Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
ALLY SYKES, PETER COLMORE, ALBERT ROTHSCHILD NA OSCAR KAMBONA
Fred Nyaluchi ni kijana ambae ameonyesha hamu kubwa sana ya kutaka kujifunza historia ya uhuru wa Tanganyika.
Kwa kauli yake anasema amevutiwa sana na makala ninazoandika na wakati mwingine huzirudia makala hizi akaziwakilisha kwa namna yake ambayo hupendeza kwa msomaji.
Hivi karibuni ameweka katika mtandao historia ya koo 13 anazodai kuwa zinazotawala dunia na moja katika koo hizo ni ukoo wa Rothschild.
Pamoja na haya amegusia Freemasons.
Suala la Freemasons limekuwa katika midomo ya watu wengi katika miaka hii ya karibuni.
Nimemwandikia Nyaluchi na kumueleza kuwa mengi yameandikwa kuhusu hayo yake ya ukoo wa Rothschild, Freemasons nk. nk. aliyotuandikia lakini tatizo kama ninavyoliona mimi na kwa muda wa miaka mingi ni kule kupata ukweli wa hayo ambayo yanayosemwa kuhusu Rothschild na Freemasons.
Nimeishi na watu waliokuwa karibu sana na mimi ambao ikisemwa ni Freemasons lakini tofauti na nyakati hizi siku zilizopita Freemasons watu wakiiogopa na kuhisi ni taasisi moja yenye usiri mkubwa wa kutisha.
Miaka hii karibuni hofu hii haipo tena na mkubwa wa Freemasons hapa Tanzania, marehemu Andy Chande amekuwa akiandikwa kwenye magazeti na sura yake ikionyeshwa katika televisheni akieleza shughuli za taasisi hiyo tofauti na miaka iliyopita.
Hapo chini nataka nimweleze Albert Rothschild kwa faida ya rafiki yangu Nyaluchi na kwa faida ya wasomaji kama nilivyokutananae katika kumbukumbu za Sykes.
Ally Sykes anamweleza Rothschild na hii ilikuwa mara tu baada ya Azimio la Arusha na yeye kwa kushindwa kufuata masharti ya kiongozi kutofanya biashara na kuwa na nyumba za kupangisha, Ally Sykes ilibidi aachishwe kazi serikalini kwa barua aliyoandikiwa na Bhoke Munanka:
‘’Nilikuwa tayari nimeshaingia katika aina nyingine za biashara.
Nilikuwa nawakilisha makampuni kadhaa ya kuuza madawa na vipuli kutoka Ulaya na Marekani.
Biashara hii mpya ikanifanya niwe nasafiri sana kwenda Ulaya na Marekani.
Katika hali kama hii nilipata marafiki wengi wenye nguvu na maadui pia wenye uwezo kama huo.
Katika marafiki zangu wenye nguvu alikuwa Albert Rothschild, mtu maarufu katika dunia ya mabenki.
Ngoja nieleze kisa kifupi ambacho Rothschild na mimi tulikutananacho kinachowahusu maofisa wa serikali ya Tanzania.
Rothschild alikuwa Myahudi na akiishi Paris.
Nilimfahamu Rothschild Nairobi kupitia Peter Colmore.
Tukawa marafiki na mwenzangu katika biashara.
Nilimtia Rothschild hima aje Tanzania kuangalia uwezekano wa kufungua biashara.
Ilikuwa siku moja wakati yuko Madagascar ndipo akanipigia simu kunifahamisha kuwa anakuja Dar es Salaam na nimpokee.
Mimi sikuwa nafahamu, kumbe Oscar Kambona, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje pia alikuwapo uwanja wa ndege kaja kumpokea Rothschild kama mgeni wa serikali.
Rothschild alikuwa ametua na ndege yake binafsi akiwa na wasaidizi wake.
Alipitishwa haraka sehemu ya VIP lakini Kambona alipigwa na butwaa pale Rothschild alipomwambia kuwa asingependa gari la serikali lililokuja kumchukua bali ataingia katika gari yangu na kufuatana na mimi mjini.
Hii ilikuwa kinyume cha itifaki lakini hakukubali akashikilia kupanda gari yangu.
Rothschild akapanda gari yangu akawa na mimi na mke wangu.
Nikafanya mazungumzo ya biashara na yeye kabla hajakutana na maofisa wa serikali ya Tanzania.
Haya yaliwaudhi sana watu fulani ndani ya serikali.
Mimi sikuona kosa lolote kwani sote tulikuwa tunahangaika katika kujenga nchi yetu na kumfanya mwekezaji ajihisi yuko katika mikono ya watu wema wa kuweza kutegemewa.
Kitu ambacho mimi sikuwa nakifahamu kwa wakati ule ni kuwa nilikuwa nachunguzwa na vyombo vya usalama.
Wivu na choyo vilikuwa vimeingia katika mioyo ya watu fulani wakubwa ndani ya serikali.
Hii haikuwa mara yangu ya kwanza kuwa chini ya uchunguzi wa serikali.
Wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika wakoloni nao pia walikuwa waneniweka chini ya uchunguzi.
Itakuwa jambo zuri kwa watafiti kutafiti jinsi wakoloni walivyotumia vyombo hivi vya mabavu dhidi ya wazalendo wapigania uhuru.
Kwa hakika kabisa nilikuwa nafahamu kuwa marehemu Amiri Kweyamba, siku zile yuko Special Branch, alikuwa akipeleka taarifa zangu na za Julius Nyerere serikalini.’’
Kutoka mswada wa maisha ya Ally Sykes: ''Broken Dreams the Life of Ally Kleist Sykes (1926 - 2013).''