Pre GE2025 Ado Shaibu: Hatutashiriki Vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
Joined
May 5, 2014
Posts
631
Reaction score
1,577
TAARIFA KWA UMMA

BARAZA LA VYAMA VYA SIASA LIMEPOTEZA UHALALI

Kamati ya Uongozi Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo kwenye kikao chake cha tarehe 10 Machi, 2025 imeazimia kutoshiriki vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa kuanzia kikao cha tarehe 12 na 13 Machi, 2025 kwa sababu zifuatazo;-

1. Baraza la Vyama vya Siasa linaloratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini limepoteza uhalali baada ya kushindwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na Vyama vya Siasa kwa ajili ya kujenga na kukuza misingi ya demokrasia nchini ya vyama vingi nchini, ambalo lilikuwa ndiyo lengo lake kuu wakati linaanzishwa.

2. Baraza la Vyama vya Siasa limegeuzwa kuwa jukwaa la kutumika kuhalalisha na kusafisha uchafuzi na wizi katika chaguzi kama ilivyofanyika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.

3. Serikali kupuuza maazimio ya Baraza la Vyama vya Siasa ya kuboresha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024;

Kwenye Kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kilichofanyika tarehe 11 Oktoba 2024 Jijini Dodoma na kutanguliwa na vikao vya Kamati za Baraza na Kamati ya Uongozi ya Baraza, maazimio mbalimbali yalifikiwa kuboresha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Serikali, kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitoa ahadi ya kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.

Kinyume na ahadi yake ambayo ilitolewa kimaandishi, Serikali iliyatupa mapendekezo ya Baraza la Vyama vya Siasa na kuendelea na mpango wake wa kudhulumu sauti ya wananchi kupitia wizi wa kura na uchafuzi kama ilivyoshuhudiwa nchi nzima.

WITO WETU
1. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kama kweli inataka tulichukulie Baraza hili kuwa ni chombo makini cha sisi kushiriki shughuli zake basi iweke mezani kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi na marekebisho mengine ya Sheria za Uchaguzi ikiwemo Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na pia mabadiliko madogo ya Katiba yatakayopelekea kufanyika kwa Uchaguzi Huru na wa Haki.

2. Chama cha ACT Wazalendo kimewasilisha tena kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa uchambuzi wake wa kina wa masuala yanayohitaji kufanyiwa maboresho katika tasnia ya siasa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu 2025 unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

3. Kinyume na hapo, ACT Wazalendo hatutakubali kutumika kuhalalisha na kusafisha uchafu unaoandaliwa ili kupora mamlaka ya wananchi ya kuchagua na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka kama yalivyo matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 9 ya Katiba ya Zanzibar.

Imetolewa na;
Ado Shaibu
Katibu Mkuu
ACT Wazalendo

11 Machi, 2025.
Dar es Salaam.

 
Kumeanza Kuchangamka..
Kwa kua nchi ni yetu sote bila kujali imani za dini na vyama, ni wakati sasa wa nyote muungane mkae na chama tawala na serikali mshauriane namna bora ya kutuvusha wananchi kwenye uchaguzi huu..

Hatuoni kama mbele kuzuri..!!
 
Laiti agenda ya No Reform No Election ingebebwa na vyama vyote vya upinzani kazi ingekuwa imekwisha lazima reform ingefanyika na Uchaguzi wetu ungeheshimka na wote, lakini kwa sasa hiki kinachoitwa uchaguzi ni mchezo wa kuigiza ambao unatumia mamia ya mabilioni ya fedha na kuzalisha viongozi haramu ambao hawatokani na matakwa wananchi
 
Safi sn no reforms no election.
 
Serikali tayari imo kwenye mchakato wa kuelekea kwenye uchafuzi 2025. Hatua hizi zinazo fanyika sasa hivi ni mwendelezo wa kuelekea huko.
Sasa niwasihi ACT-Wazalendo na vyama vingine vya upinzani visiishie kutoa matamko kama hili na kusubiri; huku serikali ikiendelea na juhudi zake kuelekea kwenye uchaguzi. Ni wakati hivi vyama na wao wawe na program ya nini kifanyike hapo tutakapo kuwa serikali imetufikisha kwenye hatua za mwisho na kujiandaa kupiga kura.
Haitoshi kutoa matamshi tu kama haya hapa, halafu na kusubiri, huku serikali ikiendelea na mchakato kama ulivyo pangwa.
Sasa niwaulize ACT-Wazalendo, ni lini juhudi za kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki zitaanza, na ni zipi hizo?
Mnasubiri kuzitekeleza juhudi hizo lini, siku ya uchaguzi? Mbona mtakuwa mmechelewa sana!
 
Ccm inavitumia vyama dhaifu Ili kupitia katikati Yao kuhalalisha uchaguzi
 
Hawa ACT akili zimerudi lini? wao si walikuwa wanaona CHADEMA inalalamika sana, kwamba wananjiona wao ndio chama cha muhimu pekee, kwamba huwezi kuwa unagoma, kupinga na kususia kila kitu kifanywacho na ccm.

Sasa kumetokea nini huko tena?
 
Asanteni sana ACT WAZALENDO kwa kuunga mkono kwa vitendo hoja zote zinazobebwa na kauli mbiu ya NO REFORMS, NO ELECTION...

There's no way kwamba nchi hii inaweza kupata ukombozi na mabadiliko ya mifumo ya kuweka viongozi watokanao na utashi wa wananchi kwa njia ya chaguzi HURU, ZA HAKI NA ZA WAZI isipokuwa kwa kukataa kwa herufi kubwa ulaghai (manipulation) wa walio madarakani wanaotumia kila njia na mbinu haramu ili kuendelea kushikilia madaraka na mamlaka yao isivyo halali....

Na sasa wamefikia hatua mbaya kabisa ya kutesa na kuua watu ili kulinda mamlaka na madaraka yao kwa kumwaga damu zisizo na hatia yoyote. Hii haikubaliki, Mungu amekataa na mkono wa hukumu ya haki ya Mungu Yehova uwe juu yao sasa...!

Karibuni kwenye mapambano...

Na tukumbuke daima hili: Mungu Jehovah akiwa upande wetu sisi wenye haki, ni nani aliye juu yetu? Nani atakayemshinda Mungu wetu mwenye haki...?
 
Now you are talking, No Reform No Election.
 
ACT Wazalendo na wao wanaanza kuchangamka, kule kuna NO REFORM ya CHADEMA, CCM imewekwa kati
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…