*ANGA LA WASHENZI II -- 53*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Kule chumbani, kizani, baada ya dakika tatu tangu gari lile litimke, Bwana Sheng alianza kugugumia. Na mara akakohoa kama mara sita kabla ya kunyamaza na eneo zima likawa kimya kana kwamba ni chini ya shimo.
Akataka kuita, ila akashindwa. Kifua kilikuwa kinambana haswa. Akaishia kuvuta kamasi.
ENDELEA
"We are eagerly waiting for your command, sir," sauti ilisikika toka garini. Punde gari likasimama na wanaume watatu wakashuka.
Gari hii lilikuwa ni ile cadilac nyeusi iliyotoka kule kwenye kiwanda kilichotelekezwa. Hivyo basi tuna kila sababu ya kuamini kuwa, wanaume hawa ndiyo wale waliomtia Sheng mikononi.
Walikuwa ni wazungu. Watu wanaoonekana wamestaarabika kabisa. Ila kwa yale matendo yao machache tulioyaona, inatosha kuwaweka kwenye kundi la wauaji maarifa.
Wauaji maarifa ni watu stadi wenye uwezo wa kupanga tukio la kuua kwa fomula za kisayansi. Yaani wakammaliza mtu na kubakishwa maswali mengi sana kwa washuhudiaji ama wapelelezi juu ya namna gani wametekeleza hilo.
Kama wewe ulivyobaki hapo ukiwa hutambui ni kwa namna gani watu hawa wamefanikiwa kumtia kimyani bwana Sheng. Na hata pengine ungeweza kushupaza shingo kuwa watekaji si hawa, maana hawakuwapo mafikirioni.
Hawa ni wauaji wasomi. Wamekaa darasani kufundishwa namna ya kuua, kuteka na hata kutesa. Kila kitu chaenda kimahesabu.
Na punde tu unapoona jambo linatokea kwa bahati, basi kwa upande wao hapo ndipo mambo yalipoenda kombo maana hawaamini kwenye bahati, bali nguvu za akili na miili yao.
Kwa jina la pamoja waliitwa 'the intellect instinct'. Na wapo watano tu kwa idadi. Nguo zao ni suti tu, na pengine ungeweza kuwatofautisha na wengine kwa ua dogo jekundu wanalolipachika kifuani upande wa kushoto.
Waliposhukia ilikuwa ni ndani ya nyumba maridadi sana. Si kubwa, bali ya wastani na rangi zake za kupendeza. Ni kama jengo la vyumba vinne ama vitatu mbali na jiko, choo bafu na stoo.
Hapa nje kwenye uwanja wa kuegeshea magari, kulikuwa kuna cadillac nyingine nyeusi imetulia.
Wanaume hawa watatu wa kizungu wakaingia ndani na kujumuika na wenzao wawili ambao walikuwa sebuleni wakihangaika na tarakilishi.
Na mmoja wao wale waliozama ndani alikuwa anaendelea kuongea na simu hata alipozama ndani na kuketi.
"Yes it does ... I think tomorrow I'll be very sure, sir ... no any reason for that ... ok, thanks."
Simu ikakata.
***
Saa tisa jioni ...
"Mara ya ngapi sasa?" Aliuliza Miranda akitazama bahari. Upepo ulikuwa unapuliza haswa na fukwe ilikuwa na watu wachache kwasababu haikuwa mwisho wa wiki.
Mwanamke huyu alikuwa amevalia tisheti nyeusi, na suruali ya jeans. Unaweza ukasema kama ilivyo ada yake. Miguuni alikuwa peku akikanyaga mchanga na kuoga maji ya bahari.
Kwa mbali kidogo, alikuwa amepaki gari lake. Ni kama umbali wa hatua ishirini na tatu au na nne hivi. Na hapa alipokuwa amesimama, kando yake alikuwepo mwanaume, Kinoo.
Kifua chake kilikuwa kimebanwa na kibodi cheusi na suruali yake ya kadeti rangi ya udongo ilikuwa imeminya mapaja yake manene.
“Kutakuwa na tatizo gani?” akauliza Miranda. Bado alikuwa anatazama bahari, na kabla Kinoo hajajibu, akaendelea kwa kusema, “Nahisi kuna tatizo hapa. Tena si dogo. Ni jambo la muda tu tatizo hili kuwa bayana. Haya matukio yaliyotukia hapa karibuni, yanafikirisha.”
“Ni kweli. Huenda kwenye ile …” Kinoo hakumaliza hiyo kauli, wakasikia sauti kubwa ya mluzi toka upande ule ilipo gari la Miranda. Wote wakatazama na kumwona Marwa huko. Akawafanyia ishara ya kuwaita.
“Nadhani nina kitu kwa ajili yenu!”
Wakajongea huko. Ndani ya gari alikuwapo Marwa pamoja na Jona. Wote walikuwa wamevalia mashati meupe na suruali za jeans, zikitofautiana rangi tu, bluu na nyeusi.
“Nadhani tulikuwa sahihi kwenye lile jambo. Ni wazi Sheng atakuwa ametekwa, ama amehifadhiwa mahali,” alisema Marwa ambaye mbele yake, juu ya dashboard, kulikuwa na tarakilishi iliyounganishwa na mtandao.
“Mmejuaje?” akauliza Miranda.
“Hapa karibuni mtandao wa wachina hawa, haujawa katika namna nzuri kiulinzi na hata kiutendaji. Nimeweza kuzama tena katika mtandao wao na kudukua taarifa ambazo zinakiri upoteaji wa bwana Sheng, lakini zaidi tumefanikiwa kupata code itakayotusaidia kumtia kimyani.
Ni hivi, kila kiongozi mkubwa wa wachina hawa ana jina lake la siri ‘code name’ ambalo humtambulisha popote pale kwenye himaya yao. Na tulipolipata hilo jina, tumefanikiwa kuli-trace kwa kuongezea baadhi ya taarifa, satellite ikatuonyesha wapi yupo!”
“Imewezekanaje katika namba hiyo?” Kinoo akauliza.
“Imewezekana kwasababu hiyo ‘code name’ si jina tu ambalo mlengwa hupewa, bali pia ni chip ambayo hushindiliwa ndani ya mwili wake ambayo itasaidia upatikanaji wake popote pale atakapopotea, ama kutokujulikana yupo wapi.”
“Kama ni hivyo, kwanini wafuasi wake hawajampata na kumwokoa mpaka sasa?” Miranda akatia shaka.
“Kwasababu taarifa ya kupotea kwa Sheng haijafiikishwa makao makuu, China,” Jona akajibu. “Ni huko makao makuu pekee ndipo kwenye ‘wing’ kubwa ya kimtandao ambayo hu-monitor wings zote za familia na koo ya Wu.”
“Mbona nyie mkaweza mkazipata taarifa hizo?” Kinoo akauliza.
“Kwasababu ni sisi,” Marwa akajibu kiwepesi na kisha akatazamana na Jona na kujikuta wanacheka.
“Ok, guys, sasa tunafanyaje?” Miranda akauliza. “Kuna haja ya kwenda huko kumkomboa Sheng?”
“Hapana,” Jona akajibu. “Endapo tukifanya hivyo, ni wazi kuna mambo fulani tutakayoyakosea majibu. Kwanza, ni kwanini chamber ya Sheng hawajatuma taarifa huko China juu ya hili? Ni kipi wamepanga kufanya? Alafu, ni nani anayehusika na utekaji huu? Na amepanga kufanya nini na Sheng?
Maana kama wangelikuwa na lengo la kumuua, wangelifanya hivyo toka pale hotelini.
Kuna mengi ya kujifunza hapa. Watu wale waliomteka Sheng, si wa kawaida. Haiwezekani kwa yale yote yaliyotukia, hakuna hata shahidi wala maelezo yoyote yaliyotolewa mpaka sasa.
Hatujui wamejipangaje. Hatujui ni wakina nani. Kumjua adui yako ni nusu na robo ya kumshinda. Inabidi tuwe wapole hapa, ama twaweza kuzamisha mguu kwenye kisima chenye maji meusi.”
“Jona!” Miranda akaita. “Twende kwa Mr Brown!”
“Are you serious?” Kinoo akawahi kuuliza akitoa macho.
“Yes, I am totally serious!” Miranda akajibu. Na kabla hajamngoja yeyote aseme jambo akakalia kiti cha dereva, akatia moto, safari ikaanza.
***
Baada ya honi ya gari kupigwa mara mbili, geti dogo linafunguliwa kidogo. Mwanaume mmoja mzungu anachungulia nje na kukagua usafiri kwa macho akitumia sekunde tatu, kisha anatupa swali,
“Who are you?”
“Mr. Brown associates!” Miranda akajibu. Yule bwana mzungu akatoka vema getini, alikuwa amebebelea bunduki kubwa mkononi.
“How can I prove that?”
“Kit-kat is the play of the cat, pat it before cut it out of its curiosity. Then hat it and give it to a big fat rat,” Miranda akasema maneno hayo upesi, basi bwana yule wa kizungu akaridhia, akafungua sasa geti kamili wageni wakazama ndani.
Baada ya dakika chache wakawa wameketi sebuleni, na kuwakarimu wageni, akawepo bwana mmoja mzungu pamoja nao. Bwana huyo ni mtu wa pili aliyekuwapo hapa, mbali na yule aliyewafungulia mlango.
“We are here to see Mr. Brown,” akasema Miranda kwa kujiamini.
“I am sorry,” Bwana yule mwenyeji akasema akitikisa kichwa, “Mr Brown is not here anymore. He was killed.”
“Killed?” Miranda akatahamaki.
“Yes, and that’s all I can tell. He was killed. So he’s no more.”
“Who killed him?”
“Madam,” bwana yule akaita akimtazama Miranda kwa macho dhalili, “I said that was all I can tell. He was killed. Enough. We are done here. The business with him is over.”
Basi Miranda na wenzake wakawa hawana lingine la kusema hapa, wakaondoka zao.
“Sheng amemuua Brown,” Miranda akasema akiwa anatazama mbele waendako.
“So waliyemteka Sheng watakuwa ni watu wa Mr Brown?” Marwa akauliza.
“Nadhani,” Miranda akajibu. Alisimamisha gari kwenye foleni, akaweka kiwiko kwenye dirisha na kucha mdomoni akifikiri.
“Ila mbona bwana yule hakutaka kusema zaidi? Ina maana hawakuamini?” Jona akauliza.
“Pengine wanaweza wakawa hawaniamini, ila pengine pia hata na wao wanaweza wakawa hawafahamu linaloendelea.”
“Unamaanisha nini kusema hivyo?” Jona akaendelea kueleza. Na kwa macho yake ya kijanja ndani ya miwani akaona mikono ya Miranda ikiwa inatetemeka kwa mbali. Na hata uso wake ukiwa umejawa na mashaka.
“Ni bora wakawa hawaniamini,” Miranda akajibu, “Kuliko wakawa hawajui linaloendelea.”
Akavuta hewa na kusema, “Kama hawajui linaloendelea, basi kazi itakuwa kubwa sana kuliko tunavyowaza. Kazi kubwa kuliko tunavyoweza kuwaza, kwani watakuwa wametumwa watu wa kikosi kingine kuja kumaliza kazi.”
“Ni tofauti na wale?” Jona akauliza.
“Ni tofauti kama ardhi na mbingu,” Miranda akateta. “Na sasa ndo’ napoanza kupata majibu, kwa mujibu wa lile tukio, watakuwa ni watu hao ndiyo wamelifanya, hawa watu wa siri ambao inawezekana hata wenzao hawajui kama wapo nchini.”
“Kuna haja ya kuhofia kuhusu hilo?” Jona akauliza.
“Ipo!” Miranda akajibu akimtazama. “Jona, watu hawa ni wachawi.”
“Wachawi? - Kivipi? Unamaanisha nini?”
***