Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI -- 27*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Haraka akampekua Jona na kubeba bunduki yake kisha akamtaka asogee mbali na Miriam asogee upande wake haraka. Matukio hayo yakafanikiwa ndani ya muda mchache mno! Nade akatoka na Miriam ndani ya hoteli.

Wakajipaki ndani ya gari, wakayoyoma! Jona akawatazama namna wanavyoishilia. Akatabasamu na kusema:

“Kama ilivyopangwa.”

Nade pasipo kujua alikuwa ametanguliwa hatua mbili mbele.

ENDELEA

Jona alishatambua mpango wa Nade na alifahamu fika mwanamke huyo atakuwa karibu kwani amekuwa akimfuatilia kisirisiri kwa muda sasa.

Hivyo kila kitu alichokifanya alifanya akiwa amejiandaa na uvamizi ndani ya muda wowote ule. Na akajipanga kunufaika na uvamizi huo kwa kupandikiza 'application' katika simu ya Miriam itakayomsaidia kutambua wapi mwanamke huyo yupo na pia vile vile kumwezesha kusikia angalau sauti!

Kwahiyo kuondoka kwa Nade akiwa ameongozana na Miriam, kwa Jona ilikuwa ni mpango ulio kamilika.

Jona akiwa hapo amesimama na macho yake yakishuhudia gari la Nade likiyoyoma kwenda kujichoma, haraka ya punde toka upande wake wa kulia, nje ya uzio, akaona gari aina ya Altezza, ile ile ambayo ilihusika na tukio la kujaribu kummaliza, ikikatiza kwa mwendo pole na kioo cha upande wa dereva kikiwa kimefunguliwa.

Akatazama kwa ustadi na karibu zaidi, akamwona dereva akifichamua mkono wake wa kulia! Mara akatoa bunduki na kuonyeshea kule alipo Jona!

Haraka Jona akachumpa na kujikinga kwenye mojawapo ya magari yaliyokuwa yameegeshwa hapo uwanjani. Risasi tatu zikavuma! zikamkosa na kuishia kutoboa magari ya gharama kubwa yasiyo kuwa na makosa. Kisha gari la yule adui, ambaye ni wazi alikuwa ni Panky, likaongeza mwendo maradufu lipate kupotea tukioni!

Upesi Jona akakimbia kufuata uzio, akauruka kama kiunzi! Akasimama katikati ya barabara na kuzuia gari moja, Toyota Corola nyeupe, kwa ishara ya kunyanyua mkono, akaonyesha kitambulisho chake bandia cha polisi na kumwambia dereva:

"Nitahitaji gari lako kusaidia jeshi la polisi."

Akachumpa ndani ya gari na kulitimua mno kukimbiza gari lile Altezza. Mwendo wake ulikuwa mkubwa mno na hata akatanua kando ya barabara ili apate mwanya wa kujiachia zaidi.

Dereva wa hilo gari akahofia maisha yake. Aliogopa hata kutazama namna gari inavyoendeshwa kwa kushindwa kustahimili. Alitetemeka kwa kukutana na kifo uso kwa uso. Muda wote alikuwa analia gari ipunguzwe mwendo, huku Jona akimwambia hana haja ya kupata shaka!

Ndani ya muda mfupi, Jona akawa amejiweka usawa mzuri na lile Altezza anayoikimbiza. Sasa walikuwa wamefika Afrikana kuikuta barabara ya kutokea Bagamoyo kwenda katikati ya jiji.

Panky akakata kona kushika njia kuelekea Bagamoyo. Naye Jona akaunga mkia! Akamzidi maarifa Panky na kumsogelea karibu zaidi na zaidi. Sasa wakawa wamepeana ubapa.

Ila kichwani mwa Jona hakuwa amelenga kummaliza Panky. Alikuwa na uwezo kamili wa kupindua gari lake ila alimhitaji akiwa hai. Kifo chake kwake pia ingekuwa hasara.

Hivyo nini alichokuwa anakifanya? Kumpa presha zaidi Panky wamalize njia hii kukaribia kuitafuta Bagamoyo, kule ambapo magari si mengi. Yaani mbele kidogo, katikati ya Bunju na Bagamoyo.

Akafanikiwa janja hiyo lakini geji ya mafuta ya gari alilokuwa anatumia ikaonyesha mafuta yanaenda kukauka hivyo muda si mrefu sana chombo hicho kitakuwa na kiu ya kushindwa kufanya kazi!

Sasa ikabidi atumie nafasi hiyo kabla hajawa amepoteza muda wake bure.

Huu ukawa ni muda wa kumwonyesha na kumfunda Panky ujuzi wake kwenye uendeshaji wa vyombo vya moto. Akawasha 'full lights' kisha akakanyaga mafuta zaidi. Na kutokana na uhodari wake wa kukwepa magari, punde akawa beneti na adui!

Ndani ya muda mfupi, Jona akafanikiwa kumtoa Panky kwenye barabara ya lami kwa kumtishia kumparamia na gari. Kisha akageuza gari upesi na kukita mti fulani wa wastani kwa kutumia bodi ya nyuma ya gari, mti ukaangukia Altezza na kuibonyeza paa!

Panky akapoteza mwelekeo na kujikita kwenye chaka la miti. Akajeruhiwa kichwa na miguu. Alivuta hewa mara moja tu na mara Jona akawa amewasili!

Akamalizia kupasua kioo akafungua loki na kumtwaa Panky. Alikuwa hajiwezi, hoi asiyejitambua. Kichwa kilikuwa kinachuruzika damu. Macho yamemlegea!

Jona akamlaza chini baada ya kuhakikisha ameshabeba silaha ya adui, akafanya upekuzi wa haraka ndani ya Altezza alafu akayoyoma na Panky.

***

"Kuna kitu umeelewa?" Akauliza Miranda akimtazama Kinoo aliyekuwa ameketi kando yake. Wote mkononi walikuwa wamebebelea karatasi inayofanana. Ile yenye mchoro wa Bite ambao Jona aliwakabidhi.

Kinoo akatikisa kichwa. Hakuwa amepata kitu! Ni masaa sasa wamekuwa wakiichambua picha hiyo pasipo mafanikio. Sasa wakaona wanafanya kazi ya ubuyu.

"Tunafanyaje sasa?" Kinoo akauliza. Miranda akashusha kwanza pumzi na kuiweka kando karatasi apate kunywa sharubati yake ya embe. Akafikiri na akaona kuna haja ya kumshirikisha BC katika hilo, pengine anaweza akawa na maarifa.

Lakini Kinoo akamtaka awe mwangalifu.

"Hatujamshirikisha hili tangu mwanzo, huoni linaweza likatusababishia tafrani?"

Miranda akaona hoja ndani ya kauli ya Kinoo. Lakini wasipofanya hivyo itakuaje na ilhali vichwa vishagoma? Kinoo akapendekeza wajaribu zaidi na zaidi hata kama ikiwachukua mwezi.

Kwa sasa hakuna habari itakayokuwa njema kwa BC isipokuwa ya wao kufungua fumbo hilo.

"Nahofia yule mchoraji anaweza akang'amua hili kabla yetu," alisema Kinoo.

"Unadhani akigundua atafanya nini?" Miranda akawahi kuuliza, lakini kabla Kinoo hajajibu, mwenyewe akajipa maelezo.

"Alichokipata kinamtosha. Hatakiwi ajue zaidi ya hapo. Inabidi tukumbuke kwamba yule si mshirika wala mtu wetu."

Wakaona kuna haja ya kummaliza Jona punde tu watakapopata mchanganuo wa picha ile. Aidha utoke kwao ama kwa Jona mwenyewe.

Hakutakiwa kuwa hai baada ya hapo!

"Hakikisha leo unawasiliana naye kumuuliza kama amepata chochote," alisema Miranda.

"Unajua mimi siendani na yule lofa. Kwanini usifanye hiyo kazi wewe?" Kinoo akarusha mpira.

"Ningekuwa nina muda huo, nisingekusumbua. Ila nina appointment. Sidhani kama n'takuwa huru."

Ulikuwa umebakia muda mchache kwa Miranda kwenda kukutana na Boka - waziri wa Afya. Muda si mrefu aliwasiliana na mheshimiwa huyo wakapanga miadi ndani ya Kempinski hotel ndani ya majira ya jioni.

Alishamtaarifu BC na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa wao kutengeneza daraja la pili baada ya la sasa kupiga nyufa.

Kwahiyo karata ilibidi ichezwe vema!

---

Saa 1:12 jioni, Kempinski Hotel, Posta.

"I have already arrived," (tayari nimeshawasili) alisema Miranda kwa sauti ya puani. Alikuwa amejivika gauni moja matata sana! Rangi nyekundu lisilo na mabega likijishikiza kifuani mwake.

Hapo kifuani gauni hilo lilikuwa linametameta. likaenda moja kwa moja na mwili wake uliosimamisha nyonga na kudaka mapaja mpaka chini miguuni lilipojiachia.

Nywele zake zilikuwa zinawaka zikitiririkia mgongoni. Juu kidogo ya sikio la kushoto alikuwa amepachika ua dogo jekundu. Uso wake ulikuwa umekwatuliwa vizuri kwa viwango vya kimataifa!

Katika kijiwanja hicho cha kupata chochote kitu kilichomo ndani ya hoteli, hakuna aliyekuwa amependeza kama yeye.

Punde Boka akatokea. Hakupata shida kuangaza kwani Miranda alikuwa anang'aa. Akajisogeza taratibu akiwa anatabasamu. Nyuma yake alikuwa akiongozana na mlinzi.

Alikuwa amekula suti moja matata nyeusi toka Italia.

Akaomba radhi kwa kuchelewa. Akahisi moyo wake unakuwa wa baridi kila alimpotazama Miranda ambaye alijua kucheza na macho na tabasamu lake kumzizima mwanaume.

Boka akajikuta anatabasamu mara kwa mara. Akisisimkwa vinyweleo!

"Unajua mke wangu hajui juu ya hili kutano letu, na siku ukikutana naye usithubutu kumwambia," alisem Boka akitabasamu.

"Usijali, sijawa mjinga kiasi hicho," Miranda akamtoa hofu. Mhudumu akaja na kuwahudumia glasi mbili kubwa za juisi ya Raspberry.

Wakateta kidogo kukumbushiana ya tafrija ile iliyowakutanisha. Ila Boka akapata hamu ya kumjua yule mwanaume aliyekuwa ameongozana na Miranda siku ile, yani BC.

Miranda asifanye makosa akamwambia yule ni mlezi wake. Alimuasili na kumlelea tangu mtoto kwahiyo kwake anamuita baba.

Boka akafurahi na kushukuru kwa taarifa asijue Miranda alikuwa anatengeneza 'makao'. Akaanza kumpeleleza Miranda juu ya maisha yake ya mahusiano. Na Miranda kumridhisha akampatia majibu ambayo mwanaume huyo alikuwa anataka kuyasikia.

"Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa ni mtu toka France, lakini nilishindwana naye tabia. Ni mlevi sana na mtu asiye na 'future'. Nikapata mwingine lakini naye hayupo 'serious' so nikaona inabidi nitulie kwanza kabla ya kuzama tena uwanjani."

Basi Boka akafurahi mpaka jino la mwisho. Na pasipo kukawia akamtongoza Miranda. Kwanza Miranda akaigiza mshtuko ya kwamba hakuwahi kudhani kama kuna siku anaweza akapendwa na mtu 'mkubwa' vile.

Pili akaigiza uoga juu ya usalama wake kwa mke wa Boka ambaye anaonekana ni mjawa wa wivu. Boka akamtoa shaka.

"Hilo niachie mimi. Nikubalie uonje matunda ya nchi, mrembo."

Miranda, akiwa anaminyaminya lips na kuzimumunya, akaomba apewe muda kwani moyo wake uliojeruhiwa huko nyuma unahitaji kushirikisha akili yake kwanza.

"Kwahiyo mpaka lini mpenzi?"

"Nitakutaarifu."

Baada ya hapo wakateta kidogo juu ya mkewe Boka, Boka akimtaarifu Miranda kwamba mkewe anaweza kumtafuta muda si mrefu kwani alikuwaanamwongelea hivi karibuni.

Hawakukaa tena sana, wakaagana na kila mtu akaenda zake. Miranda akampigia simu BC na kumtaarifu vile mpango ulivyokwenda.

Yote yalikuwa mema!


***
 
Back
Top Bottom