Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI II --- 70*


*Simulizi za series*



ILIPOISHIA


Lakini hapahapa, tena ikiwa ni kama sekunde kadhaa tu toka wavamizi wawekwe chini ya ulinzi, vikasikika vishindo vya watu! Mara, “Wale pale!”


Risasi zikaanza kutupwa kwa fujo kuwalenga wavamizi pamoja na wale waliowaweka wavamizi chini ya ulinzi!


ENDELEA


Basi hapa ndiyo ikawa salama ya wavamizi. Kushambuliwa kwa pamoja na wale waliokuwa wamewaweka chini ya ulinzi kuliwafanya wote watafute upenyo wa kuokoa maisha yao. Kwahiyo basi wakajikuta wakitawanyika huku na kule.


Wakajikuta wote wakiwa watuhumiwa na wahanga wa risasi zilizokuwa zinamwagwa kama njugu, baada ya kama dakika tano mvamizi mmoja akawa yupo chini kwa kushindiliwa risasi, yule aliyekuwa amejeruhiwa wakati wanafanya jitihada za kuuvuka ukuta wa Ikulu. Wengine wawili wakawa wapo mbioni kutafuta usafiri mwingine wa ziada kuwatoa eneo la hatari.


Na wakati huo wakipambana kwa kurudisha majibu ya risasi walizokuwa wanarushiwa na wale wanajeshi waokozi.


Vita ilikuwa si ndogo. Wanajeshi waokozi walikuwa wengi na hivyo basi mashambulizi yao kuwa makubwa. Kwa muda wote huu wa mashambulizi, eneo lililo karibu la Ikulu lilikuwa limesimama kwa muda. Taharuki ilikuwa imetawala, hofu, vilio na watu kupatwa maruhani!


Eneo hili liligeuzwa kuwa uwanja wa vita ndani ya muda mfupi. Kwa watu wa nchi hii ikawa jambo la kushtusha sana, na habari hizi zikasambaa na kupamba moto huko kwenye mitandao ya jamii na kutengeneza hamu kubwa ya watu kutaka kujua kinachoendelea.


Basi wale wavamizi, wawili waliokuwa wamebaki hai, wakakimbilia baharini na kupoka boti ndogo ya mvuvi. Wakamteka mwenye nayo na kumweka chini ya ulinzi kisha wakawasha mashine na kutimka kuyakata mawimbi.


Muda mfupi kabla hawajatokomea kuacha ‘war zone’, boti zingine mbili, kubwa kuliko ya wavamizi, zikajiri zikiwa zinawafukuza kwa kasi. Mwendo wa boti hizo ulikuwa mkubwa sana, zilikuwa za kisasa na za kivita. Haikuhitaji ufahamu mkubwa kutambua kuwa zilikuwa za jeshi la wana maji.


Mbali na kuwafukuza wavamizi, walikuwa wakiwatupia risasi za moto kuwanyima nafasi ya kupanga mashambulizi ama kutimiza adhma ya kutoroka japokuwa risasi nyingi zilizama majini kuliko kudhuru.


Ndani ya boti hizo kulikuwa kuna kama wanajeshi kumi na mbili, sita kwenye kila mojawapo! Kulikuwa kuna madereva na watu waliobaki wakifanya kazi za ushambulizi. Macho na akili zao zilikuwa zinafanya kazi, huenda, kwa hatua yao ya juu kabisa. Lengo hapa lilikuwa ni kuhakikisha wavamizi hawafanikiwi kuponyoka mkono wa dola.


Basi wakazidi kuwafukuzia na kuwafukuzia. Na kwakuwa boti zao zilikuwa za kisasa zaidi, zilikata mawimbi na kupambana na nguvu ya bahari inavyotakiwa hivyo wakazidi kuwasogelea walengwa wao. Zaidi … zaidi … na zaidi!


Mara …


“Acha kufyatua! Acha kufyatua!” amri ilisikika toka kwa mkubwa wa kikosi, wakiwa sasa wameshaisogelea kwa ukaribu mno boti ya wavamizi.


Ajabu ni kwamba, boti hiyo ya wavamizi ilikuwa bado yayoyoma, mashine yafanya kazi, ila ndani ni kama vile kulikuwa na mtu ambaye hakuwa anatikisika, mtu kama sanamu!


Basi wanajeshi walipogundua hilo wakapatwa na kiwewe. Walipoangaza vema, wakagundua mtu huyo alikuwa amekufa. Na hata hakuwa mvamizi bali mvuvi tu. Hapa wakajita, japo walifanya jitihada, bado wavamizi walikuwa wametoroka!


“Huenda tukawa tumewaua!” Hoja hii kidogo ikaleta mashiko, lakini ikawapunguziia machungu wanajeshi wale dhidi ya kuonekana wamefanya kazi ya kutwanga maji kinuni.


Ila kwa kamanda wa kikosi bado hakuwa ameridhia na hili.


“Tafuteni miili hiyo mpaka pale itakapopatikana. Kinyume na hapo, tutakuwa tumefanya kazi ya kukimbiza pepo.”


Basi wakaanza kurandaranda huku na kule huku na kule kutafuta ushahidi wa miili kuthibitisha kuwa wamefanikiwa kuwamaliza wavamizi. Hawakuambulia chochote kwa masaa mawili.


“Wametoroka,” akasema kamanda wa kikosi. “Hata boti lao halina viashiria vyovyote mbali na huyu mvuvi waliyemuua!”


Habari hizi zikawa za simanzi. Punde, mwanajeshi mmoja akamwita kamanda na kumwambia kuna jambo wanahitaji alitupie macho. Basi kamanda akaitikia wito na kwenda mpaka kwenye kachumba kadogo ka boti hii ya kisasa ambayo nchi ilipatiwa kama msaada toka nchi zilizokwisha endelea. Kwenye kachumba hako kulikuwa kuna mifumo na mashine ya kusaidia mawasiliano. Kilikuwa ndiyo sehemu kitovu ya kupokea na kutuma mawasiliano ndani na hata nje ya boti ikiwa na uwezo mkubwa wa kutimiza majukumu yake hata maeneo ya mbali na yenye ufinyu wa mtandao.


Humo kulikuwa na watu wawili, mmoja wao alimwelekezea kamanda kwenye ‘screen’ ya ukubwa wa wastani iliyokuwa imepachikwa ukutani akamwambia,


“Wakati kurunzi inamulika mara ya kwanza, inaonyesha kulikuwa na watu. Unaweza ukawaona kwa mbali …”


Hapa kamanda akafinya macho yake kutazama.


“Lakini baada ya boti kukwepa kurunzi kwa muda wa dakika moja tu, hawakuonekana tena!” mwanajeshi alitoa maelezo kamanda akitazama kwa umakini.


“Ebu rudisha hiyo video nyuma,” kamanda akaagiza. Video iliporejeshwa, akaitazama kwa ukaribu zaidi. Hapa akagundua jambo. Si kwamba wavamizi walikuwa wamepotea baada ya kurunzi la boti yao kwenda kombo, bali watu wao walitoroka mapema zaidi.


Walikuwa wamechezewa akili. Na muda wote ule wakidhani wanawakimbiza wavamizi, walikuwa tayari wamejitosa kwenye maji wakiacha nyavu na vifaa vya mvuvi pamoja pia na mwili wake katika namna kuwalaghai kuwa bado wapo botini.


Hapa kamanda akajiona mjinga sana. Ni kwa namna gani walikuwa wamefanywa kuwa watoto tena karibia na mbele ya macho yao. Lakini pia akawaza, watu hao, yaani wavamizi, watakuwa wameelekea pande ipi ya dunia, nchi kavu ama bado wapo majini?


Taarifa ikasambaa kwa vikosi vingine maeneo mbalimbali kufanya doria ya kuhakikisha wavamizi hao hawatoki salama kwenye pwani yote hii ya Afrika ya Mashariki.


Basi punde kidogo baada ya kufanya hivyo, boti ikatikisika kwanguvu kana kwamba imekumbwa na wimbi kali! Kufumba na kufumbua, ‘alarm’ kali ya hatari ikaanza kulia!


Duuiiiil! Duuiiil! Duuuiiil! Duuuiil! Duiiiil!


Haraka wahusika wakatazama kwenye ‘boat operation system’ kung’amua nini tatizo. Ajabu machoni mwao, wakaona boti yazama! Kando kidogo ya mashine ya kukatia maji kulikuwa na tundu kubwa ambalo laingiza maji ndani kwa fujo haswaa!


Hawajakaa vema, wakasikia milio ya risasi. Kutazama yatokea wapi, wakagundua ni kutoka kwenye boti mwenza. Risasi zilikuwa zinarushwa kwa fujo haswa. Zinapasua vioo na kutoboatoboa boti kuwa chujio.


Risasi hizi zikawanyima kabisaa wanajeshi hawa fursa ya kuikomboa boti yao inayozama kwa kuwafanyia wazingatie zaidi uhai wao dhidi ya ncha za risasi zilizokuwa zinarindima.


Mpaka zinakoma, boti ilikuwa imeshazama nusu na robo. Sehemu yote ya nyuma ilikuwa ndani ya maji. Boti yabinuka juu! Boti ile mwenza ikatokomea kama kishada.



***


Kwenye korido za hospitali …



Waziri mkuu anaingia, bwana Sospeter Mhenga. Ametoka kutumbukiza simu yake mfukoni muda si mrefu. Mwendo wake ni wa kasi na uso wake umepaliwa na mashaka. Kando yake anaongozana na ‘bodyguard’ wake lakini pia maafisa usalama wawili.


Baada ya muda mfupi akaonana na maafisa kadhaa waliokuwepo kwenye tukio, kisha daktari anayehusika, bwana Mahenge, ambaye aliyeongozana naye mpaka chumba alimolazwa Raisi.


Humo Waziri mkuu akapata shaka. Macho yake madogo yalitumbua ndani ya lenzi ya miwani.


“Atapoa kweli?”


Mheshimiwa Raisi alikuwa amezingirwa na mashine za kumsaidia kupumua na mashine za kumsaidia kusukuma mapigo yake ya moyo. Ndani ya chumba kulikuwa kuna milio ya ‘bip-bip’ ya mashine kadha wa kadha kumnusuru raia namba moja wa nchi.

Ngozi yake ilikuwa imebadilika rangi kueleka zambarau wakati lips na kope zake za macho zikiwa na rangi ya njano.


Waziri mkuu akaongozana na Daktari kutoka ndani ya chumba cha mgonjwa, koridoni wakakutana na familia ya Raisi, mke na mtoto wake mkubwa wa kiume. Wasitete sana, wakiwa katika hali ya haraka, Waziri mkuu akaongozana na Daktari mpaka ofisini kwake na kuketi.


“Hali yake ….” Dkt Mahenge akabinua mdomo, “… si nzuri kabisa. Amevuta sumu kali sana. Mapigo yake ya moyo yanapungua kadiri na muda, napata shaka kama mashine ile itasaidia kwa kitambo.”


“Kwahiyo tunafanyaje dokta kunusuru maisha yake?” akauliza Waziri akiwa na kimuhe.


“Tutajaribu kadiri na uwezo wetu,” akasema Dkt Mahenge. “Ila kwa sasa, haraka iwezekanavyo, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupunguza pande la virusi linalotafuna mapafu na kuziba njia zake za fahamu. Baada ya hapo tutajua kama abakie hapa nchini ama aende nje kwa matibabu zaidi.”


“Dokta,” Waziri akaita kwa upole. “Kuna nafasi ya yeye kupona lakini?” akauliza.




***
 
*ANGA LA WASHENZI II --- 71*


*Simulizi za series*



ILIPOISHA


“Tutajaribu kadiri na uwezo wetu,” akasema Dkt Mahenge. “Ila kwa sasa, haraka iwezekanavyo, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kupunguza pande la virusi linalotafuna mapafu na kuziba njia zake za fahamu. Baada ya hapo tutajua kama abakie hapa nchini ama aende nje kwa matibabu zaidi.”


“Dokta,” Waziri akaita kwa upole. “Kuna nafasi ya yeye kupona lakini?” akauliza.


ENDELEA


Dokta Mahenge akameza kwanza mate kisha akatikisa kichwa chake kuafiki, “Natumai atakuwa sawa. Tutafanya kadiri tunaloliweza arejee kwenye hali yake.”


Basi baada ya kusema vivyo, Daktari akaenda zake. Walikuwa ‘bize’ sana, kama unavyojua mgonjwa huyu hakuwa wa kawaida. Ni Raisi. Ni raia namba moja ndani ya nchi.


Madktari wote walikuwa kazi waliyo nayo mbele ni kubwa, si ya mchezo kabisa. Na huenda kazi hii inaweza kuwavumisha ama kuwayoyomesha kwenye medani hii. Madaktari hawa, wakiongozwa na Dkt Mahenge, walikuwa wamedhamiria kwenye hili. Walikuwa wanataka kuuonyeshea umma kuwa hata wataalamu ndani ya nchi wana uwezo mkubwa pia.


Hii ilikuwa ni nafasi yao adhimu. Lakini ilikuwa wazi kuwa mambo hayakuwa mepesi hata kidogo. Shughuli iliikuwa pevu haswa.


Basi usiku mzima, madaktari wakawa wanahangaika wakitumia maarifa yao yote kumwokoa mheshimiwa Raisi. Oparesheni ilidumu kwa masaa tisa, watu wakiwa nje wanangoja kwa hamu kubwa taarifa za chumba hicho. Watu hao wakiwamo familia ya Raisi, Waziri mkuu na pia makamu wa Raisi ambaye alifika papo, pia maafisa kadhaa na wafanyakazi wengine wakubwa wa serikali.


Walikuwa wanapeana habari na simulizi za hapa na pale juu ya mambo yalivyokuwa yametukia. Ilikuwa ni simulizi ya kuogofya haswa ambayo hakuna hata mtu aliyewahi kuwaza kuwa siku moja mbele ya macho yake atashuhudia Raisi kufanyiwa jaribio la kuuawa tena wavamizi ambao walidiriki kuivamia ngome yake kuu.


Ni wakina nani hao, wametumwa na nani? Na nini walikuwa wanakitaka kwa Raisi? Kumshambulia Raisi ni kuishambulia nchi nzima!


“Mmewatambua watu hao?” akauliza makamu wa Raisi, bwana Mrutu. Uso wake mnene mweusi wenye vioo vyembamba vya macho ulikuwa umefumwa kwa hofu na mkanganyiko.


“Bado,” akajibu Mkuu wa idara ya Usalama wa taifa, bwana Jovetic Holombe. “Ila tutajua tu ndani ya muda, vijana wanaifanyia kazi.”


“Ila unahisi ni wakina nani?” akauliza makamu wa Raisi. Mara Waziri mkuu naye akasonga karibu.


“Makisio ni mengi, mheshimiwa. Naomba mtupatie muda tutatoa majibu ya uhakika, ila tu kitu nachoweza kusema kwa sasa ni kuwa watu hawa watakuwa ni makomando kabisa maana ni watu wenye ujuzi mkubwa sana. Lazima watakuwa wametumwa na watu wenye maslahi mapana.”


Haikupita muda wakapata taarifa kuwa wanajeshi wale waliowafukuzia wale wavamizi wameuawa na wengine wapo majeruhi hawajiwezi. Na kama haitoshi, boti ya maafisa wa jeshi la majini imekombwa na kuwatorosha wavamizi. Habari hizi zilitolewa na mkuu wa kamandi hiyo.



***


Saa kumi na mbili asubuhi, Bagamoyo …



Maafisa wanne wa polisi walikuwa ufukweni wakipulizwa na pepo ya bahari. Wawili walikuwa wamebebelea bunduki mikononi na wamevalia sare. Wawili wengine walikuwa wamevalia nguo za raia ila mmoja ndiye aliyebebelea silaha miongoni mwao.


Huyu ambaye hajabebelea silaha, alikuwa ameshikilia ‘radio call’ mkono wake wa kuume. Alikuwa anaongea na radio call hiyo akiwa amekunja ndita, sura ya kazi. Sauti yake ilikuwa kavu na yenye ‘punch’ ya juu.


Mbali na maafisa hawa wa jeshi la polisi, kwa upande wao wa magharibi, kulikuwa na boti nyeupe ikiwa inaeleaelea. Boti hiyo, kwa ubavu wake wa kushoto, ilikuwa na chapa ya jeshi, kamandi ya maji. Pasi na shaka ndiyo ile iliyowatorosha wavamizi.


“... ndiyo, afande …” aliteta yule afisa polisi mwenye radio call. “…sawa, afande, nimekupata vema, over!” akashusha chini mkono wake wenye kifaa cha mawasiliano kisha akawatazama wenzake na kuwapasha agizo walilopewa.


“Watu hawa inabidi wapatikane. Naamini bado watakuwa ndani ya Bagamoyo hii. Vituo vyote vipewe taarifa hii na askari wote wafanye kazi hii leo hii.”


Habari hii haikuwa nyepesi kabisa. Bagamoyo ni mojawapo ya eneo la kitalii. Wazungu wamejaa hapa wakizunguka kwenye fukwe, wakijilaza kwenye vitanda vya mabwawa ya kuogelea, ama wakifurahia huko kwenye vivutio mbalimbali.


Kumtafuta mzungu mtuhumiwa ndani ya eneo hili haikuwa rahisi, achilia mbali ukubwa wa eneo.


Basi kwakuwa jambo hili lilikuwa zito, maafisa wa jeshi la polisi, wanajeshi na maafisa wa usalama wa taifa walishirikiana kulitekeleza. Walisambaa huku na huko, wengine wakiwa wamevalia nguo za kiraia kuchangamana na watu.


Vyombo vya usafiri vikawa vinasimamishwa na kukaguliwa kabla ya kutoka ndani ya Bagamoyo. Huko baharini, boti za wanausalama zinazungukazunguka kufanya doria. Na hata baadhi ya hoteli zikawa zinavamiwa na wana usalama, wageni wote wanakaguliwa.


Msako huu ulikuwa mkali haswa. Uliwapa hofu raia waishio eneo hilo, lakini zaidi wageni ambao huenda wengine walikuja nchini kutokana na sifa walizosikia kuwa mahali hapa ni kisiwa cha amani. Sasa mambo yalikuwa yanageukia mbele ya macho yao.


Kwenye majira ya saa nne asubuhi, taarifa ndipo zikaanza kuvuma sasa kuwa Ikulu ilivamiwa na Raisi yupo hoi hospitalini. Sauti ya makamu wa Raisi ilisikika redioni na sura yake ikaonekana kwenye televisheni kutangaza habari hiyo iliyowashtua watu haswa!


“ ... Mpaka sasa wana usalama wanafanya kazi yao kuwatafuta wadhalimu waliohusika na tukio hilo. Natoa rai kwa wananchi wote, tuungane kwenye hili, kutoa taarifa zozote zitakazosaidia upatikanaji wa wahalifu hao. Pia tumweke Raisi wetu kwenye maombi ya salama. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.”


Taarifa hizo zikazua soga kila mahali ambapo watu walikutana. Si kwenye daladala, ofisini wala vijiweni, hiyo ndiyo ikawa habari kuu! Watu wakijiuliza na wengine wakibashiri nani atakayekuwa anahusika na tukio hilo kubwa kabisa kuwahi tokea tangu nchi ipate uhuru.


Basi mambo yakaendelea kuwa katika hali hii ya homa ya matumbo. Ilipofika kwenye majira ya saa saba, kwenye hoteli moja kubwa, jina kapuni, inayopakana na bahari huko katika mji wa Bagamoyo, ikasikika sauti ya risasi! Ikachukua tena dakika moja, ikasikika sauti nyingine ya risasi, tena na kisha tena!


Mara sauti za kilio zikasikika, na ndani ya dakika moja tu baada ya sauti hizo za risasi, gari moja ya Tour, Toyota Landcruiser Safari, ikatoka kwa fujo na kuvamia geti! Likiwa kwenye mwendo kasi, likadaka lami! Kwa pupa likakimbia likitawala barabara yote.


Lilipokaa sawa, likatimka haswa na kuzua tafrani kubwa. Wanausalama wakapeana taarifa ndani ya eneo zima la Bagamoyo, na magari matano yakaungia kulifukuzia kwa nyuma.


Wanausalama waliamini ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wanaowahitaji hivyo kwa hali na mali ilibidi wawatie nguvuni. Hata vyombo va habari navyo vikaanza kurusha taarifa kuwa jeshi la polisi, kwa muda huo, lilikuwa njiani kufukuzana na watuhumiwa.


Basi gari lile, Toyota Landcruiser Safari, likaendelea kukimbia sana. Ni kama robo saa tangu likae barabarani tangu kukwapuliwa kwake likiwa linatafuta njia ya kutokomea toka Bagamoyo. Likiwa linakaribia kutimiza adhma yake, mara matairi yakapasuka baada ya kutwangwa risasi!


Matairi ya nyuma yakawa bazoka. Gari likaanza kuyumba, kwenda mrama! Halijakaa vema, matairi ya mbele nayo yakapasuka, sasa gari likayumba kupita kiasi, hatimaye likapinduka likibiringita mara nne na kisha kutulia. Wanausalama wakalizingira wakiwa wamelijalia silaha.


Walipotazama ndani, wakamwona mzee mmoja wa kizungu akiwa anavuja damu lukuki. Hata hakukaa vema, mzee huyo akakata pumzi. Kusaka ndani ya gari, hakukuwa na mtu mwingine yeyote. Ila kulikuwa na simu iliyopo ‘on’.


Wakaichukua simu hiyo na kuongea kujua nani aliyekuwa anaongea na mzee huyo kabla hajafa. Walichoambulia,


“You are too stupid to catch us. Mind your president!” kisha simu ikakata. Baadae walipokuja kufanya mchakato wa kujua simu hiyo ilikuwa inapigwa tokea wapi, wakaja ipata kandokando mwa bahari.


Na kumbe yule mzee alipewa agizo la kukimbiza gari kwa ajili ya kunusuru familia yake, mke na watoto wake watatu, waliokuwa wametekwa na wavamizi wa Ikulu, yaani bwana Denmark na mweziwe. Na asingeweza kudanganya kwani wavamizi hao waliifungia gari ‘tracking’, na huku wakimpa fursa ya kuwasiliana na watoto wake waliokuwa wakilalamika kubonyezewa tundu za bunduki vichwani.



***


Saa kumi na mbili jioni …


Dkt Mahenge anaweka simu yake ya mezani chini na kumtazama Makamu wa Raisi aliyekuwa amejawa na hamu ya kusikia neno toka kwake. Akashusha pumzi kwanza kisha akakuna kichwa chake chenye upara.


“Mheshimiwa,” alafu akabinua mdomo wake. “Imeshindikana. Hamna namna, inabidi apelekwe nje kwa matibabu zaidi.”


Makamu akatikisa kichwa chake kwa masikitiko.



***


Baada ya masaa mawili, Uwanja wa ndege wa Julius K. Nyerere, Dar es salaam.



Ilikuwa ni jioni ya saa moja. Ndege kubwa ya AIR TANZANIA nambari B. 20BC348 ilikuwa inangurumisha injini zake. Feni zilizo mbawani zilikuwa zinachanganyia taratibu kuelekea kwenye kasi kubwa.


Punde kidogo ndege hiyo ikaanza kukaa tenge kwa ajili ya kupaa. Rubani alitoa maelekezo, tahadhari na pia taarifa kuwa ndege hiyo kituo chake cha kwanza itakuwa ni India moja kwa moja.


Ila rubani huyu aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Tolabora, alizingumza kutoa taarifa kwa lugha ya kiingereza pasipo kutia kiswahili kama ilivyozoeleka. Hili laweza likawa si tabu. Lakini lafudhi yake ilitia shaka. Ni wazi aliyekuwa anaongea hakuwa mswahili, alikuwa mzungu.


Hakukuwapo na hilo kwenye ratiba.




***


Kuna nini hapa? Wakina Jona wapo wapi?
 
Aisee. Na leo tena mkuu, ili tujue hao akina jona na na kina nanii wako wapi.
 
Aisee ,mpaka natamani nipitishe kamchango hapa jamvini, tuchangie stivu afanye mchakato wa kuifanya kuwa the real movie
 
Back
Top Bottom