*JOANA ANAONA KITU USIKU --- 10*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Usiku usingizi haukuja, aliwaza, je atoroke? Ajiue? Au afanye nini?
Usiku ukazidi kusonga na kusonga. Kwenye majira ya saa nane, mlango ukagongwa. Akashtuka na kutazama.
ENDELEA...
Alimtazama Lisa akamuona amelala hajitambui. Akautazama mlango akijiuliza maswali kifuani. Ni nani huyo? Moa?
Akaamua kunyamaza. Hakutaka kuitikia hodi hiyo.
"Kama ni Moa nilishamwambia asije tena muda huu!"
Hodi ikaendelea kugonga pasipo kukoma, mwishowe Lisa akaamka.
"Joana, nani huyo muda huu?" Akauliza kwa sauti yenye ulevi wa usingizi.
"Sijui!" Joana akajibu, bado alikuwa anatazama mlangoni.
"Umeuliza lakini?"
"Sijataka hata kuuliza."
"Sasa atapiga hodi mpaka lini?"
Joana kimya. Lisa akapaza sauti yake:
"Nanii?"
"Moa!" Sauti ikajibu huko nje.
"Ni Moa!" Lisa akatahamaki akimtazama Joana. Joana alikuwa ametulia kana kwamba hajasikia.
"Kamfungulie, la sivyo atakamatwa hapo nje na wewe utakuwa matatani!" Akasihi Lisa. Basi Joana akanyanyuka na kwenda mlangoni.
Akafungua mlango, Moa akazama ndani upesi.
"Unataka nini muda huu?" Lilikuwa swali la kwanza la Joana.
Hakutaka kabisa kumuelewa Moa pasipo kujali namna gani alivyokuwa anajitetea. Alikuwa ameghafirika na kumchoka Moa kwa matendo yake yasiyoeleweka.
"Unaishi wapi? - kwanini unanijia saa nane za usiku?" Yalikuwa maswali ambayo Moa alishindwa kuyajibu.
Pasipo kujali ilikuwa ni majira ya usiku, Joana alijikuta anapaza sauti kufoka na kufoka. Lisa akajaribu kumtuliza pasipo mafanikio.
"Moa, nimechoka. Na tafadhali naomba kila mtu aende na njia yake!"
Kabla Moa hajasema jambo wakasikia hodi mlangoni.
"Mlinzi hapa, kuna shida gani humo ndani?" Ilikuwa sauti ya kike.
Joana na wenzake wakatahamaki. Moa akikutwa humo ndani itakuwa kazi si kidogo, haraka wakashauriana wamfiche ndani ya kabati.
Wakafanya hivyo kisha mlango ukafunguliwa.
"Kuna nini humo ndani?"
"Samahani, tulikwaruzana kidogo," akajibu Joana akijitahidi kutabasamu.
Mlinzi akatazama ndani, akamuona Lisa akiwa ameketi kitandani.
"Kama vile nilisikia sauti ya kiume."
"Hapana! Itakuwa umesikia vibaya tu."
Mlinzi akaingia ndani kuhakikisha. Kwakuwa alikuwa mwanamke basi hakuwa na pingamizi kuwandawanda chumbani humo.
Aliangaza asione lolote la kutilia mashaka.
"Bweni zima lilikuwa limetawaliwa na kelele zenu, hamjui muda huu ni usiku sana?" Mlinzi aliwaka.
"Samahani, tunaahidi haitajirudia tena," akasema Joana.
Mlinzi akawatazama tena kabla hajaondoka zake.
Wakamtoa Moa kabatini.
"Sasa tunafanyaje Joana?" Akauliza Lisa.
"Huoni tukimtoa Moa sasa hivi atakamatwa huko nje?"
Joana hakujibu kitu. Akamtazama Moa na kumwambia:
"Toka chumbani kwangu, usirudi tena hapa!" Kisha akaufungua mlango na kusontea nje.
"Nakupenda, Joana. Na sitaacha ku ..."
"Nenda nje!" Joana hakutaka maelezo. Macho yake yalikuwa mekundu, na pua pia.
Moa akautazama mkufu wa Joana kifuani. Akatabasamu na kwenda zake.
"Ilimradi una huo mkufu kifuani, basi daima utakuwa nami," Moa alisema kifuani akiyoyoma.
Ingali walinzi walikuwa wametapakaa huko nje tangu mauaji yatokee, hakuna hata mmoja aliyemuona Moa.
Alikatiza kwa amani akielekea misituni. Alikwepa taa zote akienenda kwenye njia ya giza.
Kadiri alivyokuwa anazama ndani ya msitu akawa anabadilika umbo, sura na mwendo. Alikuwa anatisha asieleweke kama ni binadamu, kigagula ama kibwengo.
Hakuwa kiumbe chenye taswira ya Moa tena, bali mnyama ama jitu!
Kabla hajapotelea humo msituni, mjumbe mmoja wa ulinzi shirikishi alimuona, akapaza sauti:
"Hey! Unaenda wapi?"
Mlinzi huyo shirikishi alikuwa amebebelea kurunzi na bunduki kubwa.
Kile kiumbe kikamtazama. Mlinzi alipokimulika akastaajabu, hakukielewa! Kilikuwa ni kama kivuli kikubwa kilichoganda.
Ni macho tu ndiyo yalibakia wakati mwili mzima ukiwa mweusi ti na umbo la ujiuji.
La haula! Mlinzi akajikuta anaishiwa nguvu baada ya kuona kiumbe hicho chaja kwa kasi kumfuata.
Haraka alichukua filimbi iliyokuwa inaning'inia kifuani mwake, akapuliza kwanguvu akikimbia.
Hakupata hata wazo la kutumia silaha yake. Pengine aliona atachelewa ama basi haitasaidia lolote.
Alikimbia haraka mno, lakini kile kiumbe kikawa kinamkaribia kwa kasi mno hatua kwa hatua!
Ilikuwa bayana mlinzi asingefika kwenye makazi ya watu kabla hajatiwa nguvuni. Alishakaribiwa kiasi cha kutosha!
Akaanguka chini. Sasa mchezo kwake ukawa umekwisha. Alimtazama kiumbe kilichokuwa kinamkimbiza akahisi hofu kubwa ndani yake.
Haraka akateka bunduki yake na kuanza kufyatua kwa fujo. Hazikusaidia. Ajabu kile kiumbe kikaanza kummeza!
Si kwa mdomo la hasha bali kwa mwili. Kilikuwa kinamsogelea zaidi mlinzi, miguu ya mlinzi ikawa inapotelea ndani ya mwili wa kiumbe isijulikane wapi ilikuwa inaelekea.
Ni kana kwamba alikuwa anazama ndani ya maji!
Katika kuhangaika, mlinzi akateka kurunzi yake na kummulika kiumbe usoni. Kile kiumbe kikapagawa. Kikapiga kelele kali kikijitahidi kujikinga.
Hiyo ikawa salama ya mlinzi.
Alimmulika zaidi na zaidi akijitahidi kukwamua miguu yake toka kwenye tope la mwili wa kiumbe.
Akafanikiwa.
Kiumbe kikashindwa kustahimili zaidi mwanga wa kurunzi, haraka kikapotelea msituni kwa kasi! Punde walinzi wengine, watatu kwa idadi, wakatokea na kumkuta mwenzao akiwa chini.
Wakamuuliza nini kimemkumba, akawaelezea. Wakamnyanyua na kumpeleka mahali salama.
"Ulimuona ametokea wapi?"
"Hapana! Nilimuona tu akielekea msituni."
"Inawezekana akawa ndiye muuaji?"
"Sijui! Hakuwa hata na miguu, uso wala umbo la binadamu."
Taarifa zikafikishwa polisi, mapema ya saa kumi na moja polisi wakafika wakiongozwa na inspekta Westgate.
Wakapekua eneo zima la tukio.
"Inaweza ikawa ndiye muuaji," akasema inspekta. "Alama za viatu vilivyopatikana hapa ndivyo vilevile vilivyopatikana eneo la mauaji ya mlinzi."
Basi ikatolewa amri ya kusakwa pori zima. Polisi zaidi wakaongezeka wakiwa na kikosi cha mbwa.
Wakasaka pori lote, lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba mia mbili hamsini. Walimaliza msako wakitumia muda wa masaa sita, hawakufanikiwa kupata mtu.
Ila wakakuta mifupa ya binaadamu. Waliikusanya mifupa hiyo kwa ajili ya upelelezi zaidi.
Mojawapo ya mifupa ilionyesha mhanga hakuwa ameuawa kwa muda mrefu. Bado mifupa yake ilikuwa na utelezi na mabaki ya damu.
Ila kabla ya polisi hao kuondoka, inspekta akamchukua Lisa, mkazi mwenza wa Joana. Alimwambia ana maswali kadhaa anayotaka kuyapata majibu toka kwake.
Lisa alikuwa peke yake chumbani wakati alipokuja kuchukuliwa. Ila alipotiwa ndani ya gari la polisi, Joana alijitokeza na kushuhudia tukio hilo.
Alipata mashaka sana. Hakuna yeyote anayejua siri yake na Moa zaidi ya Lisa. Je, ataenda kusema?
*Usikose sehemu ijayo.*
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app