*ANGA LA WASHENZI II --- 71*
*Simulizi za series*
ILIPOISHA
“Tutajaribu kadiri na uwezo wetu,” akasema Dkt Mahenge. “Ila kwa sasa, haraka iwezekanavyo, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupunguza pande la virusi linalotafuna mapafu na kuziba njia zake za fahamu. Baada ya hapo tutajua kama abakie hapa nchini ama aende nje kwa matibabu zaidi.”
“Dokta,” Waziri akaita kwa upole. “Kuna nafasi ya yeye kupona lakini?” akauliza.
ENDELEA
Dokta Mahenge akameza kwanza mate kisha akatikisa kichwa chake kuafiki, “Natumai atakuwa sawa. Tutafanya kadiri tunaloliweza arejee kwenye hali yake.”
Basi baada ya kusema vivyo, Daktari akaenda zake. Walikuwa ‘bize’ sana, kama unavyojua mgonjwa huyu hakuwa wa kawaida. Ni Raisi. Ni raia namba moja ndani ya nchi.
Madktari wote walikuwa kazi waliyo nayo mbele ni kubwa, si ya mchezo kabisa. Na huenda kazi hii inaweza kuwavumisha ama kuwayoyomesha kwenye medani hii. Madaktari hawa, wakiongozwa na Dkt Mahenge, walikuwa wamedhamiria kwenye hili. Walikuwa wanataka kuuonyeshea umma kuwa hata wataalamu ndani ya nchi wana uwezo mkubwa pia.
Hii ilikuwa ni nafasi yao adhimu. Lakini ilikuwa wazi kuwa mambo hayakuwa mepesi hata kidogo. Shughuli iliikuwa pevu haswa.
Basi usiku mzima, madaktari wakawa wanahangaika wakitumia maarifa yao yote kumwokoa mheshimiwa Raisi. Oparesheni ilidumu kwa masaa tisa, watu wakiwa nje wanangoja kwa hamu kubwa taarifa za chumba hicho. Watu hao wakiwamo familia ya Raisi, Waziri mkuu na pia makamu wa Raisi ambaye alifika papo, pia maafisa kadhaa na wafanyakazi wengine wakubwa wa serikali.
Walikuwa wanapeana habari na simulizi za hapa na pale juu ya mambo yalivyokuwa yametukia. Ilikuwa ni simulizi ya kuogofya haswa ambayo hakuna hata mtu aliyewahi kuwaza kuwa siku moja mbele ya macho yake atashuhudia Raisi kufanyiwa jaribio la kuuawa tena wavamizi ambao walidiriki kuivamia ngome yake kuu.
Ni wakina nani hao, wametumwa na nani? Na nini walikuwa wanakitaka kwa Raisi? Kumshambulia Raisi ni kuishambulia nchi nzima!
“Mmewatambua watu hao?” akauliza makamu wa Raisi, bwana Mrutu. Uso wake mnene mweusi wenye vioo vyembamba vya macho ulikuwa umefumwa kwa hofu na mkanganyiko.
“Bado,” akajibu Mkuu wa idara ya Usalama wa taifa, bwana Jovetic Holombe. “Ila tutajua tu ndani ya muda, vijana wanaifanyia kazi.”
“Ila unahisi ni wakina nani?” akauliza makamu wa Raisi. Mara Waziri mkuu naye akasonga karibu.
“Makisio ni mengi, mheshimiwa. Naomba mtupatie muda tutatoa majibu ya uhakika, ila tu kitu nachoweza kusema kwa sasa ni kuwa watu hawa watakuwa ni makomando kabisa maana ni watu wenye ujuzi mkubwa sana. Lazima watakuwa wametumwa na watu wenye maslahi mapana.”
Haikupita muda wakapata taarifa kuwa wanajeshi wale waliowafukuzia wale wavamizi wameuawa na wengine wapo majeruhi hawajiwezi. Na kama haitoshi, boti ya maafisa wa jeshi la majini imekombwa na kuwatorosha wavamizi. Habari hizi zilitolewa na mkuu wa kamandi hiyo.
***
Saa kumi na mbili asubuhi, Bagamoyo …
Maafisa wanne wa polisi walikuwa ufukweni wakipulizwa na pepo ya bahari. Wawili walikuwa wamebebelea bunduki mikononi na wamevalia sare. Wawili wengine walikuwa wamevalia nguo za raia ila mmoja ndiye aliyebebelea silaha miongoni mwao.
Huyu ambaye hajabebelea silaha, alikuwa ameshikilia ‘radio call’ mkono wake wa kuume. Alikuwa anaongea na radio call hiyo akiwa amekunja ndita, sura ya kazi. Sauti yake ilikuwa kavu na yenye ‘punch’ ya juu.
Mbali na maafisa hawa wa jeshi la polisi, kwa upande wao wa magharibi, kulikuwa na boti nyeupe ikiwa inaeleaelea. Boti hiyo, kwa ubavu wake wa kushoto, ilikuwa na chapa ya jeshi, kamandi ya maji. Pasi na shaka ndiyo ile iliyowatorosha wavamizi.
“... ndiyo, afande …” aliteta yule afisa polisi mwenye radio call. “…sawa, afande, nimekupata vema, over!” akashusha chini mkono wake wenye kifaa cha mawasiliano kisha akawatazama wenzake na kuwapasha agizo walilopewa.
“Watu hawa inabidi wapatikane. Naamini bado watakuwa ndani ya Bagamoyo hii. Vituo vyote vipewe taarifa hii na askari wote wafanye kazi hii leo hii.”
Habari hii haikuwa nyepesi kabisa. Bagamoyo ni mojawapo ya eneo la kitalii. Wazungu wamejaa hapa wakizunguka kwenye fukwe, wakijilaza kwenye vitanda vya mabwawa ya kuogelea, ama wakifurahia huko kwenye vivutio mbalimbali.
Kumtafuta mzungu mtuhumiwa ndani ya eneo hili haikuwa rahisi, achilia mbali ukubwa wa eneo.
Basi kwakuwa jambo hili lilikuwa zito, maafisa wa jeshi la polisi, wanajeshi na maafisa wa usalama wa taifa walishirikiana kulitekeleza. Walisambaa huku na huko, wengine wakiwa wamevalia nguo za kiraia kuchangamana na watu.
Vyombo vya usafiri vikawa vinasimamishwa na kukaguliwa kabla ya kutoka ndani ya Bagamoyo. Huko baharini, boti za wanausalama zinazungukazunguka kufanya doria. Na hata baadhi ya hoteli zikawa zinavamiwa na wana usalama, wageni wote wanakaguliwa.
Msako huu ulikuwa mkali haswa. Uliwapa hofu raia waishio eneo hilo, lakini zaidi wageni ambao huenda wengine walikuja nchini kutokana na sifa walizosikia kuwa mahali hapa ni kisiwa cha amani. Sasa mambo yalikuwa yanageukia mbele ya macho yao.
Kwenye majira ya saa nne asubuhi, taarifa ndipo zikaanza kuvuma sasa kuwa Ikulu ilivamiwa na Raisi yupo hoi hospitalini. Sauti ya makamu wa Raisi ilisikika redioni na sura yake ikaonekana kwenye televisheni kutangaza habari hiyo iliyowashtua watu haswa!
“ ... Mpaka sasa wana usalama wanafanya kazi yao kuwatafuta wadhalimu waliohusika na tukio hilo. Natoa rai kwa wananchi wote, tuungane kwenye hili, kutoa taarifa zozote zitakazosaidia upatikanaji wa wahalifu hao. Pia tumweke Raisi wetu kwenye maombi ya salama. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.”
Taarifa hizo zikazua soga kila mahali ambapo watu walikutana. Si kwenye daladala, ofisini wala vijiweni, hiyo ndiyo ikawa habari kuu! Watu wakijiuliza na wengine wakibashiri nani atakayekuwa anahusika na tukio hilo kubwa kabisa kuwahi tokea tangu nchi ipate uhuru.
Basi mambo yakaendelea kuwa katika hali hii ya homa ya matumbo. Ilipofika kwenye majira ya saa saba, kwenye hoteli moja kubwa, jina kapuni, inayopakana na bahari huko katika mji wa Bagamoyo, ikasikika sauti ya risasi! Ikachukua tena dakika moja, ikasikika sauti nyingine ya risasi, tena na kisha tena!
Mara sauti za kilio zikasikika, na ndani ya dakika moja tu baada ya sauti hizo za risasi, gari moja ya Tour, Toyota Landcruiser Safari, ikatoka kwa fujo na kuvamia geti! Likiwa kwenye mwendo kasi, likadaka lami! Kwa pupa likakimbia likitawala barabara yote.
Lilipokaa sawa, likatimka haswa na kuzua tafrani kubwa. Wanausalama wakapeana taarifa ndani ya eneo zima la Bagamoyo, na magari matano yakaungia kulifukuzia kwa nyuma.
Wanausalama waliamini ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wanaowahitaji hivyo kwa hali na mali ilibidi wawatie nguvuni. Hata vyombo va habari navyo vikaanza kurusha taarifa kuwa jeshi la polisi, kwa muda huo, lilikuwa njiani kufukuzana na watuhumiwa.
Basi gari lile, Toyota Landcruiser Safari, likaendelea kukimbia sana. Ni kama robo saa tangu likae barabarani tangu kukwapuliwa kwake likiwa linatafuta njia ya kutokomea toka Bagamoyo. Likiwa linakaribia kutimiza adhma yake, mara matairi yakapasuka baada ya kutwangwa risasi!
Matairi ya nyuma yakawa bazoka. Gari likaanza kuyumba, kwenda mrama! Halijakaa vema, matairi ya mbele nayo yakapasuka, sasa gari likayumba kupita kiasi, hatimaye likapinduka likibiringita mara nne na kisha kutulia. Wanausalama wakalizingira wakiwa wamelijalia silaha.
Walipotazama ndani, wakamwona mzee mmoja wa kizungu akiwa anavuja damu lukuki. Hata hakukaa vema, mzee huyo akakata pumzi. Kusaka ndani ya gari, hakukuwa na mtu mwingine yeyote. Ila kulikuwa na simu iliyopo ‘on’.
Wakaichukua simu hiyo na kuongea kujua nani aliyekuwa anaongea na mzee huyo kabla hajafa. Walichoambulia,
“You are too stupid to catch us. Mind your president!” kisha simu ikakata. Baadae walipokuja kufanya mchakato wa kujua simu hiyo ilikuwa inapigwa tokea wapi, wakaja ipata kandokando mwa bahari.
Na kumbe yule mzee alipewa agizo la kukimbiza gari kwa ajili ya kunusuru familia yake, mke na watoto wake watatu, waliokuwa wametekwa na wavamizi wa Ikulu, yaani bwana Denmark na mweziwe. Na asingeweza kudanganya kwani wavamizi hao waliifungia gari ‘tracking’, na huku wakimpa fursa ya kuwasiliana na watoto wake waliokuwa wakilalamika kubonyezewa tundu za bunduki vichwani.
***
Saa kumi na mbili jioni …
Dkt Mahenge anaweka simu yake ya mezani chini na kumtazama Makamu wa Raisi aliyekuwa amejawa na hamu ya kusikia neno toka kwake. Akashusha pumzi kwanza kisha akakuna kichwa chake chenye upara.
“Mheshimiwa,” alafu akabinua mdomo wake. “Imeshindikana. Hamna namna, inabidi apelekwe nje kwa matibabu zaidi.”
Makamu akatikisa kichwa chake kwa masikitiko.
***
Baada ya masaa mawili, Uwanja wa ndege wa Julius K. Nyerere, Dar es salaam.
Ilikuwa ni jioni ya saa moja. Ndege kubwa ya AIR TANZANIA nambari B. 20BC348 ilikuwa inangurumisha injini zake. Feni zilizo mbawani zilikuwa zinachanganyia taratibu kuelekea kwenye kasi kubwa.
Punde kidogo ndege hiyo ikaanza kukaa tenge kwa ajili ya kupaa. Rubani alitoa maelekezo, tahadhari na pia taarifa kuwa ndege hiyo kituo chake cha kwanza itakuwa ni India moja kwa moja.
Ila rubani huyu aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Tolabora, alizingumza kutoa taarifa kwa lugha ya kiingereza pasipo kutia kiswahili kama ilivyozoeleka. Hili laweza likawa si tabu. Lakini lafudhi yake ilitia shaka. Ni wazi aliyekuwa anaongea hakuwa mswahili, alikuwa mzungu.
Hakukuwapo na hilo kwenye ratiba.
***
Kuna nini hapa? Wakina Jona wapo wapi?