Familia za vijana kutoka Mathare na Huruma zimefika hadi Bungeni kudai majibu kuhusu wapendwa wao waliotoweka katika mazingira yasiyoeleweka.
Juni 18, 2026: Joel Kariuki Mwai, mfanyabiashara na aliyewahi kuwania udiwani, aliripotiwa kutekwa na watu waliokuwa wamevalia kiraia katika eneo la Mashimoni, Mathare. Mashahidi walidai watu hao walijitambulisha kama maafisa wa polisi.
Juni 19: Michael Oloo Osura aliripotiwa kutoweka eneo la Umoja karibu na Caltex.
Juni 20: Macmillan Kiarie aliripotiwa kuchukuliwa na watu waliokuwa kwenye gari lisilo na nambari za usajili karibu na Kizito Stage, Githurai.
Juni 23: Abdulaziz Duba Molu, maarufu Zizo, mkazi wa Huruma/Kiamaiko, aliripotiwa kutoweka. Kutoweka kwa Zizo na Kiarie kulichochea maandamano ya wakazi waliotaka kujua waliko vijana hao.
Maandamano na vifo
Juni 30, wakazi wa Mathare, Huruma, Kiamaiko na Kariobangi North waliandamana wakidai vijana hao wapatikane.
Barabara kadhaa, ikiwemo Outer Ring Road, zilifungwa na polisi wakatumia mabomu ya machozi. Mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine wawili kujeruhiwa.
Suala lafika Bungeni
Julai 1, Mbunge wa Mathare Anthony Oluoch aliwasilisha suala hilo Bungeni, akiomba serikali kueleza waliko Joel Kariuki, Michael Oloo, Macmillan Kiarie na Abdulaziz Molu.
Hansard ya Bunge ilisema mmoja wao alikuwa amepatikana, huku juhudi zikiendelea kuwatafuta wengine.
Hadi sasa, familia zinaendelea kudai majibu kuhusu waliko wapendwa wao, nani aliwachukua na kilichowapata baada ya kutoweka.
Katika video ya NTV, akina mama kutoka Mathare na Huruma wanaonekana kufikisha malalamiko yao hadi eneo la Bunge, wakitaka mamlaka ziwape majibu.
Kwa familia hizi, safari haijaisha wanataka kujua: Vijana wao wako wapi?
Source: NTV