Kwa muda mrefu sasa ushirikiano kati ya China na Afrika ulijikta kwenye ushirikiano kati ya pande mbili, yaani ushirikiano kati ya China na nchi moja moja ya Afrika, uliojikita kwenye mahusiano kati ya serikali. Kutokana na kuendelea kupevuka kwa ushirikiano kati ya China na Afrika, wigo wa ushirikiano umepanuka na kufikia ngazi ya jumuiya za kikanda na bara, na ngazi zote za ushirikiano mbali na kuhusisha ushirikiano wa kiserikali, sekta binafsi pia imekuwa ni mdau muhimu wa maendeleo.
Moja kati ya maeneo ambayo China na Afrika zimekuwa zikiyataja kwenye mambo ya ushirikiano na bara la Afrika, ni kuoanisha mikakati ya maendeleo, China kwa upande mmoja ikiwa na pendekezo la Ukanda “mmoja, njia moja” (BRI) na Afrika kwa upande mwingine ikiwa na Ajenda ya maendeleo ya Umoja wa Afrika kuelekea mwaka 2063 (Agenda 2063),.
Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia moja lililotolewa na China, kwa Afrika ni pendekezo ambalo kimsingi linaitikiwa mahitaji ya sasa ya maendeleo ya bara la Afrika. Kwa muda mrefu uliopita baada ya uhuru, miundo mbinu mingi ya Afrika iliendelea kuwa katika hali duni, pendekezo hilo limefanikisha mabadiliko makubwa katika eneo la miundo mbinu barani Afrika, ambayo sio tu yameleta miundo mbinu ambayo inahitajika sana kwa maendeleo ya kiuchumi ya Afrika, bali pia ajira, ujuzi na urahisi kwenye mambo ya usafiri vimeleta mabadiliko makubwa kwa nchi za Afrika.
Tukiangalia baadhi ya malengo makuu ya ajenda ya mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika, kama kuinua kiwango cha maisha ya waafrika wote, kuhimiza elimu na maendeleo ya sayansi, elimu na afya bora kwa wote, mabadiliko chanya ya kiuchumi, na kilimo cha kisasa, tunaweza kuona kuwa mengi yanaweza kufanikishwa kama kukiwa na miundo mbinu imara, ya mawasiliano ya habari, usafiri na hata majengo. Ndio maana wanazuoni wa China na Afrika wanapozungumzia kuunganisha Pendekezo la “Ukanda mmoja, Njia moja” na “Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika”, wanamaanisha kuwa hayo ni mambo mawili ambayo yanaweza kuharakisha kutimiza lengo moja.
Tukumbuke kuwa moja ya manufaa ya ushirikiano kati ya China na Afrika kupitia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja” ni kuwa kwa sasa bara la Afrika limekuwa linajitahidi kuhimiza biashara ya ndani ya Afrika, kwa kutekeleza eneo la biashara huria la Afrika (AfCFTA). Eneo hilo lililozinduliwa rasmi mwaka 2021 linatarajiwa kuwa na watu bilioni 1.7 na thamani ya biashara ya dola za kimarekani trilioni 6.7 ifikapo mwaka 2030. Licha ya malengo haya mazuri na takwimu hizi, bila kuwa na miundombinu imara ya ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi za Afrika, itakuwa ni vigumu kwa biashara ya ndani ya Afrika kukua. Hii ina maana kuwa ushirikiano kwenye ujenzi wa miundombinu kati ya China na Afrika, unakidhi maslahi ya kimsingi ya bara la Afrika.
Kutokana na sababu mbalimbali zinazotokana na hali ya sasa ya dunia, uchumi wa China kama ulivyo uchumi wa nchi nyingine duniani pia unakabiliwa na changamoto kubwa. Baadhi ya wachambuzi wamefikia hatua ya kusema kuwa hali hii inaweza kupunguza nguvu ya China katika kuchochea maendeleo ya Afrika. Lakini ukweli ni kwamba wigo wa ushirikiano kati ya China na Afrika kwa sasa umepanuka sana, mbali na makampuni ya serikali kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya ushirikiano, makampuni binafsi ya China na hata wafanyabiashara na wawekezaji binafsi wa China pia wanashiriki kwenye mambo ya kiuchumi. Hali hii inafanya ushirikiano wa uchumi na nguvu ya China kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika iendelee kuonekana.