Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

ANGA LA WASHENZI --- 09*

*Simulizi za series*



Fǎnzhèng wǒ yào tā sǐ!" (Nataka afe kwa njia yoyote ile!) Mwanaume mezani akasisitizia.

Mwanaume ndani ya suti akaitikia tena kwa kutikisa kichwa.
.
.
.
"Shì de xiānshēng!" (Ndio, mkuu!)
.
.
.
Haraka akatoka ndani ya chumba akiwa haamini kama ametoka na pumzi yake. Alihema kwanguvu jasho likimchuruza.
.
.
.
ENDELEA…
.
.
.
Aliendea gari lake akajiweka na kutoka ndani ya eneo hilo mpaka kwenye bangaloo iliyokuwa umbali wa kama kilomita tatu toka kwenye yale makazi alipofikishia taarifa.

Huko akakutana na wenzake wanne ambao alijumuika nao kwenye kunywa ulabu na kuvuta shisha iliyopo katikati ikiwa imezungukwa na kochi kubwa rangi nyekundu lililokuwa limejikunja kutengeneza umbo la ‘c’. Mwanaume mmoja alikuwa mwenye asili ya Uchina; nywele nyeusi, macho madogo na umbo dogo pia, alikuwa anajulikana kwa jina la Lee. Alikuwa mchangamfu na akiongea lugha ya Kiswahili kwa ufasaha kasoro tu lafudhi.
Wengine watatu walikuwa weusi ila wenye maumbo makubwa. Mmoja aliyekuwa amenyoa panki, pia akiwa na ndevu za duara, alikuwa anaitwa Mombo. Macho yake yalikuwa makubwa na sauti yake nzito.

Mwingine alikuwa ana nywele hafifu kichwani, vichengachenga vya ndevu vya hapa na pale kidevuni. Mdomo wake ulikuwa mpana, sauti yake ikikwaruza kana kwamba amekula chokaa. Jina lake Devi.

Wa mwisho yeye hakuwa na ndevu bali afro kubwa nyeusi ti! Alikuwa mwembamba mwenye macho mekundu malegevu. Mdomo wake mkavu mweusi kama kunguru. Aliitwa Nigaa. Alikuwa ndiye anayeshikilia bomba la shisha mara nyingi kuliko wenzake.
Walipeana salamu kwa kugusanisha mabega yao kabla mwanaume huyu aliyevalia suti nyeusi kuketi na kuanza kuwapasha wenzake habari namna mambo yalivyotukia. Kwenye haya maongezi, alitambulishwa kwa jina la Bigo.
.
.
“Una kazi nyepesi sana, Bigo,” akasema Devi na sauti yake inayotesa masikio. “Yani unahangaika na mchoraji?! Raha iliyoje. Si unammaliza ndani ya sekunde moja tu!”
Wenzake wakamuunga mkono.
.
.
“Yani kama ungeuawa kwasababu ya kushindwa kumuua mchoraji, kingekuwa ni kifo cha kizembe sana. Au una mpango wa kwenda mbinguni, Bigo?” Alisema Nigaa. Lee akaangua kicheko kikali wakati wenzake wakiishia kutabasamu.

Mchina huyu ungeweza kumdhania kama mtu mpole wa pendo, na asiye na tatizo na watu. Mkarimu, mtulivu na mwenye kupenda kufurahi. Ila kiuhalisia, hayo yote yangekuwa uongo kupitiliza.

Mwanaume huyu mwenye asili ya huko mashariki ya mbali mwa dunia, alikuwa ni miongoni mwa watu wauaji wakubwa kabisa kupata kutokea duniani. Alikuwa mkatili na mwenye upungufu wa huruma mwilini pindi awapo eneo la kazi.

Si tu kwa hapa Tanzania, bali hata huko kwao Uchina. Alishaua watu wengi kiasi kwamba hakumbuki tena idadi. Anaweza akamuua mtu lisaa limoja nyuma kisha akasahau hata uso wake!

Miaka ishirini na mitano huko nyuma, mchina huyu aliokotwa akiwa mdogo kabisa katikati ya jiji la Hongkong akiwa anazurura, hana makazi. Akalelewa katika familia ya Wu akichangamana na wenzake ambao nao pia waliokotwa ama kutekwa maeneo mbalimbali ya Uchina.
Takribani walikuwa mia mbili, wavulana kwa wasichana. Walihudumiwa vema kwa chakula na sehemu za kupumzikia. Ila walikuwa wanapewa mafunzo ya kupambana, mafunzo ya kufa ama kupona.

Walifundishwa namna ya kuua, na wakapandikiziwa roho mbaya ya unyama. Walifundwa kutokujali wala kutokuwa na rafiki. Ilipogundulikana mtoto mmoja ana urafiki na mwingine, basi alijaribiwa kwa kupewa pambano apambane na mwenzake mpaka pale kifo kitakapo watenganisha.

Japokuwa walikula na kulala mahali pazuri, mazoezi haya yaliwafanya wawe wapweke kwa muda mwingi. Kutokuwa na furaha, wala amani. Ila kwa upande wa familia ya Wu, hiyo ilikuwa sherehe kubwa.
Lengo lao lilikuwa linatimia. Walifanikiwa kuwaandaa watoto waliokuja kurithi mikoba ya wauaji waliosambaa ulimwenguni kote wakifanya hili ama lile kwa manufaa ya familia ya Wu.

Miongoni mwa watoto mia mbili, ni watoto thelathini tu ndiyo ambao walifanikiwa kukua na kuungana na jeshi, wengine wakienda na maji! Miongoni mwa watoto hao waliofanikiwa, alikuwa ni huyu Lee Sun. Mtambo wa mauti wa familia ya Wu.

Kabla hata hajaenda kwenye uwanja wa mapambano, huko ‘duniani’, alikuwa tayari ameshanyofoa uhai wa binadamu kumi na tano. Wote wakiwa watoto wenzake ndani ya mafunzo.

Kazi yake ya kwanza ilikuwa ndani ya jiji la Hongkong, baadaye Bangkok, Thailand na kisha Rabat, Morocco. Kote huko akifanya kazi moja tu, kuua pasipo mjadala. Alikuwa anakabidhiwa picha ya mlengwa na makazi yake, kisha yeye anaenda kumaliza kazi.
Baada ya mafanikio ya shughuli zake hizo, ndipo akahamishiwa Dar es salaam kuipa nguvu makao yao mapya yaliyoanza kumea ndani ya Afrika ya mashariki.
.
.
.
"Si kwamba nimeshindwa kumuua, ila majira ya kumuua. Unadhani ningemmaliza pale mgahawani polisi alipokuwapo ingekuaje?” aliuliza Bigo, kisha akaendeleza soga: “Hata tuseme ningemmaliza na polisi pia, huoni kama ingekuwa msala mkubwa – kuchoma utambi mapema hivyo?”
.
.
Lee akatikisa kichwa.
.
.
“Ndiyo maana umeachwa hai la sivyo ungeshakuwa historia sasa, Bigo. Ila ndani ya siku hizo mbili hakikisha unamaliza hiyo kazi. Kama utakwama, usisite kututaarifu. Twaweza kutoa msaada.”
.
.
“Msijali,” Bigo akasema akitikisa kichwa. “Ni kazi ya mkono mmoja tu, sidhani kama nahitaji mkono mwingine wa ziada.”
.
.
.
***
.
.
.
Kwa mujibu wa saa ya mkononi ya Jona, ilikuwa ni saa moja na dakika nane jioni. Kwa kiasi kikubwa alikuwa amesogeza kazi zake ‘lukuki’ na sasa alikuwa akifunga ajirudishe nyumbani kwa ajili ya mapumziko.

Jumanne alikuwa tayari ameshaondoka, hivyo alikuwa mwenyewe. Kwenye mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea mfuko mweupe wa Rambo wenye chapa nyekundu, ndani ukiwa umejazwa na baadhi ya vitu.

Alipanda bodaboda, kama ilivyo kawaida yake mara kwa mara, akaenda moja kwa moja mpaka kwenye bar karibu na makazi yake alipojiweka na kuagiza kinywaji laini kisicho na kilevi.

Akiwa anangojea kinywaji, alichomoa simu yake mfukoni akaitazama. Kulikuwa kuna ujumbe kwenye mtandao wa Facebook toka kwa mwanamke fulani ambaye hakumtambua kwa haraka.
Mwanamke huyo alikuwa anampa salamu akiambatanisha na vimdoli vitatu vinavyotabasamu.
Kabla hajamjibu mwanamke huyo, akaenda kutembelea kwanza ‘profile’ yake. Kwa mujibu wa maelezo aliyoyakuta huko, mwanamke huyu alikuwa ni raia wa Afrika ya kusini. Mjasiriamali anayejihusisha na mauzo ya nguo akimiliki maduka kadhaa ndani ya jiji la Pretoria.

Hakufanikiwa kuona uso wake kwakuwa hakuwa ametuma picha yake hata moja, bali bidhaa zake anazoziuza. Kilichomfanya akajua kuwa ni mwanamke ni jina la mtu huyo na uchaguzi wa jinsia aliouteua kwenye ‘setting’ yake, ‘Female’. Akamjibu salamu yake kwa ufupi, kisha akaacha aone ni nini kitatokea. Punde kinywaji nacho kikaja akakinyaka na kuanza kunywa. Akaagiza pia na chakula ale hapo hapo ili amalize kila kitu kabla hajaenda zake nyumbani ambapo alilenga atajipumzisha moja kwa moja kutokana na uchovu aliokuwa nao.

Alikula na kunywa akisahau kabisa kuhusu simu. Alipomaliza akalipia chakula na kwenda zake nyumbani. Alioga kisha akaendea jokofu kuchomoa chupa kubwa ya kilevi na kuketi kitandani.
Hakuwa na mawazo mazito kichwani, alijitahidi kujipuuzisha. Alikunywa kileo chake taratibu macho yake yakiwanda wanda ndani ya nyumba yake pweke.

Haikupita muda mrefu, simu yake ikaita. Alikuwa ni mheshimiwa. Alisita kupokea akijiuliza. Ila akaamua kukata shauri na kuiweka sikioni.
.
.
“Kesho, majira ya saa tano asubuhi naomba tuonane nyumbani kwangu,” sauti ya mheshimiwa ilinguruma. Kabla Jona hajaongea, simu ikakata.
Jona akajikuta anatabasamu akitikisa kichwa chake. Akanywa mafundo matatu, kisha akajilaza kitandani.
.
.
“Mheshimiwa, bila shaka bado hatujafahamiana vizuri,” aliongea mwenyewe. “Tumeshayavulia nguo haya maji, hatuna budi kuyakoga.”
.
.
Kama maneno hayo angeliyasikia bwana Eliakimu Mtaja, basi bila shaka angezidi kuchochea hofu.
Kwa muda huu tu, akiwa ndani ya sebule yake mkononi akiwa amebebelea glasi yenye kiywaji chekundu, alikuwa tayari amepaliwa na mashaka.

Mkono wake uliobebelea kinywaji ulikuwa unatetemeka. Alikuwa ameubinua mdomowe kama upinde wa mshale. Uso wake ulikuwa mweusi, macho yake yakizama ndani ya fikira.

Pembeni yake alikuwa ameketi Nade akiwa amekunja nne, mapaja yake meupe yakiachwa wazi na kimini cheusi alichokuwa amevaa. Naye mkononi alikuwa amebebelea glasi kubwa ya kinywaji.

Mazingira yalikuwa tulivu.
Watu hawa wawili walikuwa wametekwa na mawazo. Walikuwa kimya ila sura zikiwa nzito. Kwa muda kidogo, tendo lililokuwa linafanyika ni kupeleka tu glasi ya kinywaji mdomoni kabla Nade hajauvunja ukimya kwa kuuliza:
.
.
“Kwahiyo sasa? – Kuna haja ya kummaliza?”
.
.
Mheshimiwa akashusha pumzi ndefu. Akanywa kwanza fundo moja.
.
.
“Hapana, Nade. Si haraka kiasi hiko.”
.
.
“Vipi sasa kama akiligundua ya chini ya zulia? Huoni tutakuwa tumeshachelewa?” Nade akauliza.
.
.
“Hapana,” mheshimiwa akajibu akitikisa kichwa. “Jona ni mtu mdogo sana kumhofia. Ataenda kush’taki wapi?”
“Mheshimiwa, ishu si wapi atashtakia, ila mambo yetu ya siri yataanza kuwa wazi. Inaweza ikakamata atensheni ya watu na mwishowe chombo kikaenda mrama. Tone moja la chumvi laweza kuharibu chakula.”
.
.
Mheshimiwa akanywa kwanza kinywaji. Fundo moja tena.
“Ila Nade, tukimmaliza sasa hivi, hatutampata Mariam. Tutampatia wapi yule mwanamke mzandiki? Mimi namhofia sana Mariam kuliko Jona. Mariam anajua vyetu vingi vya uvunguni.
Kadiri anavyoendelea kuwa mbali ya mikono yetu, ndivyo mambo yanavyozidi kuchacha. Mariam anajua mikataba, nyaraka, mipango, watu na mpaka washirika wangu.

Huko alipo hatujui anafanya nini, na yupo na nani. Nilitamani sana kumuagiza Jona ammalize mwanamke huyu pindi tu atakapomuona, ila niliona litazalisha maswali kichwani mwake.
Nakosa usingizi kumuwaza mwanamke huyu. Sina raha kabisa! Lengo langu la kwanza ni kumpata huyu mwanamke. Kuhusu Jona, sijali. Nataka tu kumtumia kwasababu najua ana uwezo wa kumpata huyo mwanamke.

Punde tu akapompata, ummalize upesi kabla hajaanza fyoko fyoko yoyote!”
.
.
“Mheshimiwa,” Nade akaita. “N’tajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu, ila inabidi sasa niwe namfuatilia Jona kwa siri maana naona hatakuwa na mpango wa kunishirikisha kwenye mambo yake tangu aone namfuatilia kupitiliza.”
.
.
“Hakikisha haumtoi machoni mwako, sawa?”
.
.
“Bila shaka.”
.
.
Dakika tano mbele, mlango unagongwa. Mheshimiwa anatabasamu kidogo, ana habari na ujio huu. Anampa Nade ishara ya kichwa, Nade ananyanyuka na kuuendea mlango.
Mgeni alikuwa Miranda. Alikuwa amevalia koti dogo jeusi la ngozi, suruali ya jeans ya kumbana na viatu rangi ya kahawia vyenye visigino virefu.
.
.
.
.
*MIRANDA AMEKUJA KUFANYA NINI HAPA?*
.
.
*ANA MAHUSIANO GANI NA MHESHIMIWA?*
.
.
*NINI MHESHIMIWA NA NADE WANAFICHA?*
.
.
.
*JONA ANAFUATILIWA NA WATU WANGAPI SASA?*
.
.
.
*NANI ATAKUWA WA KWANZA KUZAMA KWENYE RADA ZAKE? – WAKINA MIRANDA, BIGO AMA NADE?*
 
SteveMollel, heko sana kaka kwa utunzi wa riwaya kali kabisa. Ni miaka mingi toka nikutane na riwaya ya Kiswahili iliyonivutia na kunipa hamu ya kusoma na kusubiri kwa hamu kama mtoto anayesubiri peremende. Ustadi wako ni mahiri kabisa na umenikumbusha waandishi wa enzi hizo ambao nao walikuwa mahiri sana. Nakufananisha na Eddie Ganzel, unamkumbuka huyu jamaa? Pia staili yako ya kijasusi kama riwaya za mzee Elvis Musiba (RIP) na riwaya zake kama Kufa na Kupona ama Kikosi cha Kisasi na Njama. Nakupa heko na shukurani kwa kutupa burudani hii bure kabisa kaka. Una uwezo wa kuuza kitabu kaka. Nakuahidi siku yoyote nikikutana na riwaya mtunzi akiwa Steve Mollel nitatoa majasho yangu bila kinyongo. Keep it up bro. Na pia asante kutuwakilisha machalii wa Arachuga [emoji3][emoji3]
Nashukuru sana Broh! Pamoja arif! Hii kitu ni mapenzi na pia ni taaluma yangu niliyoikalia darasani.
 
JOANA ANAONA KITU USIKU --- 07

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA…
.
.
.
“Moa,” sauti ikajibu kwa nje. “Nifungulie haraka kabla sijaonekana na mlinzi.”
.
.
Joana akajikuta anatabasamu. Haraka akaweka mashine yake pembeni na kukimbilia mlangoni.
.
.
Akafungua na kuangaza, hakuona mtu!
.
.
ENDELEA…
.
.
.
Alikunja uso akiduwaa. Ila punde Moa akatokea na kumtisha. Kumbe alikuwa amejificha kwa nyuma kidogo ya jengo.
.
.
“Ungeniua ujue!” Joana akasema wakiingia ndani. Waliketi juu ya kitanda wakashikana mikono.
.
.
Jambo la kwanza kwa Joana kuulizia likawa mawasiliano finyu ya Moa hivi karibuni.
.
.
“Haupatikani, haun’tafuti. Nini shida?”
.
.
Moa akatabasamu akitazama chini.
.
.
“Simu ilipotea mpenzi. Nisamehe kwa kushindwa kupata namna.”
“Usijali,” Joana akampooza. “Naelewa kipenzi. Vipi lakini nyumbani, wanaendeleaje?”
“Wako salama, wanakusalimu.”
Joana akajibu kwa tabasamu, kisha akauliza:
“Mama alisemaje ulipompatia ile bangili?”
“Bangili?” Moa akashtuka. “Bangili gani?”
“Moa, umesahau bangili uliyochukua kwangu? Ile ambayo mama alinipa?”
.
.
Moa akatafakari, ila akamezea na tabasamu la uongo.
.
.
“Anhaa, nimekumbuka! Lakini tuachane na hayo, kuna kitu nimekuletea.”
.
.
Kabla Joana hajasema kitu, Moa akazamisha mkono wake ndani ya mfuko akachoropoa mkufu mzito wenye kidani cha pembe tatu.
Kidani hichi mithili ya almasi kilikuwa kinang’aa, na basi kikawa kinaakisi mwanga. Mkufu huu ulikuwa wa dhahabu na kwa macho tu ulikuwa unaonyesha kuwa aghali.
.
.
Joana aliufurahia, akaupokea na kuuweka shingoni.
.
.
"Imekupendeza, na kimpendezacho mtu ni chake," akasema Moa akitabasamu.
.
.
Kweli mkufu ulikuwa umempendeza Joana. Ni kama vile ametoka kuununua kwenye maduka makubwa huko Abu dhabi.
.
.
Aliupapasa kwa kiganja chake akitabasamu kwa mshangao.
.
.
Akauliza kama mkufu umetoka kwa mama ama mpenziwe ameamua kumnunulia.
.
.
"Ni pesa yangu," akajibu Moa kwa majigambo, na kuongezea: .
.
"Sitaki kuona kifua chako kikiwa kitupu tena. Muda wote uwe na mkufu huu, kama ishara ya penzi langu kwako."
Joana akatabasamu. Alishindwa kuzuia hisia zake, akadondosha chozi.
.
.
Walikaa na mpenziwe huyo wakaongea na kuteta mengi kuhusu ya mbele. Ila mapenzi yake mazito yakamfanya awe kipofu asijue udhaifu wa Moa.
.
.
Mwanaume huyo hakuwa na majibu ya kueleweka kuhusu chuo wala miadi zao. Kila mara Joana alikuwa anamkumbusha ama kumuelekeza. Pengine alidhani Moa anampima.
.
.
"Acha kuwa msahaulifu hivyo, Moa. Ulikuwa unakula nini huko nyumbani?" Joana alitania.
.
.
.
Muda ulikuwa umeenda na sasa ni saa tisa kasoro. Walisahau kabisa kwamba Moa anatakiwa kuondoka kwa kunogewa na simulizi.
Mwanaume ndani ya mabweni ya wasichana muda mpaka huo, ilikuwa hatari.
Pale Lisa alipojigeuza na kuamka akitaka kwenda maliwatoni, ndipo Joana anashtuka na kumtaka Moa aende.
.
.
"Kuwa makini na walinzi. Wakikukamata itakuwa kesi."
.
.
"Usijali, hawataweza," Moa akajibu kisha akambusu Joana na kunyanyuka kuufuata mlango. Akaufungua na kuchungulia nje.
Palikuwa salama, basi akachoropoka na kuhepaze.
.
.
Alikuwa mwangalifu mno akikwepa kila alipoona si shwari. Alidaka ngazi akajishusha chini. Alikanyaga sakafu taratibu kuepusha vishindo vya miguu.
.
.
Akafanikiwa kutoka jengoni, sasa akabakiwa na kazi ya kutoka ndani ya uzio.
.
.
Kwa kujua getini hataweza kukatiza kiurahisi, basi akazunguka nyuma ya jengo akaruke ukuta.
.
.
Ila hakufanikiwa, ghafla akajikuta akimulikwa na kurunzi kubwa.
.
.
"Simama hapo hapo!" Sauti ikamuamuru. Akatii kwa kusimama na kunyoosha mikono juu.
.
.
Punde akakaribiwa na mwanaume mtu mzima mwenye mustachi wa kahawia akivalia sare za kampunzi ya ulinzi.
.
.
Mkononi alikuwa amebebelea kirungu, ila hivi vya kisasa. Kiunoni akining'iniza pingu na mashine ya shoti ya umeme.
.
.
"Wewe nani na unafanya nini huku?" Akauliza mlinzi. Alimsogelea Moa akampapasa kumkagua.
.
.
"Naitwa Moa. Nasoma hapa."
"Unaitwa Moa, unasoma hapa!" Mlinzi akashangazwa na majibu hayo mepesi. Alitabasamu akamtazama Moa kwa kumkazia macho.
.
.
"Naomba kitambulisho chako," akasema akimwonyeshea Moa kiganja.
.
.
Moa hakuwa na kitambulisho wala nini. Zaidi hakuwa hata na taarifa kuhusu jambo lolote la chuoni.
.
.
Alichokuwa anakijua ni kozi anayosoma, jina la chuo, na chumba cha Joana tu.
.
.
Alijua fika hataweza kuchomoka kwenye maswali ya mlinzi, na pia hana sababu ya kueleweka kwanini alitoka bwenini mwa wasichana.
.
.
Lakini pia hakutaka kukamatwa, na alipanga hilo lisiwezekane kwa njia yoyote ile.
.
.
"Nimetoka kumwona rafiki yangu, kuna kitu chake muhimu nilimletea," alijitetea Moa.
.
.
"Naomba kitambulisho, kijana," mlinzi akasisitiza. Sura yake haikuwa na masikhara.
.
.
Moa akashusha mikono yake chini. Na baada ya punde damu zikamwagikia chini kisijulikane nini kiliendelea.
.
.
Miguu ya mlinzi ilikuwa inatetemeka na baada ya muda ikakoma na kutulia.
Moa akaonekana anayoyoma akikimbia, tayari akiwa ameshaacha uzio wa bweni la wasichana kwa mbali mno.
.
.
Asubuhi na mapema taarifa ikasambaa chuoni juu ya mauaji ya mlinzi. Alikutwa akiwa amechanwa koo na kitu kikali. Haikujulikana nani aliyefanya tukio hilo.
.
.
Polisi walifika pamoja na mpelelezi wakaanza mahojiano na baadhi ya wanafunzi. Hakuna mtu aliyekuwa na taarifa ya maana.
Waliamua kutazama na kamera zilizopachikwa makoridoni na baadhi ya maeneo yazungukayo bwenini.
.
.
Akaonekana mwanaume mmoja, ila hawakuweza kumtambua. Alikuwa anapita gizani kana kwamba mtu mwenye ufahamu na kamera hizo.
.
.
Kitu pekee walichokiambulia ikawa ni rangi la shati la mtu huyo ambaye walimuhisi ndiye mhusika wa mauaji.
.
.
Rangi ya njano.
.
.
"Hakuna yeyote aliyekuwa na ugeni nyakati za usiku? Au ambaye alimuona mtu mwenye shati la njano?" Inspekta aliuliza wanafunzi wakazi wa bweni.
.
.
Ila hakuna aliyetoa majibu ya ndio, basi wakaaga lakini wakiahidi upelelezi zaidi kuendelea kumbaini muuaji.
.
.
Yani siku moja tu wanafunzi wamerejea na mauaji yameanza! Hili liliwashtua sana watu, lakini likathibitisha zaidi kwamba wauaji ni wanafunzi na si wengine.
.
.
Lakini lilimpa hofu zaidi Joana ambaye alijua fika ni yeye ndiye alitembelewa na mgeni. Na zaidi zaidi, mgeni wake huyo ndiye alikuwa amevalia shati la njano!
.
.
Ina maana Moa ndiye muuaji?
Hakutaka kujipa majibu haraka kwasababu hakutaka kuamini. Alikata shauri la kumtafuta Moa ampatie majibu zaidi.
.
.
Akaenda chumbani kwa mwanaume huyo ambapo aligonga na kupokelewa na mwanaume mgeni machoni.
.
.
Alikuwa mwanaume mwenye asili ya India.
.
.
"Samahani, unaishi na Moa?"
.
.
"Hapana, simjui."
Akastaajabu. Akajaribu kuwatafuta marafiki wa Moa apate kuwauliza. Akampata mmoja punde tu alipoenda kwenye eneo fulani wanafunzi wanapokutania kwa ajili ya majadiliano.
.
.
Alikuwa ni mwanaume mrefu mpana, muingereza kwa jina la Smith. "Umeonana na Moa?" "Hapana, sijaonana naye tangu tulipokuja." "Wapi naweza nikampata. Nina shida naye sana." "Mmh sijui kwakweli. Ila kamtazame kantini ama maktaba, pengine unaweza kumbahatisha."
.
.
Alimtafuta kote lakini hakumpata. Hata kwenye simu hakupatikana. Joana akapata hofu huenda Moa ametoroka kwa kuhisi anaweza kukamatwa.
.
.
Alijikuta anamuonea huruma Moa, na kujiuliza maswali mengi.
.
.
Maswali haya yakamkosesha usingizi hata akakaa macho kwa muda mrefu akiwaza. Alijitahidi kujipumbaza kwa tamthilia lakini haikusaidia sana.
.
.
Ikiwa ni katikati ya usiku, na akiwa macho mwenyewe, anasikia tena sauti mlangoni. Sauti ya kubisha hodi.
.
.
Alishtuka kabla hajavuta pumzi kujituliza.
.
.
"Nani?" Akauliza.
.
.
"Mgeni wako," sauti ya kiume ikajibu.
.
.
Akatazama saa, saa nane na robo!
.
.
.
*NI NANI YUPO MLANGONI? NI MOA AMA MWINGINE?*
.
.
*NINI MAANA YA MKUFU AMBAO MOA AMEMPATIA JOANA?*
.
.
*NINI HATMA YA MAUZA UZA HAYA?*
.
 
*JOANA ANAONA KITU USIKU --- 08*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA…

Ikiwa ni katikati ya usiku, na akiwa macho mwenyewe, anasikia tena sauti mlangoni. Sauti ya kubisha hodi.

Alishtuka kabla hajavuta pumzi kujituliza.

"Nani?" Akauliza.

"Mgeni wako," sauti ya kiume ikajibu.

Akatazama saa, saa nane na robo!

ENDELEA…

Alipata hofu na maswali kwa pamoja. Alijiuliza aliyekuwepo mlangoni ni nani, Moa? Ama mtu mwingine? Kama ni Moa ina maana amerudi tena muda na wakati kama wa jana? Haogopi ukizingatia kile kilichotukia?

Kama si Moa, ni nani mwingine? Je ni salama kwenda kumfungulia majira hayo?

Alinyanyuka akaenda mpaka mlangoni, alijuta kwanini alikuwa wa mwisho kulala kwani asingekutana na adha kama hiyo. Alimtazama Lisa akamuona anakoroma usingizini, akamtamani.

Alipiga moyo konde, akauuliza mlango:

“Nani?”

“Ni mlinzi,” sauti ikasema toka nje.

Kidogo Joana akatua hofu. Sasa akafungua mlango lakini kwa tahadhari. Alichungulia nje akamuona mlinzi: mwanaume mrefu, mwili wa kujaa, nywele fupi nyeusi, amevalia sare, mkononi akibebelea fimbo nyeusi iliyotengenezwa kiustadi.

Kiunoni alikuwa amening’iniza pingu. Sura yake ilikuwa makini, mikono yake ameiweka nyuma ya mgongo.

“Tafadhali hakikisheni milango imefungwa, hakuna mtu yeyote anayetembea nje ya bweni wala kumuingiza mgeni yeyote wakati huu wa usiku” alisema mlinzi. Joana akatikisa kichwa kuupokea ujumbe.

“Samahani kwa usumbufu.” Mlinzi akasema kisha akaenda zake.

Alikuwa anapitia vyumba alivyokuwa anasikia sauti, ama kuona kuna mwanga kumaanisha watu bado wapo macho.

Joana alimtazama mlinzi huyo kwa muda kabla hajaingia ndani na kuufunga mlango.

Hakujua kwanini hana usingizi. Alijitahidi kujilaza lakini hakupata chochote. Baadae baadae kwenye majira ya saa tisa, akiwa kitandani anajigeuzia huku na huko, akasikia hodi tena mlangoni!

Akakurupuka kutazama.

Mlinzi amerejea? Alidhani pengine ni mawenge yake ya kuukosa usingizi basi akangoja kwanza. Punde, hodi ikajirudia. Kumbe alikuwa sahihi, alisikia hodi.

Akataka kupuuzia, ila akajiuliza:

“Hawezi akawa Moa?”

Akanyanyuka na kuusogelea mlango karibu.

“Lakini Moa aje afanye nini muda huu? Ama mlinzi?”

Alihofu.

“Nani?” akauliza kwa sauti ya chini.

“Moa!” sauti ikajibu toka nje. Akastaajabu. Kwa kuhofia Moa asije akaonekana na mlinzi ambaye alikatiza kutoa taarifa muda si mrefu, uoesi akaufungua mlango na kumruhusu aingie ndani.

“Moa, kwanini unakuja wakati huu na unajua kabisa ni hatari?” Joana aliwaka. Moa akatabasamu akiketi kitandani.

“Mbona una hofu hivyo?”

“Mbona nina hofu!” Joana akatahamaki. “We unaona ni sawa hiki unachofanya?”

“Acha hofu, mpenzi. Najua ninachofanya.”

“Kuua walinzi?” Joana akaropoka. Mara akashika mdomo wake na kumshika Moa mkono.

“Nisamehe, haikuwa dhamira yangu. Nimekwazika sana.”

“Usijali,” Moa akasema akimtazama machoni.

“Lakini Moa kwanini unakuja muda huu?”

“Labda ndiyo muda ninaohitaji kukuona zaidi,” Moa akajibu akipapasa uso wa Joana.

“Ukikamatwa na walinzi utasemaje?” Joana akauliza. Asingoje majibu, akauliza tena:

“… Moa, unahusika na kifo cha mlinzi?”

Moa akashusha pumzi ndefu.

“Sihusiki,” akajibu.

“Moa, ni wewe ndiye uliyekuwa umevaa shati la njano jana, na ulitoka huku kwangu usiku mzito, Ni nani kama si wewe?”

“Joana, ilibidi nifanye hivyo la sivyo ingekuwa kesi kubwa,” Moa akajitetea.

“Kesi kubwa kuliko ya mauaji?”

Moa akanyamaza.

“Moa, umekuwa muuaji?”

Hawakuketi na shwari, walijibizana hapa na pale kabla Moa hajataka kwenda.

Joana alikumbuka jambo, akamuuliza Moa:

“Unaishi wapi?”

“Kwani hujui ninaishi wapi?”

“Nilikuja na haukuwepo. Moa una nini lakini wewe?”

“Nakushangaa wewe!”

“Ebu, naomba uende!” Joana akasema akinyooshea mkono wake mlangoni. Alikuwa ameghafirika, uso na macho yake vilikuwa vyekundu.

Moa akaondoka.

Joana akashusha pumzi ndefu na kujirejesha kitandani. Mawazo yalikuwa yameongezeka zaidi hivyo akakosa kabisa usingizi akiwaza.

Kwanza aliwaza kama Moa atafanikiwa kutoka salama ndani ya eneo la bweni pasipo kukamatwa. Pili alikuwa anawaza namna Moa alivyobadilika. Alihisi si mzima.

Lakini hakujua wakati anazozana na Moa, Lisa alikuwa anawasikia. Alifungua macho yake kuwatazama kabla hajayafumba na kupoteza ushahidi kama aliamka.

Dakika kama ishirini mbele, Joana bado akiwa hana usingizi, anasikia tena hodi mlangoni. Hodi ilipigwa kwanguvu kiasi cha kumshtua Lisa aliyekuwa usingizini.

Ilipigwa mara tatu alafu ikakoma.

“Joana, nani huyo?” Lisa akauliza kwa sauti yenye kilevi cha usingizi. Joana akajibu kwa kupandisha mabega juu.

Akasimama na kuusogelea mlango.

“Nani?”

“Mlinzi!”

Moyo wa Joana ukapiga fundo! Alafu ukaanza kukimbia haraka.

Moa amekamatwa? Wamegundua nilikuwa na mgeni? Maswali yakapita upesi kichwani mwake. Akajikuta anahofia kufungua mlango.

Hodi ikabishwa tena kwanguvu. Joana akafungua mlango kwa mkono unaotetemeka. Akakutana na mlinzi, yule aliyekuwa anakatiza kuwapasha habari.

“Ulikuwa na mgeni?” lilikuwa swali la kwanza mlinzi kuliuliza.

Joana akatikisa kichwa pasipo kusema kitu, alikuwa ameificha mikono yake kwa kujikumbatia asionekane anavyotetemeka.

“Una uhakika?” mlinzi akauliza akimtazama Joana machoni. Joana akakwepesha macho.

“Ndio, nina uhakika,” alisema huku moyo wake ukivuma. Alihofia pengine mlinzi anaweza akasikia namna moyo wake unavyokita. Basi akaweka kiganja chake kifuani.

“Unaona hii,” Mlinzi akamuonyeshea chini, kulikuwa kuna nyayo za viatu.

“Hivi ni viatu vya kiume, madam na inaonyesha zimetokea hapa kama si kuja hapa. Unavitambua?”

“Hapana.” Joana akatikisa kichwa.

“Naweza nikaingia ndani?” Mlinzi aliuliza, Joana akatazama ndani upesi alafu akarudisha uso wake nje.

“Ndio, unaweza.”

Mlinzi akazama ndani na kutazama chini. Bahati kulikuwa kuna zulia gumu rangi ya kijani, halikuonyesha jambo.

Mlinzi akatoka zake nje.

“Nakutakia usiku mwema,” alisema kisha akaondoka. Sura yake ilikuwa inatosha kueleza namna alivyokuwa na mashaka. Joana mwenyewe alilijua hilo, mlinzi alimtilia shaka.

Aliufunga mlango akarudi kitandani.

Hakulala sasa mpaka jua linachomoza. Asubuhi ndiyo akapata usingizi, ambao ulikuja kukatishwa na hodi.

Alikuwa ni inspekta Westgate ndani ya suti yake rangi ya udongo na briefcase nyeusi mkono wake wa kulia.



JOANA ATASALIMIKA KWA INSPEKTA? JE INSPEKTA AMEKUJA KUFANYA NINI HAPO CHUMBANI KWA JOANA?

NINI HATMA YA MOA ASIYEELEWEKA?

MTU PEKEE MWENYE SIRI YA JOANA NA MOA NI LISA, ATATUNZA SIRI HIYO KIFUANI?

Usikose sehemu ijayo.
 
Weeeewwwweeeeeee [emoji91][emoji91][emoji91][emoji91][emoji2][emoji2][emoji2][emoji2][emoji2]
 
"Akiwa hewani amejifyatua,
Miranda akamsukuma, alafu
kufumba na kufumbua akajituma
hewani na kumpa teke kali
alilolituma kwa nguvu zake zote,
mwanaume akajikuta yupo chini akiugulia maumivu makali."

Safi
 
Back
Top Bottom