia kuwa SUK ni zao letu. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ndugu Maalim Seif Sharif kwa kushirikiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar Ndugu Amani Abeid Karume ndio waliokuwa waasisi wa SUK kwa ajili ya kuleta muafaka na maelewano miongoni mwa Wazanzibari.
3. Kujiunga SUK ni kuwasaliti wenzetu waliokamatwa, kuteswa, kuachwa vilema na kuumizwa na wale waliouawa kutokana na uchaguzi?
Hapana. Vitendo vilivyofanywa na Vikosi vya Zanzibar, Vikosi vya JMT (Polisi, Jeshi, Usalama wa Taifa) vya kuuwa, kutesa na kujeruhi watu tena baadhi yao wakiwa mikononi mwa vyombo husika ni vitendo vya kijinai. Jinai haifi. Tutaendelea kutetea haki yao ndani na nje ya nchi hadi haki ipatikane na waliotenda unyama wawajibishwe.
4. Kujiunga SUK kutafifisha kesi yetu ICC?
Hapana. Chama hakitaachana na kesi yake ICC. Kesi itaendelea hadi waliofanya unyama kwenye Uchaguzi Mkuu wawajibishwe.
5. Kujiunga SUK kutafifisha madai yetu kimataifa (Jumuiya ya Madola, AU, Jumuiya ya Ulaya n.k) kuhusu uchaguzi kuhujumiwa?
Hapana. Chama hakitaondoa malalamiko yake kwenye vyombo vya kimataifa kuhusu hujuma kwenye Uchaguzi Mkuu. Tutaendelea kupaza sauti ndani na nje ya nchi kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya ili Uchaguzi uwe huru, haki na wa kuaminika.
6. Viti vilivyotangazwa ni vichache, hakuna mabadiliko yoyote tutakayoleta SUK?
Ni kweli tumedhulumiwa sana. Uchaguzi ungekuwa huru na wa haki, tungepata wawakilishi wengi zaidi. Lakini hilo halitunyimi kuwaruhusu wachache waliotangazwa kwenda kwenye vyombo vya Uwakilishi. Wakati mwingine, wingi si hoja. Kwenye Bunge lililopita tulikuwa na Mbunge mmoja tu, Zitto Kabwe. Lakini, alikuwa na mchango wa kipekee Bungeni. Chama kitahakikisha kuwa kinawasimamia Wawakilishi wake kwenye vyombo vyote wasimame kidete kutetea maslahi ya umma.
7. Kujiunga SUK ni kukosa msimamo kama wa wenzetu CHADEMA?
Hapana. Kila Chama kinapaswa kufanya maamuzi yake kwa kuzingatia maslahi ya Chama na maslahi ya Taifa. Maamuzi haya yamefanywa na vikao halali vya Chama kwa kuzingatia maslahi ya ACT Wazalendo na Taifa kwa ujumla.
8. Kujiunga SUK ni kuwasaliti Wazanzibar?
Hapana. Chama chetu kimezungumza na wanachama na viongozi wetu kwenye Mikoa yote ya Zanzibar. Wengi wanaunga mkono Chama kujiunga SUK.
9. Kujiunga SUK ni kujali maslahi binafsi (Ruzuku, vyeo n.k?)
Hapana. Chama hiki kimesheheni viongozi wengi ambao wana rekodi zisizoyumba za kutanguliza maslahi ya Taifa badala ya maslahi yao binafsi. Hata uamuzi wa sasa wa kujiunga SUK unazingatia maslahi ya Chama badala ya maslahi binafsi ya mtu.
10. Kujiunga SUK ni kurejesha nyuma madai ya Msingi ya harakati ya mageuzi?
Hapana. Mapambano ya kupigania mageuzi nchini hayatakoma hadi mabadiliko ya msingi yanayopiganiwa kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii yapatikane.