*ANGA LA WASHENZI --- 39*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Geti likafunguliwa, na akastaajabu kuona gari aina ya Murrano nyeupe ikiingia ndani. Kutazama, akamwona mke wa Boka akishuka toka kwenye gari hilo, akamtazama kwa tabasamu akimpungia mkono.
Kichwani akajiuliza mwanamke huyu ametokea wapi? Kwa namna moja akahisi pengine ndiye aliyekuwa anatumia simu ya mumewe, Boka, kumtumia ujumbe. Basi akawa na hofu.
Lakini wakati mama huyo anamjongea akiwa anatabasamu, simu yake ikaingia ujumbe. Akatazama upesi. Ulikuwa unatoka kwa Boka.
‘Nakaribia kufika.’
Moyo wa Miranda ukapasuka pah!
ENDELEA
Kwahiyo Boka na mkewe hawakuwa wanajua kama wanakutana sehemu moja! Miranda akajua hilo. Sasa afanyaje? Japokuwa alimpokea mke wa Boka na kumkarimu kwa tabasamu matata, akili yake haikuwa pale kabisa.
Haraka alitumikisha vidole vyake kuandika ujumbe na kuutuma. Akimtaarifu Boka juu ya ujio wa mumewe eneo hilo. Kama haitoshi, pengine kwa kuhofia Boka anaweza akawa hajaupata ujumbe huo, akaibipu simu yake kumtaarifu.
Boka akatazama simu yake akikunja uso. Kiooni akaona ujumbe toka kwa Miranda. Ila kabla hajaufungua ujumbe huo, dereva akawa tayari ameshapiga honi mara tatu getini! Na kwakuwa mlinzi alikuwa na taarifa juu ya ujio huo, haraka akafungua geti.
“Simama!” Boka akampiga dereva begani. “Rudi haraka, tuondoke hapa!” Dereva hakuelewa kinachoendelea. Alipigwa na butwaa, ila kutii amri ya bosi akarudisha gari nyuma upesi, na kuligeuza. Alidhani pengine itakuwa ni kuhusu mambo ya usalama. Wakayoyoma.
Lakini mama Boka akahisi jambo. Akauliza:
“Nimeona kama gari ya mume wangu,” alisema akitazama nje kupitia dirishani. Miranda akaigiza kushtukiza. Mama akanyanyuka na kwenda nje. Akaangaza pasipo mafanikio kwani geti lilikuwa limefungwa.
“Hamna kitu, mama! Utakuwa umeona vibaya,” akasema Miranda akitabasamu kiuongo.
“Hapana, sidhani. Nimefikia uzee huo!”
Basi Miranda kumaliza zogo akamwita mlinzi aliyemkonyeza tayari kwa ishara. Akamuuliza eti ni nani yule aliyekuja na kuondoka, kwanini ameondoka, na alikuwa anataka nini?
“Aaah Madam, ni Kinoo yule!” Mlinzi akasema akijichekesha. “Amesema kuna kitu alikuwa anakuletea ila sasa bahati mbaya amekisahau?”
“Kwahiyo ndo’ ameenda kukichukua?”
“Eeeenh! Ndo maana nikaona hamna hata haja ya kuja kukwambia huku … anaweza akarudi muda si mrefu.”
Angalau Mama Boka akawa ametuliza kifua. Wakarejea ndani na kueleza lile lililonyanyua mguu wake kumleta hapo.
“Samahani sana, najua nimekuja kwa kukushtukiza. Nilikuwa njiani kuelekea City mall, nikaona kuna haja kama nikikatiza hapa maana nina habari za kupasua kifua.”
Akaweka kituo akimeza mate.
“Kuna kampuni kubwa sana ya usambazaji ya huko nchini Kenya, wamevutiwa na kazi zetu na hivyo basi wanataka tuwe na ubia. Maana yake ni kwamba, bidhaa zetu sasa zitavuka mipaka na kwenda Kenya kwa uhakika!”
“Habari nzuri sana hizo!” Miranda akatahamaki. Ila kinafki. Hakuna wazo lake lolote lililokuwa pale. Alikuwa anamuwaza Boka. Namna alivyomkosa. Akijipa moyo ni kukuwe na hana haja ya kumshikia manati.
Ila alikuwa anataka kumaliza kazi. Huyu kuku atakaa nje ya banda kwa muda gani? Basi mawazo hayo yakapeleka mbali kichwa chake, yale aliyokuwa anayaongea Mama Boka kwake yakawa kama kelele za chura. Alichokuja kusikia mwishoni ni kile cha kuambiwa lazima interview yake ifanyike kesho kutwa.
“… Tutakapofanya hicho kitu, hapo ndo’ tutaeleza pia umma kwamba kampuni yetu imetanuka na sasa imefika Kenya.”
Akaitikia: “Sawa.”
Na hata hivyo vingine vyote vilivyofuatia, akamkubalia pasipo shida. Alikuwa anataka mama huyo aondoke amwache huru, haikupita muda akaaga na kwenda. Kitu cha kwanza ambacho Miranda alifanya ni kuchukua simu yake na kumtumia ujumbe Boka.
‘Ameondoka.’
Boka akamjibu baada ya muda mfupi:
‘Tutaonana siku nyingine mpenzi. Usijali.’
***
Saa tano usiku …
“Sasa Mustapha? – nataka kuondoka,” akasema Glady. Alikuwa amevalia bukta fupi rangi ya pinki na kaushi nyeupe nyepesi. Hakuwa amevalia sidiria, na hivyo basi chuchu zake zilikuwa zinaonekana vema zikitoboa kaushi. Miguuni alikuwa amevalia raba nyeupe – converse, mkononi akibebelea mkoba mkubwa mweusi.
“Sawa, we nenda tu,” Mustapha akajibu. Alikuwa ameketi kitandani nyayo zake zikigusa sakafu. Glady akacheka.
“Unajua unachekesha we Mustapha. Niende wapi na wewe umetuama humu? Au mpaka nikuambie amka uende mie nataka kufunga chumba?”
Mustapha akawa kimya kwanza. Sijui akitafakari nini, akamtazama Glady kwa huruma akisema:
“Unajua mikasa yangu ndugu yangu, unadhani n’taenda wapi? Huko nje si salama kwangu,”
“Leo nimekuwa ndugu yako, Mustapha?” Glady akapiga kofi akiangua kicheko. “Kweli shida kirusi. Sasa na mimi chumba changu hakipo salama nikikuacha humu. Umesikia? Mie n’takufuga humu mpaka lini labda?”
“Naomba unihifadhi kwa leo tu,” Mustapha akanyenyekea. “Kesho n’tajua mie pa kuelekea.”
“Sasa Mustaphaa …” Glady akakaa kitandani na kumtazama Mustapha. “Mie nikienda nikapata danga langu huko, n’talipeleka wapi? Mfano halina chumba, au anataka tufanyie kwangu? Ntafanyaje?”
“Kwa leo tu, Glady.”
“Mustapha mie n’takula nini?”
Mustapha akazamisha mkono wake mfukoni, “Basi lala na mimi leo.” Akatoa shilingi alfu kumi na kumwonyeshea Glady. Glady akaangua kicheko kikali. Akakohoa mara kadhaa kabla hajatulia na kumtazama Mustapha kwa macho yake mekundu.
“Mustapha, yani ulale na mimi kwa shing’ efu kumi!”
“Ntakupatia zingine bana, Glady. Mbona unakuwa kama hunijui? Unajua kabisa tukipiga ile hela na wewe utapata mgao au umesahau?”
“Mustapha, mie sio mtoto, sawa?” alisema Glady akiweka pesa yake kwenye mkoba. “Kwanza sasa hivi hakuna cha dili wala nini, ona unavyohangaika hangaika hapa kama digidigi. Pili, hii … hii pesa hii … haiwezi kun’tosha kabisaa! Hii ni pesa niliyolipwa kwa busu tu, upo? … cha kukusaidia, ntakuacha ulale humu, ila haiwezi kun’fanya nikabakia nyumbani.”
Hata hivyo Mustapha akashukuru, Glady akahepa. Alichukua bodaboda mpaka maeneo ya klabu ya usiku, Maasai, akaanza kufanya doria huko akichangamana na wenzake.
Baada ya robo saa …
“Shosti, yule siyo mchina wako uliyeenda naye siku ile?” alisema mwanamke mmoja kandokando ya Glady. Mwanamke huyu alikuwa amevalia topu na sketi fupi. Ilikuwa ngumu kujua rangi ya nguo hizo kwasababu ya ufinyu wa mwanga wa wingi wa taa za rangi rangi zilizokuwa zinakatiza zikienda huku na huko kwa kukimbizana.
Glady alitazama kule alipoelekezwa, kaunta, akamwona Lee! Mwanga uliokuwepo maeneo hayo ya kaunta uliwawezesha kuona vema.
“Au nimekosea?”
“Wala! Ndiye yeye. Acha niende,” akasema Glady akichukua hatua kwa mwendo wake wa madaha.
Lee alikuwa ameketi na marafiki zake, wakina Nigaa, wakipata kinywaji. Kila mtu alikuwa ameshikilia glasi ama chupa yenye kileo. Walikuwa wanasindikizia vinywaji vyao na soga za hapa na pale pamoja na cheko.
Mara Lee akasikia mkono begani, kutazama akamwona mwanamke ambaye kwa haraka alimtambua kama malaya. Akampuuzia akimshukuru na kumwambia ahitaji huduma.
“Ni mimi, unanikumbuka?” Glady alisema kwa sauti ya kubana pua. Hapo ndiyo Lee akatazama na kumgundua sasa Glady. Akamuuliza anataka nini?
“Naweza nikaongea na wewe kidogo?” Glady alisema kwa unyenyekevu.
“Glady, sihitaji usumbufu, sawa?”
“Ni jambo la muhimu, naomba unisikilize.”
Lee akageuka na kumtazama.
“Enhe, nini unataka kunambia?”
Glady akamwambia kumhusu Mustapha na matatizo yake. Yote yakisababishwa na ile nyaraka. Namna Mustapha alivyotaka kuitumia kupata pesa lakini mwisho wa siku ikamdumbukiza matatizoni, anawindwa anyofolewe roho!
Habari hizo zikamshtua Lee. Hakutegemea kama saga hili la nyaraka lilikuwa linaendelea katika ulimwengu huo ambao alidhani ameuacha. Lakini akajiuliza ni mchina gani huyo aliyepokea nyaraka hiyo na kuanza kumsaka?
Akamuuliza Glady:
“Unamjua mchina huyo? Unajua anakaa wapi?”
“Hapana, sijui lolote lile kumhusu.”
Lee akamtaka Glady waongozane mpaka kwa Mustapha. Lakini Glady akamuuliza:
“Sasa ukinitoa hapa, maana yake sitaingiza pesa yoyote. Vipi, utan’lipa?”
Lee akaukwapua mkono wa mwanamke huyo na kumswaga baada ya kuwatonya wenzake kwa ufupi ya kwamba anatoka.
“Taratibu basi jamaniii!” alisikika Glady akilalamika.
***
Saa saba kasoro usiku …
Kuna makelele makali ya muziki. Wanaume kadhaa pamoja na wanawake wapo ndani ya mahali hapa ambapo unaweza ukapaita klabu ya usiku, lakini ilikuwa ndani ya nyumba ya mtu! Ndani ya eneo hilo kulikuwa kuna kaunta, na eneo kubwa tu la watu kujimwaya kucheza muziki uliokuwa unapigwa.
Vinywaji vilikuwa vingi na vya kumwaga. Kila mtu aliyekuwa eneo hili alikuwa amebebelea kinywaji chake, haswa mvinyo ama whisky, katika mtindo wa chupa ama glasi. Na kila mtu alionekana akiwa na mtu wake.
Mwanga ulikuwa hafifu. Taa zilikuwa mbili tu, nyekundu na ya kijani. Wakati taa moja ikiwa inamulika kushoto, nyingine ilikuwa inamulika kulia. Kwahiyo ilikuwa ngumu kujua watu waliokuwemo humo kwa uso. Labda kwa maumbo.
Kulikuwa kuna milango miwili maeneo hayo, milango yote hii ikiwa ni ya kioo. Ukutani kulikuwa kumechorwa picha kadhaa za wanawake, maua na silaha.
Muziki ukiwa unaendelea kukonga nyoyo za watu, kama si vichwa, mlango mmoja ukafunguliwa na mwanaume fulani aliyekuwa amejaza mwili. Mwanaume huyu alitembea kwa kasi kuelekea meza fulani ukutani. Hapo akamnong’oneza mwenziwe sikioni.
Ghafla huyo aliyenong’onezwa akanyanyuka. Aliangaza kule kaunta akatoa ishara ya mkono, mara muziki ukakata! Akapaza sauti kusema wamevamiwa!
***