ADHABU YA KIFO KWA KUCHINJWA MBELE YA KADAMNASI
SEHEMU YA PILI
Katika sehemu ya kwanza ya makala hii niliandika kwa kina sana juu ya mfumo was adhabu ya kifo inavyotekelezwa nchini Saudi Arabia. Sikuishia hapo tu bali pia nilijadili kuhusu mtelelezaji wa adhabu hiyo (mchinjaji) Muhammad al-Besh.
Katika sehemu hii ya pili ya makala hii nataka nijadili visa vichache vilivyopo nyuma ya maisha ya ya watu ambao walihukumiwa adhabu hii na hatimaye kuchinjwa hadharani. Nataka kujadili ilikuwaje hasa mpaka kupelekea kuhukumiwa visa hivyo?
Katika mjadala wangu huu nitagusia zaidi visa ambavyo viligusa hisia za watu wengi na visa vingine kusababisha hata hasira ya kimataifa dhidi ya nchi ya Saudi Arabia.
KISA #1: RIZANA NAFEEK
Umri: Miaka 24
Uraia: Sri Lanka
Kazi: Msaidizi wa Kazi za Ndani
Tarehe ya kuchinjwa: January 9, 2013, Saa 5 dakika 40 Asubuhi.
Nini hasa kilimkuta?
Rizana Nafeek binti muadilifu wa kiislamu, alizaliwa February 4, 1988 na kukulia katika kijiji cha Moothoor, wilaya ya Trincomalee nchini Sri Lanka.
Kutokana na wazazi wake kuwa wacha Mungu sana ndio maana hata alipozaliwa walimchagualia jina la Rizana mtoto wao likimaanisha "kuomba" (to pray).
Rizana ndiye mtoto wa kwanza kwenye familia yao yenye watoto wanne.
Familia yao ilikuwa ni moja kati ya familia masikini zaidi hapo kijijini, waliishi katika kijumba cha "mbavu za mbwa" kilichojengwa kwa nyasi.
Umasikini wao uliokithiri ulichangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na hali tete ya kiafya ya baba yake ambayo ilikuwa haimruhusu kufanya shughuli nzito. Enzi ambazo baba yake alikuwa timamu kiafya, alikuwa anajishughulisha na ukataji mbao msituni, na akasitisha shughuli hizo baada ya afya yake kuzidi kuzorota kadiri siku zilivyoenda.
Kitokana na afya ya mzee Nafeeq kuwa mbaya na kushindwa kufanya kazi, ili waweze kujikimu kimaisha, Rizana na wadogo zake walikuwa wakiokota kuni msituni na kwenda kuuza kijijini, wakati ambapo mama yao alikiwa anasaidia shughuli ndogo ndogo vibarua kwa wanakijiji wengine na kulipwa ujira.
Katika mtindo huu kwa miaka kadhaa ndivyo ambavyo waliweza kuendesha maisha yao.
Kama jinsi ilivyo kwa watoto wote wanaokua katika umasikini wa kupindukia, Rizana akajikuta anapata kiu ndani yake ya kuwa mkombozi wa familia yake. Akajikuta anapata kiu ya kutaka kuitoa familia yake katika aibu ya kuwa familia inayodharaurika na walau aweze kuipa familia yake maisha yenye staha na heshima mbele za wanakijiji wengine.
Ndipo hapa ambapo moja ya binamu zake aliyepo hapo hapo kijijini Moothoor akamshauri Rizana ajaribu "bahati" yake kwenda kutafuta ajira 'Uarabuni'.
Rizana akarudi na wazo hili nyumbani na kuwaeleza wazazi wake kuwa anataka ajaribu "bahati" ya kutafuta ajira Uarabuni.
Wazazi wake walilipinga suala hili mara moja baada tu ya Rizana kulitamka. Hoja yao kuu ilikuwa ni kwamba wanaogopa mtoto wao kwenda kunyanyasika Uarabuni. Walikuwa wamesikia 'stori' nyingi sana kuhusu wafanya kazi wa ndani namna ambavyo walikuwa wananyanyaswa na mabosi wao wakifika kwenye nchi za kiarabu. Hawakutana mtoto wao Rizana naye aende akanyanyaswe, waliona ni bora aendelee kuokota kuni kijijini.
Lakini Rizana alikuwa na kiu haswa ya kuindoa familia yake kwenye umasikini wa aibu, akajitahidi kwa uwezo wake wote kujieleza kwa wazazi wake na hasa hasa ni namna gani ambavyo kwenda kwake Uarabuni kutaleta 'neema' kwenye familia yao. Baada ya kujieleza sana kwa wazazi wake hatimaye wakakubaliana naye kuhusu kwenda kujaribu "bahati" yake huko Uarabuni.
Huu ulikuwa ni mwaka 2005, Rizana alikuwa ni kabinti ka miaka 17 tu.
Hapa ndio nyumbani kwa kina Rizana Nafeek, kijijini Moothoor, nchini Sri Lanka
Baba na mama mzazi wa Rizana Nafeek
Mama mzazi wa Rizana akiwa na wadogo zake Rizana
Baada ya wazazi kukubali Rizana aende kujaribu "bahati" yake Uarabuni, ikafanyika mipango ya kuwasiliana na makampuni ya uwakala wa kutafuta watumishi wa ndani ("mahausigeli") na kuwaunganisha na 'ajira' kwenye nchi za kiarabu. Kampuni hii iliitwa
Badurdeen.
Lakini Rizana alikuwa na changamoto kubwa mbili.
Mosi, alikuwa hajui hata neno moja la kiarabu au kingereza. Lugha pekee aliyokuwa anaifahamu ilikuwa ni Tamil.
Pili, Rizana alikuwa hajafikisha umri wenye kumruhusu kwa mujibu wa sheria za kimataifa kupata ajira kwenye nchi ya kigeni.
Lakini madalali hao walimtia moyo kwamba hakuna changamoto yoyote ambayo wao watashindwa kuisawazisha alimradi tu akiwa tayari kwenda kufanya kazi Uarabuni.
Kuhusu kutojua kiarabu au kingereza, walimtia moyo kwamba wako wasichana wenzake wengi tu ambao nao walikuwa kama yeye wanafahamu 'lugha ya mama' pekee na Kiarabu walikwenda kukijulia huko huko kwenye ajira zao. Suala hili lilikuja kumgharimu sana Rizana huko mbeleni.
Pia kuhusu umri, mawakala hao wa ajira walimtengenezea Rizana cheti kingine cha kuzaliwa cha kughushi ambacho kilionyesha kuwa Rizana ana umri wa miaka 23.
Baada ya mipango hii yote kukamilika, familia ya Rizana wakakopa fedha kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki na kuwalipa kampuni ya Badurdeen ada ya huduma hii ya kumuunganisha binti yao na ajira Uarabuni.
Mkopo huu waliokopa familia ya Rizana kutoka kwa ndugu, jama na marafiki walikuwa wameahidi kuulipa pindi tu ambapo Rizana akifika Uarabuni na kuanza kupokea mshahara.
*********
Siku ya tarehe 1April 2005, Rizana aliwasili kwenye mji wa *Dhawadhimi* (wengine hutamka "Dwadmi") nchini Saudi Arabia, karibu kabisa na mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh.
Muajiri wake ambaye alikwenda kukabidhiwa kwake alikuwa ni Bw. Naij Jiziyan Khalaf al Otaibi ambaye alikuwa ni afisa wa ngazi za juu katika wizara ya fedha ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa taratibu za kazi nchini Saudi Arabia, kazi ya Uyaya (Nanny) na 'uhausigeli' (house maid) huwa zinatenganishwa lakini mara nyingi binti akiajiriwa anajikuta akifanya shughuli zote hizi mbili, yaani shughuli za nyumbani kama upishi na usafi (house maid) na shughuli za uangalizi wa watoto wadogo (nanny).
Hiki pia ndicho kilichomba Rizana kwa muajiri wake Familia ya Otaibi. Alijikuta anawajibika kufanya shughuli zote za nyumbani za usafi na upishi na papo hapo akiwajibika kuwa muangalizi wa watoto wadogo waliopo kwenye familia ya Otaibi akiwemo mtoto mchanga wa miezi minne ambaye aliitwa
Kayed.
Kwa wiki kadhaa Rizana alichapa kazi pasipo kuwepo na mgogoro wowote na mabosi wake wala kuwepo kwa malalamiko kutoka upande wake.
Kazi ikaendelea, huku ndoto yake kichwani ya kuitoa familia yake katika umasikini uliokithiri ikizidi kuchanua kichwani mwake.
"Siku ya hatma, kiza hakichelewi"
Miezi miwili baada ya Rizana kuwa katika ajira, yaani siku ya tarehe 22 May 2005, Bw. Otaibi na mkewe waliondoka nyumbani asubuhi kama ilivyo ada.
Rizana naye aliendelea na shughuli zake kama kawaida ya siku zote.
Mnamo majira ya kama saa 6 na nusu mchana akaanza kumpatia maziwa mtoto mchanga Kayed ambaye naye alikuwa ni jukumu lake kama siku zote. Maziwa haya alikuwa anampatia kwa kutumia chupa ya watoto ya kunyonyeshea.
Akiwa anaendelea kumpa mtoto maziwa, alipokuona ameshiba akamuachia chupa achezee na kisha kwenda jikoni kuangalia maendelea ya chakula alichokuwa anapika. Ilimchukua dakika kadhaa akiwa jikoni, takribani dakika tano nzima na aliporejea alishapigwa na butwaa kumkuta mtoto mchanga Kayed chupa ameweka mdomoni kama anainyonya lakini amefumba macho.
Rizana akamuinua Kayed na kuanza kumfungua macho. Lakini kila akimfungua macho mara moja yanafunga tena. Lakini pia akagundua kuwa Kayed alikuwa hapumui.
Baada ya kumchunguza akagundua kwamba, Kayed alikuwa amebanwa pumzi (ame-suffocate) kutokana na kunyonya vibaya chuchu ya chupa ya maziwa na kusababisha kuziba koo la kupitisha hewa.
Kutokana na utoto wake (kumbuka ni binti wa miaka 17 tu) akaanza kulia na yeye papo hapo asijue afanye nini.
Watoto wengine wadogo wa familia ya Otaibi waliokuwa wanacheza chumba kinachofuata waliposikia kilio cha Rizana walikimbilia chumba hicho alichomo na kumkuta analia huku anampindua pindua mtoto na kujaribu kumuamsha Kayed.
Watoto hao nao wakabaki wamepigwa butwaa tu wasijue nini kinaendelea au wamsaidieje Rizana au Kayed.
Ghafla muda huo huo Mke wa Otaibi akarejea nyumbani na moja kwa moja akaelekea chumba ambacho alisikia kilio kinatoka huko tangu yuko getini.
Alipofika alimkuta Rizana amembeba Kayed mikononi huku analia. Mara moja mke wa Otaibi akamchukua Kayed kutoka mikononi mwa Rizana na mara tu baada ya kumgusa ndani ya sekunde chache aligundua kuwa mtoto mchanga Kayed ameshafariki.
Kama vile mbogo aliyejeruhiwa, Mke wa Otaibi alimrukia Rizana kwa hasira na kuanza kumshambulia huku akipiga yowe la kilio, akirudia neno moja tena na tena….
"KWANINI UMEMUUA MWANANGU..!!"
Itaendelea post inayofuata hapo chini...