HIVI HAYA HAPA CHINI TOKA MDOMONI MWAKE HUKUYASIKIA?
Rais Magufuli alisema alipoingia alikuta makusanyo ya mapato ni Sh bilioni 850, lakini baada ya kubana mapato yaliongezeka hadi Sh trilioni 1.5, akisema makusanyo hayo yalikuwa yakiliwa na wachache wachache walioko ngazi ya juu.
Aliongeza kuwa spidi yake ya kufanya kazi ni kubwa hivyo hataki kuona mtu anamkwamisha kwa kuwa amepanga kufanya mambo mazuri. Alisema ndio maana wameamua kujenga reli ya kisasa ili kubeba mizigo ya kutosha, kununua ndege tatu na mbili zitaingia mwezi ujao na kwamba serikali imetenga Sh bilioni 100 kwa ajili ya kuboresha viwanja vya ndege vya Iringa, Songea na Musoma.
Alizitaja huduma nyingine ambazo serikali imeamua kuboresha ni umeme ambapo mradi wa Kinyerezi II una megawati 240 na Kinyerezi I utaongezewa megawati 185 na pia Kinyerezi III na IV inakuja ili kuongeza usambazaji wa umeme nchini uwe mkubwa.
Alisema bajeti ya maji mwaka huu imeongezwa na pia kwa Dar es Salaam kuna mradi wa maji unakuja, na pia wamepata mkopo wa dola za Marekani milioni 500 (sh trilioni 1.05) kutoka Serikali ya India.
Kwenye sekta ya afya, alisema wametenga Sh trilioni 1.99 na kwamba wametenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya kununulia dawa hospitalini tofauti na mwaka uliopita ambapo ilitengwa Sh bilioni 25.
Chanzo: Habari Leo