*JOANA ANAONA KITU USIKU --- 12*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Joana akajikuta amepandwa na hasira. Alihisi kichwa kimekuwa cha moto na mwili umenyanyuka pasipo kujitambua.
alielekea kabatini akatoa rungu moja kubwa, kisha akaenda mlangoni na kufungua. Moa akaingia, lakini akakutana na rungu kubwa kichwani - pam! akadondoka kama kiroba akivuja damu kichwani.
ENDELEA...
Joana akatahamaki kwa mshangao. Ni kama vile si yeye aliyefanya hilo tukio.
"Mungu wangu, nimeua!" alisema akishika kichwa. Lisa alikuwa ameachana mdomo macho yakimtoka.
"Lisa tunafanyaje sasa?" Joana akauliza akikung'uta viganja vyake. Jasho lilikuwa tayari limeshamvuja.
Lisa akanyanyuka upesi toka kitandani na kwenda kuweka mgongo wa kiganja chake mbele ya pua ya Moa. Akasikilizia kwa sekunde kadhaa.
Loh! Moa hakuwa anahema!
"Ina maana amekufa?" Joana akawahi kuuliza. Uso wake ulifinyangwa na hofu kubwa. Hajawahi kuua akiwa na akili zake timamu.
"Inawezekana akawa amekufa," Lisa akajibu kwa sauti ya chini.
"Sasa tunafanyaje jamani! Lisa tunafanyaje?"
"Sijui, Joana! Hii ni kesi kubwa, tutaenda kufia jela."
Joana akazidi kuchanganyikiwa. Lisa alijaribu kumtuliza na kumwambia:
"Usijali, Joana. Hakuna mtu anayejua kama Moa amekuja humu."
"Una maanisha nini, Lisa? Hata kama hakuna mtu anayejua, tutaupeleka wapi mwili wa Moa?"
"Joana, inabidi ufikirie mara tatu zaidi. Upo radhi tukamatwe na kufia jela?"
Joana akajibu kwa chozi.
"Basi ndiyo tutafute namna ya kufanya. Tatizo tayari limeshatokea, na kulia kwetu hakutasaidia."
Wakakaa kama dakika tano, bado mwili wa Moa ulikuwepo chini ila umeacha kumwaga damu.
"Tukautupie mwili wake huko mbali," akashauri Joana aliyekuwa anatetemeka.
"Tutapitia wapi?" Lisa akauliza.
"Tutapitia hii njia ya huku uani. Hamna kamera, na ni fupi zaidi."
Wakatazama saa, ilikuwa saa tisa usiku na dakika za mapema. Wakakubaliana kupiga moyo konde na kufanya hivyo ili kujiepusha na kadhia ya mkono wa dola.
Ila wakati wanahangaika na kumnyanyua Moa, wakasikia vishindo vya miguu nje ya mlango. Miili yao ikapoa ghafla kwa baridi la hofu. Walijikuta wanatetemeka kama wametoka kuogea maji ya barafu.
Wakaona ni hatari tena kwenda nje, hivyo wakakubaliana kuutia mwili wa Moa ndani ya kabati na watafanya tukio la kwenda kuutupa kesho usiku wakiona shwari.
"Huyo atakuwa ni mlinzi anazunguka huko nje!" Alisema Joana.
Mara mlango unagongwa. Tambalizi la uwoga linakamata chumba. wanatazamana kama mizimu.
Damu ilikuwa chini kwenye zulia, na mwili wa Moa ulikuwa bado haujanyanyuliwa kupelekwa kabatini.
Bahati kwao, mgonga mlango hakungoja afunguliwe, akapaza sauti:
"Ni muda wa kulala, tafadhali zimeni taa."
Kisha vishindo vya miguu vikasikika vikienda mbali. Wakashusha pumzi ndefu. Haraka wakaubeba mwili wa Moa na kuutia kabatini.
Wakafunga.
Wakaligeuza na zulia chini juu, juu chini, kisha wakaketi kitandani. Usingizi ulikuwa hauji kila mtu akibanwa na maswali kichwani. Kulala na maiti ndani ya kabati si kitu kirahisi.
Kila mmoja alikuwa anahofia na kujiuliza kuhusu kesho yake. Joana akajutia alichokifanya akishangaa na kujiuliza ilikuwaje akajitia matatizoni kiasi hicho. Basi wakajikuta hawana raha wala amani.
Muda ukasonga zaidi mpaka saa kumi na moja. Lisa alikuwa amebanwa na usingizi vibaya mno akaegesha kichwa chake kitandani akilala kana kwamba yupo vitani.
Joana yeye alikuwa ameketi vilevile ila akiwa anapiga 'magoli ya vichwa', macho yalikuwa yanafumba kwa lazima, kichwa kikidondoka na kusimama.
Katika muda huo huo, Joana akashtuliwa kwa kusikia sauti kabatini! Mlango wa kabati ulikuwa unagongwa na sauti ya mtu akinguruma.
Haraka akamshtua Lisa na kumwonyeshea kidole kabatini.
"Moa mzima!"
Kabla Lisa hajasema jambo, Joana akakimbilia kabatini na kufungua. Moa akatoka akiwa hoi. Alikuwa ameshikilia kichwa akikunja sura kwa kulalama maumivu.
"Moa, mzima!" Joana alimpapasa papasa Moa akiwa haamini. Moa hakusema jambo, akaketi kitandani bado akishikilia kichwa chake na kulalama.
Alikuwa anasikia maumivu makali.
"Nisamehe Moa, haikuwa dhamira yangu," Joana akajitetea.
"Haikuwa dhamira yako nini?" Moa akauliza. Hakuonekana kama anajua kilichotokea. Lisa akambinya mkono Joana kumwashiria anyamaze.
"Ni saa ngapi sasa?" Moa akauliza.
"Saa kumi na moja na robo," Lisa akajibu. Moa akakurupuka kusimama.
"Inabidi niende!"
"Uende wapi?" Joana akawahi kuuliza.
"Inabidi niende!" Moa akarudia kauli yake pasipo kujibu. hakumngoja tena mtu aongee, akaufuata mlango upesi, akaufungua na kutimka!
Joana akafunga mlango kwa ufunguo haraka, kisha akatulia kwanza hapo mlangoni kutega kama atasikia lolote huko. baada ya kama dakika mbili, akarejea kitandani kumkuta Lisa aliyekuwa ameketi kitako.
"Joana, Moa siyo binadamu," akasema Lisa kwa macho ya kujiamini.
"Kwanini wasema hivyo?"
"Moa hakuwa anapumua!" Lisa akalipuka.
"Kwa akili zangu nilipima pumzi zake, sikuhisi kitu!"
"Pengine alikuwa anapumua kwa mbali."
"Hapana! Hapana. Alikuwa hapumui kabisa. nimemtazama pia hata hapa alipokuwepo kitandani, sikuona kifua chake kikisinyaa na kutanuka. Naapa kwa Mungu wangu!"
Sasa ile hoja kwamba Moa ni jini ikaanza kuleta mashiko kichwani mwa Joana.
"Unajua Moa anakaa wapi?" Lisa akauliza.
"Sijui!" Moa akatikisa kichwa.
"Kuna kitu, Joana. Ni wazi kuna kitu hapa. We unahisi atakuwa anaishi wapi?"
"Msituni!" haraka likaja jibu kichwani mwa Joana.
Kama alihaha kutafuta makazi ya Moa akayakosa, basi Moa ndiye yule anayeishi msituni. Ndiye yeye muuaji. Ndiye yeye anayegeuka kuwa kiumbe cha ajabu! Aliyakumbuka maneno ya yule mwanafunzi aliyekuwa anawasimulia wenzake.
"Moa anakuja hapa saa nane za usiku tu. Anaonekana nyakati za usiku peke yake, tena akiwa mwenye nguvu. Si bure aliondoka haraka punde alipojua ni saa kumi na moja, maana jua linakaribia kuchomoza!"
Maneno hayo ya Lisa yalipenya vizuri masikioni mwa Joana na kujenga nyumba kuu ya hoja. yalikuwa na mantiki ndaniye. Yalimfumbua Joana macho ambayo alikuwa ameyafumba kwa kutokujua ama kwa kujua kwasababu tu ya upofu wa mapenzi.
"Naondoka, Lisa," akasema Joana. "Siwezi nikakaa tena hapa. Tafadhali naomba uniwie radhi nakuacha peke yako. Ila ni kwa mema."
"Naelewa, Joana. Nenda," akasema Lisa. Hakuona tena sababu ya kuzozana na Joana. Alimwonea huruma rafiki yake, akamshika bega na kumvuta kumkumbatia.
"Yote yatapita Joana, hata na hili."
Joana akaangua kilio. Alipanga vitu vyake ndani ya begi dogo tu la mgongoni maana hakutaka yeyote ajue kama anaondoka, akavalia nguoze na kumwaga Lisa.
"Tutaonana pale majira yatakapofika."
Uzuri alishakata tiketi jana yake kwa kupitia mtandao, hivyo hakupata shida. Alifika uwanja wa ndege akajipaki chomboni na kuondoka Ujerumani kwenda kwao Ubelgiji moja kwa moja.
Alijisema kifuani anataka kusahau yote ya huko alipotoka akaanze maisha mapya.
Lakini utaanzaje mapya ukiwa umeyabebelea ya zamani? Shingoni mwake bado alikuwa amebebelea mkufu aliomkabidhi Moa.
Mkufu huo alikuwa anarudi nao nyumbani. Alikuwa anaupeleka nyumbani, je utamwacha salama ilhali Moa alisema ilimradi ana mkufu huo na basi atakuwa naye?
Mama yake alimpokea kwa bashasha na kumpeleka mpaka nyumbani ambapo pasipo kuficha akamweleza mamaye yale aliyokumbana nayo huko chuoni.
Mama akampa moyo na kumsihi apige moyo konde, atafanya mpango apate chuo hapa hapa nyumbani awe anamuona na kumpatia nasaha.
Zikapita siku mbili akiwa nyumbani. Siku ya tatu Joana akapata habari kwa kupitia runinga. Lisa alikuwa ameuawa na mtu asiyejulikana!
NANI AMEMUUA LISA? NINI JOANA ATAFANYA? NINI MKUFU UTAFANYA?
Usikose sehemu ijayo.
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app