Wana jf kuna swali ambalo Rais Magufuli huwa anatuuliza watanzania kila wakati kuhusu nani aliyeturoga na kusababisha watanzania tusiwe na uchungu na mali zetu hata zinapoporwa mchana kweupe. Sijasikia watu wakimpa majibu Rais wao kuhusu "Nani ameturoga" Je, wewe unalo jibu la kumpa Rais Magufuli kuhusu hili swali lake?
Nijuavyo mimi mtindo huu wa kutothamini mali zetu za taifa ulianziaga kipindi cha Ujamaa na Mashirika ya umma (SU) wakati wa Mwl. Nyerere. Kipindi kile watu walikuwa hawathamini mali ya umma hata kidogo wakidhani kuwa ilikuwa ni mali isiyokuwa na mwenyewe hadi wakatoa tafsiri ya "SU" ni Soma Ule. Mali za mashirika kama RTC, NMC, UDA, kaMAta, NAFCO na bodi za mazao kama KNCU n.k zilikuwa zinaliwa na wasomi wachache waliopewa dhamana za kuyaongoza. Na wananchi hatukuwa na uchungu nayo hata pale tulipokuwa tunawaona waliopewa dhamana za kuyaongoza wakiyafuja, maana tulikuwa tunadhani wanafuja mali isiyokuwa ya kwetu bali mali ya "umma". Hakujua wala kuwahi kuambiwa kuwa umma ni sisi na sisi ni umma.
Hatukuwahi kuambiwa kuwa elimu, afya, barabara, maji, umeme na huduma nyingine ambazo tulikuwa tukipatiwa bure zilikuwa zikitokana na mali hizo zilizokuwa zinafujwa na watanzania wenzetu waliokuwa wakiziiba na kuzitumia kwa manufaa yao, badala yake tulikuwa tukiwasifu na kuwaona kama watu "waliopata kazi nzuri". Hivyo kila mzazi alitamani mwanawe asome ili aajiliwe kwenye mashirika hayo ya umma (SU) kwakuwa wataleta nyumbani kwa wingi hela, sukari, unga, mifugo, bia, nguo, sabuni na bidhaa zilizokuwa zikizalishwa na SU hizo. Hatukujua kuwa kumbe mashirikia yale yalikuwa pia ni yetu hivyo walikuwa wakituibia sisi.
Dhana hiyo ya mali ya umma ilichagizwa pia na kitendo cha serikali kuzitumia mali zetu hizo (umma) na kuzitumia kwa harakati za ukombozi wa bara la Afrika bila idhini yetu yetu umma. Hivyo hadi leo umma hauna habari kuhusu ni mali ya umma kiasi gani tuliitumia katika zoezi zima kulikomboa bara la Afrika na itarejeshwaje au umma utafaidikaje za kwa kuzikomboa nchi nyingine. Watawala wetu waliitumia mali ya umma kama mali yao ya mfukoni bila kutushirikisha kikamilifu katika matumizi yake. Walikuwa wanafanya kwa niaba yetu, hivyo ikawa sawa na kumfunika blanket mtu anaejisikia joto na kumfunika shuka mtu anayejisikia baridi kali.
Hivi ndivyo vilivyoutafuna uzalendo wa wananchi wetu kwa mtizamo wangu.