*ANGA LA WASHENZI – 12*
*Simulizi za series inc.*
“Pole sana, Mudy, ndiyo boss huyo!” alisema Sara akitikisa kichwa na kutabasamu. Mudy akasonya. Alikuwa anatazama mbele aelekeapo. Mkono wake wa kushoto akiwa ameketi Sara, na Sasha amekaa nyuma peke yake. Ni ndani ya Rav4 nyeupe.
Mudy akatikisa kichwa na kutahamaki:
“Mpumbavu kweli yule. Sasa alikuwa analalamika nini kuhusu polisi kama hataki tuchangie mawazo?”
Sara na Sasha wakaangua kicheko.
“Sasa na hivi Bite amefariki, yule mzee si ndo’ atatupelekesha mpaka basi!” Sasha akapayuka.
“Nakwambia!” Sara akadakia. “Tutapelekwa kama gari bovu maana mzee yule hataki kushauriwa wala nini!”
“Tatizo mkoloni sana!” Mudy akaunga mkono hoja. “Sijui ametuitia nini kwenye hicho kikao chake kama kila kitu tayari ana majibu nacho. Si angetutumia tu ujumbe!”
“Kwakweli. Lakini Mudy, ulikuwa na taarifa gani kuhusu Bite? Mbona hujawahi hata kun’tonya siku zote hizo?” Sara aliuliza.
“Tatizo mambo mengi,” Mudy akajibu. “Huwezi kuamini nilikuwa nimesahau kabisa mpaka pale niliposikia tena kuhusu Bite pale kwenye kikao.”
“Tuambie basi nasi tujue,” Sasha akashupaza masikio, Mudy akatabasamu.
“Mnapenda sana umbea na nyie.”
“Tuambie bana, Mudy,” Sara naye akashadadia. “We hujui umbea kwa mwanamke ni sunna!”
Kabla Mudy hajasema neno, hamaki dereva bodaboda akakatiza upesi mbele yake! Alijitahidi kukwepa bodaboda kwa kupeleka gari kando ambapo napo huko kulikuwa kuna gari iliyokuwa inakuja nyuma kwa kasi, hivyo akaishia kubamizwa ubavuni na kusababisha tafrani barabarani!
Sara na Sasha walipiga kelele kali za hofu. Mudy alifanikiwa kulimudu gari akilipakia pembezoni mwa barabara.
“Shit!” Akalaani akisaga meno. Dereva bodaboda alitokomea asionekane wapi alipoelekea. Hakuna hata aliyenakili pleti namba yake.
“Ahsante, Mungu!” Sara alisema akihema kwanguvu. Vifua vyao vilikuwa vinapwita kwa hofu pana. Sasha yeye alikuwa ameishiwa nguvu kabisa.
Hawakuamini kama wametoka salama katika sekeseke hilo. Walikuwa wazima wa afya ila shepu ya mbele ya gari ikiwa imeharibika kiasi.
Punde alitokea dereva wa gari lile lililoparamiwa wakati Mudy anamkwepa bodaboda. Akaongea na Mudy kwa muda mchache kabla Mudy hajatoleshwa pesa, noti nyekundu kadhaa, dereva huyo akaondoka zake.
Hwakuhitaji trafiki polisi, waliona ni vema wakamalizana wenyewe.
“Pole sana, Mudy. Sasa?” Sara aliuliza.
“Siku yangu ishaharibika. Sina pesa yoyote hapa, yote nimetoa sababu ya yule bodaboda fala!”
“Pole sana, Mudy. Ila bora una uhai, hayo mengine ni ziada tu, na yanatafutwa.” Sasha alimfariji. Mudy akashusha pumzi ndefu.
“Tatizo gari yenyewe ilikuwa ina mafuta kiduchu, nilikuwa nimepanga nipitie sheli hapo mbele nitie mafuta, sasa pesa imeshaenda … anyway, nyie pandeni tu daladala muende, mie n’tajua cha kufanya.”
Sara na Sasha wakaondoka zao. Mudy akasema na yake kifuani: kweli wanawake si wa kuwategemea kwenye shida, hapa ningekuwa na wash’kaji zangu chap tatizo lingekuwa limeisha.
Akiwa hapo bado hajajua cha kufanya, mara Range Rover sport inatokea na kupaki kandokando yake, Kinoo anashuka na kumsalimu. Anamjulia hali na anapendekeza kumsaidia.
“Pole sana, ndiyo mambo ya barabarani hayo. Sasa inabidi uipeleke gereji ifanyiwe matengenezo.”
Mudy akaomba apelekwe kwanza ATM apate kutoa pesa kwa ajili ya mahitaji yake. Kinoo akambeba kumpeleka huko. Safari ikasindikizwa na soga ambazo Kinoo alikuwa amelenga kupatia majibu maswali yake.
“Nyumbani ni mbali sana?”
“Kiasi, naishi Mbweni.”
“Mmh … ni mbali!”
“Basi mie kwakuwa nimeshapazoea, naona si mbali sana. Ila kila mtu ninapomwambia naishi Mbweni husema ni mbali.”
Kinoo akatabasamu pasipo kuonyesha meno.
“In fact, ni mbali … Ila inabidi upunguze mawazo usije ukapata maswahibu mengine barabarani, Mudy. Mambo kama yale hutokea tu.”
Mudy hakuelewa, kabla hajapata mwanya wa kunena, Kinoo akaendelea kujazia nyama simulizi yake.
“Kiukweli Brokoli hakutakiwa kukukrash namna ile, alifanya makosa. Sikupendezwa naye kabisa. Na naanza kupata mashaka kama tutawezana naye kwenye biashara.”
Mudy akaguna na kutikisa kichwa pasipo kutia neno.
“Kama kuna watu ambao wamezaliwa kwa ajili ya biashara duniani, Bite alikuwa mmojawao. Mwanamke yule alikuwa smart sana. Anajua kuongea, kupanga na kusimamia. Alikuwa mhimili mkubwa wa kampuni yenu. Pengo lake gumu kulijaza.”
“Ni kweli,” Mudy akaunga mkono hoja. “Zaidi ya yote alikuwa anaishi vizuri sana na wafanyakazi wake, kila mtu alikuwa anampenda. Kifo chake kilitushtua mno. Ametuacha kwenye mikono migumu.”
“Kwakweli. Ni jukumu letu kuhakikisha angalau kifo chake kinaheshimiwa kwa kupata haki na kuwatia nguvuni wauaji.”
“Kivipi sasa na wakati polisi na mkurugenzi hawaeleweki? Naona kama Bite ameenda na hamna lolote litakalokuja kufanyika.”
“Wewe unataka iwe hivyo?”
“Hapana, ila sina la kufanya sasa.”
“La kufanya halikosekani Mudy. Mimi pia sitaki iwe hivyo kama wewe, sasa watu wawili ni wachache kufanya jambo?”
Mudy akasita kujibu.
“Ulisema ni Barclays?” Kinoo aliuliza. Mbele yao umbali mfupi kulikuwa kuna ATM ya Barclays. Yalikuwa ni maeneo ya Sinza, Kijiweni.
“Yah! Ni Barclays,” Mudy akalipuka kujibu. Gari likatafuta mahali pa kuegeshwa, akashuka na kwenda kwenye ATM kutoa pesa. Kinoo akampeleka tena sheli alipochukua mafuta kwa kutumia kidumu kisha akamrejesha mpaka kwenye gari lake.
Wakaagana, Kinoo akahepa zake wakipeana miadi ya kukutana karibuni wapate kutazamia namna gani ya kujadili na kufufua kesi ya Bite. Walibadilishana namba za simu kwa ajili ya mawasiliano zaidi.
***
Majira ya saa nane mchana, maeneo ya Mwenge.
Kwa kiasi kikubwa sasa Jona alikuwa amesogeza kazi zake zilizokuwa zimemtinga. Mgongo ulikuwa unamuuma kwasababu ya kuukunja kwa muda mrefu. Alijinyanyua akaunyoosha akipiga mihayo.
Alimtazama Jumanne aliyekuwa amelala kitini, akamshtua na kumuuliza:
“Vipi, hatwendi kula?”
Jumanne akatikisa kichwa na kufumba macho yake mazito mekundu.
“Unaendekeza usingizi enh?”
“Hamna … sina njaa.”
“Njaa unayo sema usingizi kwako ndiyo bora zaidi. Haya mimi naenda.”
Jumanne akatikisa kichwa akiwa amefumba macho yake.
“Sasa ukiwa umelala, utaona wateja kweli Jumanne?”
“Nikisikia tu miguu, naamka,” Jumanne akajibu akiwa bado amefumba macho. Jona akatikisa kichwa na kwenda zake kwa mama K wa mgahawani.
Kama kawaida aliketi na kutoa simu yake wakati anangojea chakula na kuanza kuiperuzi. Alizama mtandaoni Facebook, akakuta jumbe tano, nne toka kwa mwanamke yule wa Afrika ya kusini.
Alikuwa anamjulia hali na pia amemtumia picha kadhaa za bidhaa zake, nguo na mikoba akiulizia kuhusu mrejesho wa fasheni. Jona akampuuzia. Akaenda moja kwa moja kwenye ujumbe mmoja uliosalia, ulikuwa pia wa mtu mgeni – mwanaume mmoja toka Uarabuni.
Nayo akapuuzia.
Hakuona kama kuna la maana huko mtandaoni. Akakagua akaunti ya Mariam – mke wa mheshimiwa, hakupata jambo. Basi akaamua kuacha simu na kufikiri mambo yake mengine.
Chakula kikaja, akala taratibu. Alimfikiria Nade kidogo, akaachana naye. Alimfikiria Mheshimiwa, hapo akakumbuka kwamba ana miadi naye siku hiyo. La haula! Alikuwa amesahau kabisa.
Alitazama saa yake mkononi. Aliwaza ni muda gani anaweza akaenda kumuona Mheshimiwa, akaona kuna haja ya kumuuliza. Akanyanyua simu na kumpigia. Simu ikaita pasipo majibu.
Alirudia kwa mara nne lakini hakukuwa na mabadiliko. Akapata mkanganyiko.
“Pengine akikuta missed calls zangu atan’tafuta,” alihitimisha kwa kusema hivyo kabla hajaweka simu chini, akamalizia chakula.
Akalipia na kutoka ndani.
Akiwa hana hili wala lile akashika barabara kufuata njia mbili kubwa za lami apate kuvuka na kwenda ofisini. Alivuka njia ya kwanza. Akiisogelea ya pili, kuna gari moja ndogo Mark 2 nyeusi, ikahamia upande wa pili wa barabara.
Upande huu ndiyo ambao Jona alikuwepo akiangaza avuke barabara.
Baada ya kuona kuna mwanya wa magari, Jona akashusha miguu yake juu ya lami na kupiga hatua za haraka haraka avuke salama.
Ajabu ile Mark 2, upesi nayo ikahama upande, ila sasa ikiwa imeongeza kasi maradufu! Mlio wake mkali uliokuwa unanguruma ulimshtua Jona, akarusha macho yake kutazama.
Hatua kama tano tu mbele yake, gari hilo, Mark 2, lilikuwa linakuja kwa kasi kubwa. Kwa mahesabu tu ya haraka ni kwamba asingeweza kumaliza barabara kwa kasi ya hatua zake.
Haraka aliwaza. Akarusha hatua zake kukimbia, ila napo hakuweza kumaliza kuvuka, gari lilikuwa tayari limeshamfikia karibu mno kumpindua na kumvunjavunja.
Hapo sasa ikabidia atumie ujuzi wake kujiokoa maisha. Kwa kutumia mguu wake mmoja akajirusha juu, kufumba na kufumbua, mgongo wake ukatua kwenye bodi la gari, akabiringita mara mbili kabla hajamwagikia kando gari likipita!
Alitua akiweka mkono wa kulia chini, mguu wa kushoto ukinyookea nyuma na wa kulia ukiwa umejisimika kwa kuukunja.
Ilikuwa ni ajabu! Walioshuhudia tukio hilo waliachwa kwenye bumbuwazi. Walichozoea kukiona kwenye tamthilia walikiona mbele ya macho yao, tena kamera zikiwa hazipo.
Upesi alisimama kana kwamba hakuna lililotokea, akatafuta miwani yake aliyoiona kando na kuiokota. Ilikuwa imevunjika kioo kimoja na fremu zake zikiwa legelege. Akaikunja na kuiweka mfukoni, akaenda zake ofisini.
Watu walikuwa wanamtazama, wengine wakidhani pengine ameumia pasipo yeye mwenyewe kujua. Aliwaambia yu salama akizidisha hatua apotee hapo.
“Upo sawa, Jona?” Jumanne alimpokea kwa maswali.
“Nipo sawa, usijali J,” Jona akajibu akiketi kitako kwenye kiti. Akachomoa miwani yake mfukoni na kuitazama.
Jumanne alikuwa anamkagua kwa kumuangaza huku na kule kama ataambulia kuona jeraha. Macho yake yalionyesha bado yupo kwenye bumbuwazi la kutoamini kilichotokea.
Kabla Jona hajaanza kuwaza kuhusu lile gari, alikuwa anawaza kuhusu miwani yake kwanza. Alijua fika yeye pasipo miwani ni nusura kipofu. Miwani yake ndiyo macho yake, sasa itakuwaje pasipo nayo?
Ataweza pambana kwenye hii vita akiwa haoni? Alijikuta anajiuliza.
*NANI ALIYEKUWA ANATAKA KUMGONGA JONA?*
*NINI JONA ATAFANYA NA NUSURA UPOFU WAKE?*
*KINOO ATAFANIKIWA KUPATA NINI KWA MUDY?*
*MWANAMKE WA AFRIKA YA KUSINI NI NANI?*